Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika, amemhoji Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kwanini Serikali inapuuza kupeleka bungeni ripoti ya utekelezaji wa maazimio ya kamati ndogo ya kamati ya Bunge kuhusiana sakata la aliyekuwa Katibu Mkuu wa Nishati na Madini, David Jairo.
Kamati hiyo iliundwa kuchunguza sakata la Jairo kuchangisha Sh. milioni 180 kwa idara na taasisi zilizo chini ya wizara hiyo kwa ajili ya kushawishi wabunge wapitishe bajeti ya wizara hiyo ya mwaka 2011/12.
Mnyika alihoji suala hilo wakati wa maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu, bungeni mjini Dodoma jana.
Alisema Bunge lilipitisha azimio Novemba 21, mwaka juzi, baada ya kufanya uchunguzi juu ya matumizi mabaya ya fedha, lakini hadi sasa ni zaidi ya mwaka mmoja na nusu bado serikali haijaleta taarifa ya utekelezaji wa taarifa wa kamati ndogo ya Bunge.
“Na wala waliokuwa wanatakiwa kuchukuliwa hatua, hawajachukuliwa hatua ni kwanini serikali yako imekuwa ikidharau kutekeleza maazimio ya Bunge kwa wakati?” alihoji.
Akijibu Pinda, alisema jitihada zinafanyika kila wanapopata ushauri wa Bunge na kwamba hawapuuzi hata siku moja.
“Si kwamba hakuna kilichofanyika, tumechukua hatua kadhaa ndani ya Serikali, pengine kilichokosekana ni kurejesha mrejesho wa kipi tumekamilisha na tusichokamilisha,” alisema.
Katika swali la nyongeza, Mnyika alitaka kufahamu ni lini ripoti hiyo itapelekwa bungeni.
Akijibu swali hilo, Pinda alisema ripoti hiyo itapelekwa wakati wowote.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment