Saturday, April 20, 2013

Chadema waruhusiwa uzinduzi M4C Dodoma


Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimeruhusiwa kufanya uzinduzi 
wa harakati za mabadiliko wa chama hicho M4C leo ambao awali ulizuiwa na jeshi la polisi.
 
Katibu wa Chadema mkoani hapa, Jerry Mambo, alisema kuwa wameruhusiwa kufanya uzinduzi huo nje ya mji baada ya Mwenyekiti wa Chama chao, Freeman Mbowe, kuzungumza na Waziri Mkuu Mizengo Pinda.
 
Hata hivyo, alisema bado hawajapanga eneo watakalokwenda kufanyia uzinduzi huo baada ya kukataliwa viwanja vyote vya katikati ya mji wa Dodoma.
 
Akizungumza jana na waandishi wa habari mjini hapa, Kamanda wa Polisi
mkoani Dodoma, David Misime, alisema zuio hilo ni kutokana na maamuzi ya Kamati ya Ulinzi na Usalama ya mkoa kuamuru kuwa katika kipindi cha Bunge kusifanyike mikutano au maandamano ya vyama vya siasa.
 
Alisema kuwa Aprili 8, Katibu wa Chadema wilaya ya Dodoma alimwandikia mkuu wa polisi wa wilaya ya Dodoma akimtaarifu nia yao ya kufanya uzinduzi huo
Aprili 21 katika Uwanja wa Barafu mjini hapa.
 
Hata hivyo, alisema Aprili 10 aliandika barua nyingine
akimjulisha Ocd kuwa tarehe ya uzinduzi imebadilika na badala ya Aprili  21 itakuwa Aprili 20.
 
“Tarehe 15 mwezi huu Ocd alimwandikia barua akimjulisha kuzuia uzinduzi huo kwasababu uwanja wa barafu ulishatolewa kwa mtu mwingine
 
kwaajili ya shughuli za kidini…Pili ilishaamuriwa kuwa katika kipindi cha bunge kusifanyike mikutano au maandamano ya vyama vya siasa hapa Dodoma,” alisema Misime.
 
Alifafanua kuwa Katibu huyo wa Chadema aliandika tena barua kwa Ocd akimjulisha kuwa kwavile uwanja wa barafu utatumiwa na watu wengine basi wao watatumia uwanja wa shule ya msingi Uhuru.
 
Akizungumza na NIPASHE jana jioni, Misime alisema kuwa hawajapata taarifa ya kuruhusiwa kwa uzinduzi huo.
 
“Nasikia wamekata rufaa kwa Waziri wa Mambo ya Ndani, inawezekana hawajaruhusiwa. Sisi tukishatoa maelekezo haturudi tena kufuatilia. Tunasubiri taarifa kutoka kwa Waziri,”alisema.
 
Alisema juzi katibu wa chama hicho aliandika barua nyingine kwa Ocd akimjulisha kuwa wamebadili uwanja na watafanyia katika kiwanja kilichopo njia panda ya wajenzi.
 
“OCD alirejea msisitizo wake wa awali kuwa uzinduzi huo usifanyike na akamshauri kama hawakuridhika na sababu alizozitoa kuzuia uzinduzi wa M4C katika kipindi hiki cha Bunge basi wafuate jinsi sheria ya Polisi na polisi wasaidizi sura ya 322 kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002 inavyoelekeza kwenye kifungu cha 43(6) kukata rufaa kwa waziri wa mambo ya ndani ya nchi,” alisema.
 
Alisema lengo la katazo hilo ni kuwaacha wabunge kufanya kazi zao kwa amani na utulivu hivyo mikutano na maandamano hayatakiwi kufanyika.
 
 CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment