Tuesday, April 30, 2013

Ngurumo: CHADEMA ipuuze tuhuma za ugaidi


CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimeshauriwa kupuuza tuhuma za ugaidi na udini dhidi yake zinazoenezwa na Chama cha Mapinduzi (CCM).
Ushauri huo ulitolewa mjini hapa jana na mshauri wa CHADEMA, ambaye pia ni Mkurugenzi wa Vox Media, Ansbert Ngurumo, alipokaribishwa kutoa neno wakati wa kufunga hafla ya kuchangia harakati za M4C Geita, iliyofanyika Hoteli ya Gold Crest, jijini Mwanza.
Alisema CCM imekuwa na mazoea ya kurusha taarifa zisizo za ukweli dhidi ya vyama vya upinzani kila inaposhikwa pabaya.
Alisema dhana hiyo mbovu ya kuvibambikiza vyama vya upinzani hasa vyenye nguvu, ilianza miaka ya nyuma, ambapo Chama cha Wananchi (CUF), kiliundiwa njama hizo kwa lengo la kukidhoofisha.
Alisema wakati huo CUF iliundiwa zengwe la kujihusisha na ugaidi, tena kwa kusingiziwa kwamba imeingiza shehena ya visu, lakini hakuna kesi yoyote iliyofunguliwa na serikali, badala yake serikali ya CCM na CUF ziliamua kufunga ‘ndoa’ ya pamoja katika kuongoza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Bonyeza Read More Kuendelea




“Huu ni wakati wa Watanzania kubadilika kifikra na kimaamuzi. Serikali ya chama tawala imeanzisha siasa chafu za kubambikizia vyama vya upinzani vyenye nguvu kashfa mbaya ya ugaidi. Dhana hii ni hatari sana katika mustakabali wa maendeleo. Inalenga kudumaza na kuua upinzani nchini.
“Kama mnakumbuka kwa sasa CHADEMA inatuhumiwa na serikali kwamba ni chama cha kigaidi. Njama hizi chafu zilianzia CUF baada ya chama hicho kutuhumiwa kujihusisha na ugaidi, mbaya zaidi serikali ya CCM ilitangaza kukamata shehena ya visu ilivyodai vimeingizwa na CUF,” alisema mshauri huyo wa CHADEMA.
Ngurumo ambaye alidai kwa sasa maisha yake yako hatarini na hajui kama ataiona kesho, alisisitiza kwamba wananchi hata ndani ya CCM wanataka mabadiliko, kwa sababu wanaona mfumo uliodumu kwa miaka 50 unakaribia mwisho wake.
Alisema kazi ya kuleta mabadiliko si ya CHADEMA peke yake, bali ya wananchi wote katika nyanja na taaluma zote.
Aidha Ngurumo alisema mabadiliko ya msingi yanayotakiwa ni ya nafsi ya kila Mtanzania, na baadaye mabadiliko ya mfumo mzima, na lengo la mabadiliko ni kuinua maisha ya wananchi wa kawaida na kujenga mfumo wa utawala unaowajibika kwa wananchi.
Akisisitiza hoja kwamba mabadiliko hayaepukiki, alinukuu usemi wa aliyekuwa Rais wa Marekani, Thomas Jefferson, akisema: “Kila kizazi lazima kiwe na mapinduzi yake.”
Kwa upande wake, Kamanda wa M4C mkoa wa Geita, Alfonce Mawazo, na Ofisa Uwanda anayeshughulika na masuala ya Operesheni ya M4C Kanda ya Ziwa, Tungaraza Njugu, walisisitiza umuhimu wa wananchi kuiondoa CCM madarakani 2015, kwani ndiyo chanzo kikuu cha Watanzania kuwa umaskini.
Mawazo alisema safari ya CHADEMA kwenda vijijini kueneza elimu ya uraia ya kuikataa CCM kwa njia ya kura imeanza kuzaa matunda, kwani wananchi wengi wanaonyesha kuchukizwa na utawala wa chama tawala.
Katika hafla hiyo, ulifanyika mnada wa kuiuza keki maalumu iliyoandaliwa kwa ajili ya wajumbe, na kwamba keki hiyo ilinunuliwa na kada mmoja wa CHADEMA kwa zaidi ya sh 260,000, huku cheni moja ya mkononi na shingoni zilizotengenezwa kwa rangi ya bendera ya CHADEMA, kwa ujumla wake zilipigwa mnada na kununuliwa kwa sh 80,000.
Katika hafla hiyo iliyoandaliwa na CHADEMA kupitia kitengo chake cha Vuguvugu la Mabadiliko (M4C), Kanda ya Ziwa na kuhudhuriwa na wananchi, makada, wapenzi na mashabiki wa chama hicho kutoka maeneo mbalimbali ndani na nje ya mikoa ya kanda hiyo, iliingiza zaidi ya sh milioni 5.5.

No comments:

Post a Comment