MNYIKA: WANGEKUBALI HOJA YANGU TUSINGEFIKA HAPA
KAMA dalili zilivyoonesha tangu mapema ndivyo hali ilivyokuwa jana baada ya wabunge kuikwamisha hotuba ya bajeti ya Wizara ya Maji iliyowasilishwa juzi na Waziri Jumanne Maghembe.
Bajeti hiyo ilikwama baada ya Spika wa Bunge, Anne Makinda kutoa mwongozo wa kuahirisha mjadala huo hadi Jumatatu ijayo.
Spika Makinda aliahirisha mjadala wa hotuba hiyo wakati akitoa mwongozo wa mbunge wa Iramba Magharibi, Mwigulu Nchemba (CCM).
Katika mwongozo wake, Mwigulu aliomba kiti cha spika kuiondoa hoja hiyo ili wizara ikutane na Kamati ya Bajeti kuifanyia marekebisho.
Akitoa mwongozo wake, Spika Makinda alisema mwenendo wa uchangiaji wa bajeti hiyo, umeonesha dhahiri kwamba wabunge wengi wamekataa kuiunga mkono.
“Kwa hali hiyo naiagiza Wizara ya Maji ikutane na Kamati Ndogo ya Bajeti na Hazina ili kuifanyia marekebisho bajeti hiyo. Hivyo naahirisha shughuli za Bunge hadi Jumatatu saa tatu asubuhi,” alisema.
Hata hivyo, uamuzi huo ulikuwa ufikiwe mapema kama Waziri Mkuu Mizengo Pinda angekubali wakati akijibu swali la Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe aliyetaka hoja hiyo iondolewe ili ikafanyiwe marekebisho.
Katika swali lake kwa Pinda wakati wa kipindi cha maswali ya papo kwa hapo kwa Waziri Mkuu, Mbowe aliitaka serikali kuiondoa hoja hiyo kutokana na mwelekeo wa mjadala huo kuonesha kuwa wabunge wengi hawaiungi mkono.
Hata hivyo, kama ulivyo utamaduni wa viongozi wa Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kujibu hoja kwa kuangalia imeletwa na mbunge wa upande gani, Pinda alikiri kuwa wabunge wengi wameonesha kutoridhishwa na bajeti hiyo, lakini si busara kuiondoa.
Alisema tatizo kubwa ni uhaba wa fedha na hata wizara zingine zitakapowasilisha bajeti zake, tatizo litakuwa ni uhaba wa fedha.
“Mimi nadhani tuchukue ushauri wa kuhamisha fedha kutoka fungu la matumizi mengine, ziingizwe kwenye bajeti hiyo,” alisema pinda.
Licha ya Pinda kukataa hoja ya Mbowe kwa kudhani angeipa sifa kambi ya upinzani, mwongozo wa Mwigulu uliokuwa na mwelekeo sawa na muuliza swali, spika aliukubali na kuamua kuahirisha hoja hiyo.
Bonyeza Read More Kuendelea
Mjadala ulivyokuwa
Mjadala wa hotuba hiyo ulioanza juzi ulikuwa moto kutokana na wabunge wengi kuzungumza kwa hisia kali na kutishia kutoipitisha kwa madai kuwa haitaondoa kero ya maji nchini.
Wabunge hao bila kujali itikadi zao walieleza kuchoshwa na ahadi hewa, uongo na kauli tamu za mikakati ya kukabiliana na tatizo la maji.
Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola (CCM) alikuwa kivutio kikubwa kutokana na stahili yake ya uchangiaji.
Huku akiwaacha hoi wabunge kwa vicheko, Lugola aliingia bungeni na picha kubwa ya katuni inayowaonesha kinamama wanavyopata adha ya maji na kuita katuni hiyo kuwa ni ‘Nyoka wa Shaba’.
