Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe amewasifu wabunge wa chama hicho waliosimamishwa huku akimshambulia Spika wa Bunge, Anne Makinda na Naibu wake, Job Ndugai kuwa wanaliendesha Bunge kiharamia.
Akizungumza jana katika uzinduzi wa Chadema kwa Kanda ya Kati, Mbowe alisema Spika Makinda amekuwa ni mwongo hata kuidanganya dunia kuwa uamuzi wao ni sahihi jambo ambalo si kweli.
“Spika Makinda ni mwongo, ameidanganya dunia na amekuwa akitumia maneno ya uongo kuhalalisha uharamia uliofanywa na Naibu Spika wa Bunge kwa kuwatoa ndani wabunge watano wa Chadema,”alisema na kuongeza:
“Uhuni kama huu ndugu zangu haukubaliki, tutaendelea kufanya kazi usiku na mchana kuhakikisha tunatetea masilahi ya nchi hii na watu wake. Na hapa natangaza mbele yenu kuwa wabunge walioondolewa ndani ya Bunge ni mashujaa,” alisisitiza Mbowe.
Mbowe ambaye ni Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, aliwaambia wanachama na mashabiki wa Chadema kuwa wanafanya kazi katika mazingira magumu ndani ya Bunge na kwamba wanatakiwa kuwa majasiri wakiwa bungeni.
Alisema kwamba wakati wote wamekuwa wakishutumiwa kuwa wanafanya fujo ndani ya Bunge, jambo alilosema siyo kweli bali wao wanasimamia Kanuni za Bunge ambazo zimekuwa zikivunjwa na Spika na Naibu wake kila wanapokuwa ndani ya viti vyao.
Alisisitiza kuwa hawako tayari na kamwe hawatakuwa tayari kutii mamlaka yoyote wanayoamini kuwa inawakandamiza na kuwaondolea haki yao, zaidi ya kupambana.
Kiongozi huyo alinukuu baadhi ya vifungu vya Kanuni za Bunge alivyosema kuwa vingetumika kwa kumaliza tatizo la Lissu, aliyemwelezea kuwa alikuwa sahihi, hata angesimama mara mia moja kwa sababu alikuwa akipinga upuuzi.
Kuhusu Katiba
Akizungumzia masuala ya mchakato wa Katiba Mpya, Mbowe alisema kuwa uamuzi uliotolewa ndani ya Bunge katika hotuba yake ndiyo msimamo wa Chadema, akatahadharisha kuwa ikiwa Serikali haitakubali kufanya marekebisho waliyopendekeza, chama hicho kitajitoa.
“Ule ulikuwa ni msimamo wa Kamati Kuu ya chama chetu na bado tunasisitiza kuwa wasipokuwa makini tutajitoa. Kama noma na iwe noma, hata kama uchaguzi, tutashinda kwa nguvu ya Mungu,” alisema na kushangiliwa na umati wa watu.
Hata hivyo, alionya kuwa kama Serikali itapuuza ushauri wao, itaisoma namba kwa kuwa wanajua kinachotaka kufanywa na tayari wameshajipanga kukabiliana nacho.
Dk Slaa ammwagia sifa Lissu
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Chama hicho Dk Wilbrod Slaa alimwagia sifa Mbunge wa Singida Mashariki ambaye pia ni Mnadhimu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Tundu Lissu, kuwa yeye na wenzake watano waliondolewa kishujaa na wanatakiwa kusonga mbele zaidi.
No comments:
Post a Comment