Baada ya Spika wa Bunge, Anne Makinda kutoa mwongozo na kuunga mkono uamuzi wa Naibu wake, Job Ndugai kuwasimamisha wabunge sita wa Chadema, wasomi, wanasiasa na wanaharakati wamesema Kiti cha Spika ndiyo chanzo cha mvutano bungeni kwa kuwa kinapendelea wabunge wa chama tawala (CCM).
Wamesema licha ya Bunge kuongozwa na kanuni, wakati mwingine viongozi hao wa Bunge wanatumia kanuni hizo kuwapendelea wabunge wa CCM, huku wakieleza kuwa licha ya wabunge wa chama hicho kutukana, hawakupewa adhabu yoyote.
Jumatano ya wiki hii, Ndugai aliwasimamisha Tundu Lissu (Singida Mashariki), Joseph Mbilinyi (Mbeya Mjini), Mchungaji Peter Msigwa (Iringa Mjini), Highness Kiwia (Ilemela), Ezekiah Wenje (Nyamagana) na Godbless Lema wa Arusha Mjini kutohudhuria Bunge kwa siku tano kutokana na alichokiita kufanya vurugu ndani ya Bunge.
Uamuzi huo wa Spika Makinda ulikuja baada ya Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe kumtaka Ndugai aeleze alitumia kanuni gani kuwasimamisha wabunge hao.
Licha ya wabunge hao kupewa adhabu hiyo baada ya kuomba mwongozo wa Spika na baada ya kupinga mwenzao kutolewa ndani ya ukumbi wa Bunge, wapo wabunge wa CCM waliotukana na kutoa lugha za kukera lakini hawakuchukuliwa hatua yoyote.
Wabunge hao ni Peter Serukamba ambaye alitukana tusi zito la nguoni kwa lugha ya kimombo wakati ulipozuka mzozo wakati wa hotuba ya Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani kwa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Profesa Kulikoyela Kahigi.
Bonyeza Read More kuendelea
Wengine ni mbunge wa Kondoa Kusini, Juma Nkamia, Mwigulu Nchemba (Iramba Magharibi) na Livingstone Lusinde (Mtera).
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na Mwananchi Jumapili jana, Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu Dar es Salaam, Profesa Gaudence Mpangala alisema, “Bunge la sasa linakabiliwa na mambo mawili makubwa; la kwanza ni udhaifu wa kiti cha Spika na pili ni wabunge wa CCM kuamini kuwa Chadema ni maadui wakati katika hali ya kawaida siasa ni ushindani na ndiyo demokrasia kwa kuwa sasa tuko katika mfumo wa vyama vingi.”
Alisema kuwa Spika na Naibu wake wameshindwa kudhibiti vurugu bungeni kwa sababu ya kuendekeza itikadi za vyama.
“Kushindwa huko ndiyo kunachangia vurugu kwa sababu wote wanaegemea upande mmoja, wabunge wengine wa upinzani hawawezi kukubaliana na hali hiyo na huo ndiyo mwanzo wa malumbano,” alisema Profesa Mpangala.
Alisema tatizo jingine ni kitendo cha wabunge wa CCM na chama chao kudhani kuwa upinzani ni uadui, “Hayo ndiyo matunda ya mfumo wa vyama vingi. Mfumo huu ni wa ushindani na kuna mambo ya msingi yanayotolewa na wapinzani na mengine hayana ubaya wowote.”
Mhadhiri mwingine wa Chuo hicho, Bashiru Ally alisema Spika anaongoza Bunge kwa ushabiki wa vyama; “Hatuwezi kutenganisha tabia za wabunge ndani na nje ya Bunge, ila pamoja na hilo bungeni sasa kuna ushabiki wa vyama.”
Alisema hali hiyo inasikitisha kwani licha ya kuongezewa posho wabunge sasa wamegeukia malumbano badala ya kujadili mambo ya msingi.
Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi nchini (Tucta), Nicholas Mgaya alisema kuwa viongozi hao wa Bunge wanafanya uamuzi bila kufuata kanuni za Bunge.
“Hatuwezi kuwalaumu wabunge kwa sababu wanaowaongoza wameshindwa kusimamia kanuni hivyo wanajua wazi kuwa hata wakifanya ndivyo sivyo hakuna hatua zozote watakazochukuliwa,” alisema Mgaya.
Kaimu Mwenyekiti wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk Rodrick Kabangila alisema Bunge limekosa usimamizi mzuri, huku akifafanua kuwa limeshindwa kuwachukulia hatua wabunge wa CCM ambao wanatumia chombo hicho cha kutunga sheria kujizolea umaarufu.
“Wabunge watatu wa CCM walitukana, lakini hawakuchukuliwa hatua yoyote ila wabunge wa upinzani walioomba miongozo wamechukuliwa hatua ikiwa ni pamoja na kusimamishwa kuhudhuria vikao vya Bunge, hii si sawa” alisema.
Mwenyekiti wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Helen-Kijo Bisimba alisema; “Inaonekana wabunge hawajui cha kufanya wala kilichowapeleka bungeni.”
Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Ezekiel Oluoch alisema kuwa moja ya mambo yaliyotakiwa kujadiliwa na wabunge hao ni pamoja na madai ya walimu ya muda mrefu.
“Walimu wanaidai Serikali Sh25 bilioni, kuna suala la kutokuwapo kwa mitalaa, haya yote hawayaoni wanaishia kutupiana vijembe tu,” alisema Oluoch.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Profesa Prosper Ngowi alisema wabunge wanatakiwa kutambua kuwa wapo bungeni kwa fedha za wananchi, hivyo wanatakiwa kulipa fadhila.
“Wananchi wanawategemea wabunge wasimamie haki na usawa na kujenga hoja za kutetea masilahi yao, naona 2015 ndiyo uwe muda wa wananchi kuchagua anayewafaa,” alisema Profesa Ngowi.
Mwenyekiti wa Chama Cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, amekitaka kiti cha Spika wa Bunge kufuata sheria, haki, kanuni na miongozo ya kibunge na si kuegemea upande mmoja kwa mustakabali wa kulinda heshima ya taasisi hiyo nyeti kwa taifa.
Pia amemtaka Spika wa Bunge, Anne Makinda kuwakutanisha viongozi wote wa Bunge kutoka pande zote ili kutafuta mwarobaini wa kile kinachoendelea hivi sasa bungeni.
Profesa Lipumba akizungumza jijini Dar es Salaam jana, alisema kinachoendelea bungeni kinatakiwa kutafutiwa ufumbuzi haraka iwezekanavyo.
“Kinachotokea bungeni ni matokeo ya kiti cha Spika kutokutenda haki na wakati mwingine kimekuwa kikiegemea upande mmoja jambo ambalo linafanya kipoteze mwelekeo,” alisema Profesa Lipumba
Alisema kiti hicho kinatakiwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za Bunge na kutokufuatwa kwa vitu hivi, matokeo yake ndiyo haya tunayoyashuhudia sasa, lugha chafu zinazodhalilisha utu wa binadamu.
Mwenyekiti huyo alisema wabunge wanatakiwa kuwawakilisha wananchi wao ipasavyo na kuepuka kujiingiza katika mambo yasiyokuwa na tija kwa wapiga kura wao.
Makinda juzi alilazimika kutoa mwongozo baada ya Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni, Freeman Mbowe kumtaka aeleze, Ndugai alitumia kanuni gani kuwasimamisha wabunge hao.
Baada ya kipindi cha maswali na majibu, Alhamisi iliyopita, Mbowe alisimama na kuomba mwongozo wa Spika akitumia Kanuni ya 68(7) .
No comments:
Post a Comment