Thursday, April 18, 2013

Akunaay akumbushia ahadi ujenzi uwanja wa ndege


MBUNGE wa Mbulu, Mustapha Akunaay (CHADEMA) ameitaka serikali kueleza ni lini itatimiza ahadi ya kujenga uwanja wa ndege kwa wananchi wa Babati, Mbulu na Katesh.
Mbunge huyo alitoa kauli hiyo bungeni jana alipouliza swali la msingi na kusema kutokana na sera ya uchukuzi ya mwaka 2003, serikali iliahidi kujenga uwanja wa ndege mkoani Manyara katika eneo la Magugu ili kutoa huduma za usafiri wa ndege kwa wananchi wa mkoa huo, lakini hadi sasa haujajengwa, hivyo kuhoji utajengwa lini.
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Uchunguzi, Dk. Charels Tizeba alikiri  kuwa katika eneo hilo walikubaliana uongozi wa mkoa uanze mchakato wa kuandaa ramani ya mipango miji ambayo itaainisha eneo litakalojengwa kiwanda cha ndege.
“Baada ya kukamilisha ramani hiyo waiwasilishe kwenye vikao vya ushauri vya mkoa kuomba kibali cha serikali kuidhinisha matumizi yake na miradi mbalimbali ya maendeleo ianze kutekelezwa kulingana na ramani ya mipango miji ukiwemo mradi wa ujenzi wa kiwanja kipya cha ndege cha Manyara,” alisema.
Hata hivyo, alisema uwezo wa serikali ni mdogo, hivyo haiwezi kujenga kiwanja cha ndege kila mkoa kwa mara moja na badala yake miradi hiyo itakuwa inatekelezwa kwa awamu.
“Wizara inazingatia ushauri wa Bunge kwamba tuandae miradi ambayo serikali itakuwa na uwezo wa kutekeleza katika kila bajeti, kinachotakiwa sasa ni kutekeleza miradi hii kwa awamu.
“Mfano, kwa sasa miradi hii ya ujenzi wa viwanja vya ndege inayoendelea Kigoma, Bukoba, Tabora, Mafia, Songwe na Mwanza,” alisema.
Alisema kwa mwaka huu wa fedha 2013/14 miradi ya ujenzi wa uwanja wa ndege wa Sumbawanga, Shinyanga na Mtwara itatekelezwa kwa fedha za mkopo kutoka Benki ya Uwekezaji ya Ulaya (EIB).
Aidha, alisema miradi ya viwanja vya ndege iliyopo katika hatua za awali za utekelezaji ni pamoja na kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa viwanja vya ndege 10 vya Iringa, Njombe, Songea, Mtwara, Tanga, Kilwa Masoko, Lindi, Musoma, Singida na Manyara.

No comments:

Post a Comment