Saturday, April 20, 2013

Tume ya mabadiliko ya katiba yapata kigugumizi


Tume ya Mabadiliko ya Katiba nchini, imesema itatoa taarifa maalumu ya nini kifanyike kutokana na malalamiko ya mchakato wa kuwapata wajumbe wa mabaraza ya kata baada ya kupata mrejesho wa kazi hiyo kutoka mikoa yote ya Tanzania.

Kauli hiyo imekuja siku chache baada ya kasoro kadhaa kujitokeza kwenye mchakato wa kuwapata wajumbe wa mabaraza ya katiba ya kata.

Miongoni mwa malalamiko hayo ni pamoja na mchakato huo kugubikwa na siasa, dini na wakati mwingine wanaosimamia wamelalamikiwa kuwauliza wanaoomba kama ni wa chama gani.

Akizungumza na gazeti hili, Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Joseph Warioba alisema kwa sasa hawana kauli kwani hawawezi kutoa maamuzi kwa kutumia kauli za mitaani.

Alisema wanasubiri taarifa maalumu kutoka mikoani juu ya  zoezi zima lilivyoendeshwa katika kuwapata wajumbe hao.

Mchakato wa kuwapata wajumbe hao ulianza mapema mwezi Machi mwaka huu na kwamba kati ya Aprili 13 na 17 majina ya wajumbe hao waliochaguliwa na kikao maluum cha kamati cha maendeleo ya kata yatawasilishwa kwa Mkurugenzi wa Mamlaka ya Serikali za Mitaa husika.

Kwa mujibu wa Jaji Warioba, kwa sasa tume yake haina majibu ya nini watafanya katika kushughulikia malalamiko hayo hadi mchakato mzima utakapo kamilika na kupata ripoti kutoka mikoa yote.

Kwa mujibu wa utaratibu wa kuwapata wajumbe hao, kila kata kwa Tanzania Bara isipokuwa Dar es Salaam, itatoa wajumbe wanne wakati Dar es Salaam itatoa wajumbe wanane huku madiwani wote 4,453 wakijumuishwa kama wajumbe.

Tanzania Bara ina kata 3,339 ikiwa ni pamoja na 90 za mkoa wa Dar es Salaam ambapo wajumbe wa kata zote ni 13,716 na ukiongeza na idadi ya madiwani wote, wajumbe wa mabaraza hayo ya kata watakuwa 18,169.

Kwa upande wa Zanzibar kila shehia itatoa wajumbe watatu ambako kuna shehia 335, hivyo wajumbe wa shehia watakuwa 1,005 na wakijumuishwa madiwani wote 193 jumla ya wajumbe wote watakuwa 1,198.

Warioba alisisitiza kuwa mwombaji lazima atimize vigezo ambavyo ni kuwa raia wa Tanzania, mwenye umri wa miaka isiyopungua 18 na mwenye uwezo wa kusoma na kuandika.

Sifa nyingine alizitaja kuwa ni awe mkazi wa kudumu wa kijiji, mtaa na shehia husika, awe mwenye hekima, busara na uadilifu lakini pia awe na uwezo wa kujieleza na kupambanua mambo.

Tume hiyo inayotarajia kumaliza kazi yake Oktoba mwaka huu, wajumbe wake ni Mwesiga Baregu, Dkt. Salim Ahmed Salim, Riziki Shahari Mngwali, Fatma Said Ali, Dkt. Edmund Sengondo Mvungi, Omar Sheha Mussa, Richard Shadrack Lyimo, Raya Salim Hamad, John Nkolo, Awadh Ali Said, Alhaj Said Hamad El-Maamry na Ussi Khamis Haji.

Wengine ni Jesca Mkuchu, Salma Maoulidi, Profesa Palamagamba Kabudi, Nassor Khamis Mohamed, Humphrey Polepole, Simai Mohamed Said, Yahya Msulwa, Mohamed Yusuph Mshamba, Esther Mkwizu, Kibibi Mwinyi Hassan, Maria Malingumu Kashonda, Suleiman Omar Ali, Al-Shaymaa Kwegyir, Salama Kombo Ahmed, Mwantumu Malale, Abubakar Mohamed Ali, Joseph Butiku na Ally Abdullah Ally.

 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment