LEMA AIBUKA, AMTAKA RC AACHE KUMTUMIA VITISHO
KATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa amefafanua kauli yake, kwa kutaja sababu kadhaa ambazo zitasababisha nchi isitawalike kama alivyowahi kuonya.
Mwaka juzi, Dk. Slaa alimtaka Rais Jakaya Kikwete kuwa makini na kuchukua hatua za haraka kurejesha amani kabla Watanzania hawajaishiwa uvumilivu na utawala wa serikali yake.
Hata hivyo, kauli hiyo ya kwamba nchi haitatawalika, kwa siku za karibuni imekuwa ikipotoshwa na viongozi wa serikali na CCM wakidai kuwa CHADEMA ilikuwa ikimaanisha kufanya vitendo vya fujo ili kuidhoofisha Serikali ya Rais Kikwete.
Akihutubia mkutano wa hadhara jana mjini Njombe katika Jimbo la Njombe Kusini linaloongozwa na Spika wa Bunge, Anne Makinda uliofanyika kwenye viwanja vya National Housing, Dk. Slaa alisema alichomaanisha ni mtiririko wa matukio ya watu kunyanyaswa.
“Narudia tena hapa kuwa itafika mahali nchi hii haitatawalika na itamshinda Kikwete. Yaliyojiri Rwanda na Burundi kuhusu ukabila wananchi waliyapigia kelele mapema, lakini watawala wakapuuza, kilichofuata nchi zikavurugika,” alisema.
Dk. Slaa ambaye aliambatana na baadhi ya wabunge wa chama hicho waliokuwa wamesimamishwa kuhudhuria vikao vya Bunge kwa siku tano, alifafanua kuwa hatari hiyo ya amani kutoweka nchini aliiona mapema kama kiongozi wa siasa, ndiyo maana akaonya.
“Tangu mapema manyanyaso ya wananchi hayasikilizwi, sakata la korosho Lindi tuliliona kwenye ziara yetu mwaka jana, wabunge wetu wakalifikisha bungeni lakini serikali ikapuuza, sasa wananchi wa Lindi na Mtwara wameishiwa na uvumilivu, CCM wanadai ni CHADEMA,” alisema.
Katibu huyo alitumia fursa hiyo kuwapa pole wananchi wa Liwale kwa vurugu zilizotokea juzi na kuharibu mali mbalimbali akisema kuwa walipigwa mabomu wakidai haki zao.
“Adui wa Kikwete si CHADEMA, Slaa wala Mbowe kama CCM na serikali yao wanavyopotosha, bali wajue kuwa adui ni manyanyaso wanayofanyiwa wananchi, wamechoka na hilo ndilo nililoonya kuwa itafika mahali nchi haitatawalika,” alisema.
Dk. Slaa mbele ya wabunge wake, Mchungaji Peter Msigwa (Iringa Mjini), Joseph Mbilinyi (Mbeya Mjini) na Ezekiel Wenje (Nyamagana) alisema kuwa hata vurugu bungeni zinatokana na Bunge hilo kuongozwa kwa misingi ya vyama badala ya kujali maslahi ya kitaifa.
Alisema kuwa wananchi wa kila kada wamechoka na maisha duni, hivyo wanaishinikiza serikali yao iliyokuwa imekataa kuwasikiliza ichukue hatua sasa.
“Walimu kutopewa mishahara yao, wanafunzi wanaendelea kufeli kwa sababu walimu hawajaboreshewa mazingira ya kutoa elimu bora, watu wachache kuendelea kunufaika na jasho la wengi, hayo yote yamesababisha Watanzania kuishiwa uvumilivu.
“Na utawala wa serikali umedhihirisha kwa mara nyingine kuwa Kikwete ameendelea kufumbia macho mambo hayo, nchi inazidi kukosa mwelekeo,” alisema.
Dk. Slaa aliongeza kuwa aliposema nchi haitatawalika, alimaanisha serikali itatue kero za wananchi, itekeleze wajibu wake badala ya kufanya siasa kwenye matatizo.
“Serikali ingekuwa makini wangenisikiliza, mambo yanayotokea sasa yasingetokea. Serikali imekuwa ikiishi kwa matukio, likitoka hili linakuja jingine, likimalizika hili linaibuka jipya,” alisema.
Bonyeza Read More Kuendelea
Lema amuonya RC
Habari kutoka Arusha zinasema kuwa Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema ambae ametangazwa kusakwa na Jeshi la Polisi mkoani humo, jana alijitokeza na kutangaza mgogoro na Mkuu wa Mkoa Magesa Mulongo.
Lema alisema kuwa Mulongo amemtumia vitisho kupitia ujumbe wa maandishi kwenye simu (sms).
Akizungumza na waandishi wa habari katika mgahawa wa Ethiopia jijini Arusha, Lema alisema amepokea ujumbe wa maandishi kutoka kwa Mulongo ukisomeka; “umeruka kihunzi cha kwanza, nitakuonyesha kuwa mimi ni serikali, ulikojificha nitakupata na nitakupa kesi ninayotaka mimi.”
Lema alionesha sms hiyo kwa waandishi wa habari, ikiwa imetumwa kutoka katika namba 0752 960276 ambayo alidai ni ya Mulungo.
“Nilimjibu kuwa nimekupata, nimekuelewa na nipo tayari. Na ujumbe huo ulionesha kuwa ulipokelewa katika simu ya mkuu wa mkoa. Huo ni mwendelezo wa vitisho vyake kwangu,” alisema.
Alisema kuwa hatambui chanzo halisi cha Mulongo kumtumia vitisho hivyo, lakini akasema tayari ameishamjua vyema mkuu huyo wa mkoa na kamwe hatamuogopa bali atatoa ushirikiano wowote kwake.
“Nimeshangaa kusikia kwenye vyombo vya habari jana kuwa mkuu wa mkoa ameagiza nikamatwe kwa kuchochea vurugu katika Chuo cha Uhasibu wakati mimi nilifika hapo kuzungumza na wanafunzi na kuwazuia wasiandamane.
“Mimi namshangaa sana huyu Mulongo, nilimpigia simu mimi kumuarifu na kumuita kuzungumza na wanafunzi ili kutoa tamko la serikali na akaahidi kufika baada ya dakika 10, lakini akafika baada ya saa moja,” alisema.
Mulongo alipoulizwa na mwandishi wetu kuhusu madai ya kumtumia Lema ujumbe wa vitisho, alionesha kushangazwa na maelezo hayo lakini hakukiri wala kukataa.
“Unaandikia chombo gani? Sasa huo ujumbe anaosema nimemtumia umeuona unatoka kwangu?” Alihoji.
Akizungumzia vitisho hivyo, Dk. Slaa alisema kuwa CHADEMA wamekubaliana kumchukulia hatua za kisheria Mulongo kwa kumfungulia kesi mahakamani.
Alisema vitisho hivyo ni hatari na pia ni kielelezo cha matumizi mabaya ya madaraka.
No comments:
Post a Comment