“Mheshimiwa naibu spika, Mussa aliambiwa na Mungu atengeneze sanamu ya nyoka wa shaba ili kila mtu atakayegongwa na nyoka, akiiangalia sanamu hiyo atapona. Mimi nimekuja na katuni hii kama nyoka wa shaba ili kila mbunge anayetaka kurudi bungeni asiunge mkono hoja hii.
“Ila akija kuangalia nyoka wa shaba, atapata baraka za wakina mama wanaoteseka kwa shida ya maji na watampigia kura kurudi hapa bungeni,” alisema na kuwaacha wabunge hoi kwa vicheko.
Huku akishika picha hiyo, Lugola aliomba kiti cha spika kukubali kuiweka ndani ya ukumbi wa Bunge kama nyoka wa shaba ili kupata tiba kwa wabunge wanaotaka kubaki bungeni.
Mbunge huyo alisema haungi mkono hoja hiyo kwani anaamini ni sawa na mchezo wa karata tatu. Kwamba kwa zaidi ya miaka sita, amekuwa akiunga mkono hoja ya maji kutokana na miradi ya maji iliyokuwa imeainishwa na serikali bila mafanikio.
Lugola aliwataka wabunge wenzake kuacha kuiunga mkono hoja hiyo kwa madai kuwa hakuna kitakachofanyika katika mipango hiyo ya serikali.
“Mh wabunge, tumeunga mkono mradi wa maji Kibaha hakuna kilichofanyika, mradi wa maji Bunda uongo mtupu, miaka nane sasa bila mafanikio. Leo waziri anakuja na mipango mingi ya maji. Mimi siungi mkono safari hii, ndiyo maana nimekuja na nyoka wa shaba,” alisema Lugola.
Mbunge wa Longido, Lekule Laizer (CCM) naye alisema haungi mkono hoja kwani katika jimbo lake familia zinaoga kwa zamu.
“Kule kwenye jimbo langu familia zinaoga kwa zamu. Kama leo zamu ya baba kuoga, mama haogi na watoto marufuku. Kesho ikiwa zamu ya mama, baba haogi. Hali ni mbaya sana,” alisema mbunge huyo.
Akichangia mjadala huo, Mbunge wa Ubungo, John Mnyika (CHADEMA) alisema kuwa kama wabunge wa CCM wangekubali hoja yake iliyokataliwa bungeni, leo serikali ingekuwa na majibu na mikakati ya kuondoa kero ya maji nchini.
Mnyika alisema haungi mkono hoja hiyo kwani mipango mingi aliyoainisha waziri kuanzia ile ya Jiji la Dar es Salaam na vijijini haitekelezeki.
“Mimi niwatake wabunge wa CCM safari hii waache unafiki hapa. Haitakuwa na maana mnatangaza kutounga mkono bajeti, Bunge likikaa kama kamati mnapitisha. Hamlisaidii taifa,” alisema Mnyika.
Mbunge wa Kigoma Mjini, Peter Serukamba (CCM) alipendekeza serikali ipungunze fedha zilizotengwa kwa ajili ya matumizi mengine kama ya safari za nje, mikutano na warsha ili fedha hizo ziingizwe kwenye bajeti ya maji.
Serukamba alipendekeza kuwa asilimia 15 ya fedha za matumizi mengine zikatwe na kuingizwa kwenye bajeti ya Wizara ya Maji ambapo watakusanya zaidi ya sh bilioni 600.
Nimrod Mkono, Mbunge wa Musoma Vijijini (CCM) alisema haungi mkono hoja hiyo kwani katika jimbo lake kuna miradi ya tangu mwaka 1974, haijatekelezwa.
Christopher ole Sendeka wa Simanjiro (CCM) alipendekeza posho za wabunge zipunguzwe na kuelekezwa kwenye miradi ya maji.
Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassar (CHADEMA) alisema waziri amelidanganya Bunge kwani kijiji alichokitaja kwamba kina mradi wa maji katika jimbo lake hakipo na wala mradi wenyewe haupo.
Katika mwaka huu wa fedha, Waziri Maghembe aliomba Bunge kuidhinisha sh bilioni 398.
No comments:
Post a Comment