LICHA ya kasoro lukuki katika uchaguzi wa wajumbe wa mabaraza ya Katiba ngazi ya kata, Tume ya Mabadiliko ya Katiba, imesema uchaguzi huo hautarudiwa.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Joseph Warioba, alisema kwenye masuala ya msingi maoni yanakinzana ambapo kila upande umetoa maoni.
Alisema kuwa tume iko tayari kufanya maamuzi magumu kuchukua baadhi ya maoni hayo na mengine kuyaacha, na vile vile aliwashauri wananchi nao wachukue maamuzi kama hayo kuyakubali kwani kila kundi likitaka mawazo yake yaingizwe kwenye Katiba hatutafika.
“Lazima kila mmoja wetu awe tayari kusikiliza mawazo ya wengine, na wakati wa kujadili mawazo ya Katiba ukifika tunaomba wananchi waipitie kuijadili na kutoa maoni bila woga kama walivyofanya wakati wa kukusanya maoni.
“Sisi tuko tayari, tutapeleka rasimu wananchi waijadili, tuko tayari kueleza kwa nini tumechukua mengine na kuacha mengine,” alisema.
Jaji Warioba aliwaomba wananchi wajadili bila kuingiliwa, akisema kuwa hawatengenezi Katiba ya vyama wala vikundi fulani, hivyo alionya makundi hayo yasiwalazimishe wazingatie mawazo yao.
Alisema kuwa wanaviomba vikundi hivyo visikilize maoni ya wananchi waseme ni Tanzania gani wanaitaka.
Akizungumzia kuhusu njia zilizotumika kuwapata wajumbe ambazo watu wanazilalamikia, Jaji Warioba alisema, “Hiki sio kitu kipya, wananchi wamezoea kuteua viongozi katika kamati mbalimbali, wana kamati za maji, kamati za shule, kamati za afya, kamati za maendeleo nakadhalika.
“Iweje linapokuja kwenye suala la mabadiliko ya Katiba ndiyo ionekane kuwa kuna mvutano wa kisiasa?” alihoji.
Jaji Warioba pia alitaja changamoto zingine zilizojitokeza katika uchaguzi kuwa ni baadhi ya maeneo ya uchaguzi wa vijiji, mitaa, shehia kutofanyika kutokana na mivutano ya kisiasa na kidini zilizosababishwa na baadhi ya wananchi kufungamanisha chaguzi za wajumbe wa mabaraza ya Katiba ya wilaya na masuala ya kisiasa.
Changamoto nyingine ilikuwa ni baadhi ya wananchi na vyama vya siasa kudhani kuwa mabaraza ya Katiba ya wilaya ni jukwaa la kutetea maslahi na misimamo ya vyama vya siasa kuhusu Katiba mpya.
Aliongeza kuwa baadhi ya wananchi kwenye mitaa, vijiji na shehia waliwakataa watendaji kuitisha mikutano licha ya viongozi hao kutambuliwa kwa mujibu wa sheria ya serikali za mitaa.
Jaji Warioba alisema kwa sasa katika kipindi hiki tume inaandaa rasimu ya Katiba na kuwahakikishia wananchi kuwa inafanya kazi kwa weledi na inayo dhamira na nia ya kutoa rasimu hiyo ambayo inazingatia maoni ya wananchi.
No comments:
Post a Comment