Thursday, April 18, 2013

Mnyukano bungeni



MJADALA WA LWAKATARE, ULIMBOKA, KIBANDA MARUFUKU
MVUTANO mkali umeibuka bungeni baada ya serikali na baadhi ya wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kutaka hotuba ya Msemaji wa Kambi ya Upinzani isisomwe.
Mawaziri na baadhi ya wabunge wa CCM walipinga hotuba hiyo isisomwe kwa madai kuwa inagusa kesi ya Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa CHADEMA, Wilfred Lwakatare, Dk. Steven Ulimboka na Absalom Kibanda ambao walidai masuala yao yako mahakamani na masuala ya Usalama wa Taifa.
Hali hiyo iliibua malumbano mazito ya kisheria na kusababisha Naibu Spika, Job Ndugai, kuahirisha mjadala huo na kuagiza Kamati ya Kanuni kukutana kwa dharura kulipatia ufumbuzi suala hilo.
Katika mjadala huo, Mbunge wa Kigoma Mjini, Peter Serukamba (CCM) alijikuta akipandwa jaziba na kutoa tusi ambalo gazeti hili haliwezi kulichapisha.
Mbunge wa kwanza kuwasha moto huo alikuwa Serukamba ambaye aliomba mwongozo wa spika kutaka kiti cha spika kizuie kujadili hotuba hiyo.
Serukamba alitoa mwongozo huo takriban dakika mbili kupita tangu Msemaji wa Kambi ya Upinzani, Profesa Kolikoyela Kahigi, kuanza kusoma hotuba mbadala ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Menejimenti ya Utumishi wa Umma kwa mwaka wa fedha 2013/ 2014.
“Mheshimiwa Spika, ukisoma taarifa ya Msemaji wa Kambi ya Upinzani, ukurasa wa pili hadi wa nne, kwanza tunaingilia uhuru wa mahakama. Ni juzi tu Mheshimiwa Mustafa Akonay (CHADEMA), alitukumbusha juu ya jambo hili.
Pili, tunataka kuleta jambo la mahakamani kulifanyia siasa ndani ya Bunge, na tatu tutakuwa taifa na Bunge la ajabu sana duniani, tunataka kujadili jambo ambalo liko mahakamani,” alisema Serukamba.
Kauli ya Serukamba ilimnyanyua Mbunge wa Ubungo, John Mnyika (CHADEMA) na kutoa taarifa bungeni kupinga mwongozo wa mbunge aliyetangulia.
“Mheshimiwa Spika, msemaji aliyetangulia (Serukamba), amefanya rejea ya hotuba ya kambi ya upinzani hata kabla haijasomwa.
Taarifa ni kwamba katika kurasa alizozitaja hakuna jambo la mahakamani. Kurasa hizo zinazungumzia kuhusu utekaji nyara wa Dk. Uimboka, Kibanda, gazeti la MwanaHalisi kufungiwa na kazi za Usalama wa Taifa. Hakuna jambo lililoko mahakamani hapo,” alisema Mnyika.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera na Uratibu wa Bunge, William Lukuvi, naye alisimama na kuomba mwongozo wa spika akitaka hotuba ya kambi ya upinzani isisomwe.
“Mheshimiwa Waziri Mkuu, tunaweza kufanya sarakasi nyingi bila sababu za msingi.  Ukurasa wa tatu umetaja jina la Lwakatare. Alichosema Serukamba ni utangulizi tu. Hii kesi ipo mahakamani na ni kuingilia uhuru wa mahakama.
“Na hii ni kinyume cha sheria ya Usalama wa Taifa. Ni marufuku kutaja hata majina ya watumishi wa Usalama wa Taifa, lakini hotuba ya wenzetu inataja mambo ya Usalama wa Taifa.
“Mimi nashangaa mambo hayo hayo yanarudi tena bungeni kwa mlango wa nyuma. Lengo langu ni kuanzia ukurasa wa kwanza hadi wa nne yanayohusu masuala ya Usalama wa Taifa, Ulimboka na Lwakatare, tuyaache,” alisema Lukuvi.
Mbunge wa Kawe, Halima Mdee, naye alipata nafasi na kutoa ufafanuzi kwamba kuanzia ukurasa wa kwanza hadi wa tatu hakuna mahala jina la Lwakatare limetajwa, lakini katika ukurasa wa nne jina lake limetajwa bila kuingilia mwenendo wa kesi.
Alisema ukurasa wa nne unaeleza jinsi alivyokamatwa, jambo ambalo haliingilii uhuru wa mahakama.
