Wednesday, May 8, 2013

Mnyika ataka ukaguzi miradi ya visima


JIBU LA SWALI LA MBUNGE UBUNGO
MBUNGE wa Ubungo, John Mnyika (CHADEMA), ameihoji serikali ni lini Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) itafanya ukaguzi wa kiufanisi wa miradi ya visima vya maji vilivyochimbwa na serikali na kukabidhiwa kwa Shirika la Majisafi na Majitaka (DAWASCO), jumuiya ya wananchi na taasisi mbalimbali lakini havitoi huduma inayostahili.
Pia mbunge huyo alitaka kujua ni lini serikali itawasilisha muswada wa sheria ya mabadiliko ya sheria mbalimbali za majisafi na majitaka, ili kushughulikia upungufu uliojitokeza katika utekelezaji wa sheria zilizopo na kuweka mfumo thabiti wa usimamizi wa sekta ya maji nchini.
Mnyika alihoji hatua hiyo bungeni jana alipouliza swali la msingi.
“Je, serikali imeweka mfumo gani kuhakikisha kwamba mpango maalumu wa 2011-2013 wa kuboresha huduma za majisafi na uondoshaji wa majitaka katika jijiji la Dar es Salaam uliopitishwa na Baraza la Mawaziri mwaka 2011 unatekelezwa kwa wakati na ufanisi kuwezesha mabomba yaliyopo yatoe maji na mtandao usambazwe mpaka maeneo ya pembezoni jimbo la Ubungo?” alihoji Mnyika.
Naibu Waziri wa Maji, Dk. Binilith Mahenge, akijibu swali hilo alisema wizara inatekeleza mpango maalumu wa kuboresha huduma ya majisafi na uondoshaji wa majitaka jijini Dar es Salaam kupitia Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (DAWASA).
Alisema katika kutekeleza mpango huo, serikali imeweka utaratibu wa usimamizi na ufuatiliaji wa karibu kwa kuzingatia hadidu za rejea zilizopo kwenye mikataba na ratiba za kazi.
Alisema vikao na ukaguzi wa miradi hufanywa kila mwezi kati ya wizara, Dawasa, Bodi ya Dawasa, makandarasi na wataalam washauri katika maeneo ya miradi, ili kudhibiti ubora na kuharakisha utekelezaji.
“Desemba mwaka 2012, EWURA ilifanya ukaguzi wa kiufanisi wa miradi ya visima vya maji 147 vilivyochimbwa na serikali chini ya usimamizi wa Dawasa,” alisema.
Alisema kati ya visima hivyo, visima 80 vilikutwa vinafanya kazi wakati 67 vilionekana kutofanya kazi.
“Sababu za visima hivyo kutofanya kazi ni pamoja na ubovu wa pampu, kuibiwa kwa pumpu, kupungua kwa wingi wa maji, kukauka kwa visima, kuwepo kwa madeni ya umeme na migogoro ya kijamii,” alisema Naibu Waziri huyo.
Alifafanua kuwa katika utekelezaji sheria za maji, wizara inaendelea kubaini mapungufu yaliyopo kwenye sheria za maji.

No comments:

Post a Comment