Thursday, April 18, 2013

Selasini ahoji walimu wapya kucheleweshewa malipo


MBUNGE wa Rombo, Joseph Selasini (CHADEMA) ameihoji serikali kuchelewesha malipo kwa walimu wapya na kusema hali hiyo inawasababishia usumbufu walimu hao.
Selasini alitoa kauli hiyo bungeni jana alipouliza swali la nyongeza na kuitaka serikali ieleze ni kwanini imekuwa haitekelezi mipango yake hususani malipo kwa walimu hao ambao walitakiwa walipwe mara wanapoanza kazi.
Mbali na hilo, Selasini alisema katika Wilaya ya Rombo walimu wengi hawajalipwa fedha zao za posho na stahili nyingine kama walivyotegemea, jambo ambalo limewasababishia kukata tamaa ya kufanya kazi.
Katika swali la msingi, Mbunge wa Sumve, Richard Ndassa (CCM) alitaka kujua iwapo walimu wote nchini hukatwa asilimia 2 ya mishahara yao na kwamba tangu mwaka 2005 hadi 2011 ni kiasi gani cha fedha kimekusanywa.
Pia alitaka kujua jengo la Mwalimu House pamoja na majengo mengine katika mikoa ya Mtwara, Kigoma na Mbeya yanapangishwa kwa shilingi ngapi kwa mwaka.
Akijibu maswali hayo, Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo alisema walimu wa ajira mpya ambao wamecheleweshewa kulipwa posho na mishahara yao ni wale waliochelewa kuripoti katika vituo vyao vya kazi.
Alisema kwa mujibu wa taarifa ya Msajili wa Vyama vya Wafanyakazi kiasi kilichochangwa na wananchama kutoka mwaka 2005 hadi 2011 ni sh bilioni 81.2.
“Kuhusu jengo la Mwalimu House lilikamilika mwaka 2007 na ndipo lilipoanza kutumika hadi kufikia mwaka 2011, jengo hilo lilikuwa limepata sh milioni 920 kama mapato ya kodi ya pango kutoka kwa wapangaji.
“Fedha hizo zimepelekwa kwenye mifuko ya SACCOS za walimu mikoani na wilayani,” alisema Mulugo.

No comments:

Post a Comment