Mbunge huyo ambaye ni mwanasheria, kuhusu sheria ya Usalama wa Taifa, alimtaka Waziri Lukuvi alete sheria ya Usalama wa Taifa ili ilinganishwe na hiyo inayotajwa bungeni. 
Naye Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, alipingana na maelezo ya Waziri Lukuvi na wabunge waliotaka hotuba hiyo izuiliwe.
“Mheshimiwa Spika, kabla sijasema, niseme ninayo sheria hapa ya Idara ya Usalama ya mwaka 1996. Maneno kwamba masuala ya Usalama wa Taifa hayazungumziki bungeni ni maneno ya mitaani.
Kinachokatazwa kwenye magazeti, mikutano na mahala pengine ni kutaja majina ya watumishi wa Usalama wa Taifa.
“Idara ya Usalama wa Taifa inaongozwa na mkurugenzi ambaye anapewa maelekezo na waziri. Kama wanafanya vibaya huko nje, anayewajibishwa ni waziri na namna ya kumwajibisha ni kuruhusu msemaji wa upinzani aendelee,” alisema.
Alisema ni jambo la hatari kumzuia msemaji kuzungunzia idara ya serikali inayotumia fedha za serikali.
”Hakuna mahala popote kesi ya Lwakatare, Idara ya Usalama wa Taifa imetajwa kwa namna ambayo ina influence uamuzi wa mahakama,” alisema Lissu.
Alisema kama hakuna mahala popote hotuba ya upinzani imetaja kesi ya mahakamani, litakuwa jambo baya sana kuiziba mdomo kambi ya upinzani.
Naibu Spika alimpa nafasi tena Serukamba ili kujibu hoja za wabunge waliopinga ambapo badala ya kuzungumza alijikuta akitoa tusi ambalo haliwezi kuandikika.
Mbunge wa Simanjiro, Christopher ole Sendeka (CCM), naye alisema hotuba hiyo izuiliwe kwa madai kuwa inaingilia uhuru wa mahakama.
Akitoa mwongozo wake, Naibu Spika aliiagiza Kamati ya Kanuni kukutana mara moja na kuja na majibu ambayo yatasaidia mjadala huo kuendelea jioni.
Baadaye jioni hotuba hiyo ilisomwa baada ya pande hizo kukubaliana kuwa kurasa zilizokuwa na matatizo ziondolewe.
Hata hivyo, mjadala wa jumla ulipoanza kwa wabunge wote, Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, aliibua mtafaruku mkubwa pale alipodai kuwa Rais Jakaya Kikwete ndiye kinara wa mgogoro wa udini nchini.
Kauli ya Lema iliwafanya baadhi ya wabunge wa CCM na mawaziri William Lukuvi, Stephen Wassira na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Fredrick Werema, kuinuka na kuomba mwongozo wa spika wakimtaka mbunge huyo afute kauli yake.
Lukuvi alijenga hoja akisema kwa mujibu wa kanuni ni marufuku jina la rais kutajwa kwa msamaha, hoja ambayo hata hivyo Lissu aliipinga akidai kanuni inatumika kimakosa kwani haikatai kiongozi huyo kukosolewa.
Hata hivyo Lema alipopewa nafasi ya kufuta kauli yake ama kuithibitisha, alirejea maneno yake kuwa Rais Kikwete ndiye kinara wa udini nchini akishirikiana na mawaziri kama Wassira na Lukuvi.
Kabla ya kubanwa, Lema alitumia muda wake kuwashambulia Usalama wa Taifa kwa kutajwa kuhusika katika matukio kadhaa ya kuteka na kutesa raia.
Alisema yuko tayari kung’olewa kucha au meno, lakini hataogopa kusema ukweli.
Akizungumzia zaidi suala la dini, Lema alisema taifa limefika mahala pabaya na kama hali itaachiwa, kuna hatari ya kutokea vurugu za kidini.
Aliilaumu tena serikali kwa kuachia hali hiyo kwani imeshindwa kuchukua maamuzi magumu kwa wakati kutokana na hofu na woga usio na sababu.
”Sasa hivi rais akifanya uteuzi, baada ya nusu saa watu wanaanza kujadili nani Mkristo, nani Mwislamu. Hii ni hatari,” alisema Lema.

No comments:

Post a Comment