MIONGOZO mitatu iliyoombwa na wabunge, Zitto Kabwe, Tundu Lissu na John Mnyika, jana asubuhi ilisababisha Bunge kuahirishwa kwa muda kuiptisha bajeti ya Wizara ya Maji iliyowasilishwa bungeni wiki iliyopita na Profesa Jumanne Maghembe.
Kizazaa hicho kilitokana na hatua ya Waziri wa Fedha na Uchumi, William Mgimwa, kulitangazia Bunge kuwa ameongeza sh bilioni 184 kwenye bajeti hiyo ambayo awali ilikuwa sh bilioni 398 bila wabunge kugawiwa nakala.
Hata hivyo, Spika wa Bunge Anna Makinda alilazimika kumtaka Waziri Mgimwa kuja na nakala ya tamko la serikali kuhusu nyongeza hiyo ya bajeti iliyofanyika na kuisambaza kwa wabunge.
Pia aliitaka Wizara ya Maji kuja na vitabu vinavyoonyesha nyongeza ya mafungu ya miradi ya maji iliyoongezeka ili kutoa fursa kwa wabunge wakati wa kupitia vifungu hivyo.
Wiki iliyopita bajeti hiyo ilikwama baada ya wabunge wengi waliochangia mjadala wa hoja hiyo, kukataa kuiunga mkono kwa madai kuwa kiasi cha fedha kilichotengwa na serikali, hakiwezi kuondoa tatizo la maji nchini.
Kutokana na ufinyu huo, Spika Makinda aliagiza Kamati Ndogo ya Bajeti, Wizara ya Fedha na Wizara ya Maji, kukutana na kujadili namna ya kupata fedha za nyongeza katika nakisi ya bajeti hiyo.
Zitto (Kigoma Kaskazini) alisema kanuni inawataka mawaziri wa serikali kugawa nakala ya taarifa wanazozitoa bungeni ili wabunge waweze kuibana serikali pale inaposhindwa kutimiza mipango yake.
“Mheshimiwa Spika, waziri alipotangaza kwamba wameongeza fedha kwenye bajeti ya maji, ulimbana aseme wameongeza kiasi gani. Lakini kibaya zaidi, waziri hakuwa hata na kikaratasi, tamko la serikali linatolewa bila wabunge kupata nakala ya taarifa hiyo, jambo ambalo ni kinyume kabisa na kanuni za Bunge.
Bonyeza Read More Kuendelea
“Hapa tuna hofu kwamba tunapigwa changa la macho maana hakuna mahala ambapo serikali ‘inajikomiti’ na sisi tutashindwa kuibana,” alisema.
Zitto alitolea mfano wa Wizara ya Uchukuzi kwamba mwaka jana iliongezewa sh bilioni 94, lakini serikali hadi sasa imeshindwa kutoa fedha hizo, hivyo aliomba mwongozo wa Spika kama Mgimwa alikuwa sahihi au la.
Naye Lissu (Singida Mashariki), alitilia mkazo mwongozo wa Spika kwa kumtaka waziri awasilishe taarifa kwa wabunge kwa mujibu wa kanuni 49 (3).
Baadaye Mnyika (Ubungo), alitaka mwongozo kutaka Waziri wa Maji, kuwa Prof. Maghembe wakati akitangaza miradi ya maji iliyofanyiwa marekebisho kwa kuongeza fungu la bajeti, marekebisho hayo yaonekana kwenye vitabu vya wabunge ili iwe rahisi kufuatilia.
Akitoa mwongozo wake, Makinda alisema tatizo la waziri kutoa taarifa ya serikali na nakala kutosambazwa kwa wabunge, lilitokana na waziri huyo kupewa taarifa jana asubuhi hivyo hakuweza kujiandaa.
Hata hivyo, alimuagiza Waziri Mgimwa kuja na nakala ya taarifa ya serikali kuhusu marekebisho hayo wakati wa jioni.
Kuhusu wizara kutofanya marekebisho ya nyongeza ya mafungu ya fedha zilizoongezwa kwenye baadhi ya miradi ya maji nchini, Makinda alisema hali hiyo inatokana na ugeni wa kutumia Kamati ya Bajeti ambayo imefanya kazi kubwa ya kusaidia kuainisha maeneo ya mafungu yaliyoongezwa.
Baada ya mvutano wa hapa na pale katika baadhi ya vifungu, hatimaye bajeti hiyo ilipitishwa na wabunge.
No comments:
Post a Comment