Thursday, April 18, 2013

CHADEMA: Tupeni miaka mitano tuwaoneshe uongozi


CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimesema serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), imedumaa kupeleka maendeleo kwa Watanzania, hivyo kimewaomba Watanzania wakipatie fursa ya kuongoza nchi hata kwa miaka mitano ili kioneshe uwezo wa kuwatumikia wananchi.
Kauli hiyo ilitolewa juzi na Mkurugenzi wa Sera na Utafiti wa CHADEMA taifa, Waitara Mwita, alipohutubia mkutano wa hadhara uliofanyika uwanja wa Mbuzi mjini Mugumu wilayani hapa.
Alisema kadiri siku na miaka inavyokwenda Watanzania wanazidi kuwa maskini, licha ya kuwapo rasilimali  nyingi, na kuongeza kuwa matatizo hayo yanasababishwa na serikali ya CCM isiyojali maisha ya wananchi wake.
Kutokana na hali hiyo, Waitara aliyewahi kuwa Katibu wa CCM Mkoa wa Tanga kabla ya kujiunga na CHADEMA, aliwaomba Watanzania waipe CHADEMA nafasi ya kuongoza nchi japo kwa miaka mitano ili itoe mfano wa namna nchi inavyoongozwa kwa kuwaletea wananchi maendeleo.
“CHADEMA hatuhitaji miaka 50 ya CCM, tunahitaji miaka mitano tu, ili muweze kuona mabadiliko ya kimaendeleo hapa nchini. Rasilimali zilizopo lazima zitatumika vema katika uongozi wote wa CHADEMA,” alisema Waitara.
Awali, ofisa kutoka Kurugenzi ya Kampeni na Uchaguzi wa CHADEMA taifa, Ali Bananga, alisema CCM imewageuza Watanzania kama kuku wa kienyeji ama makarai ya zege na mifagio isiyokuwa na thamani, baada ya nyumba kupendeza.
Bananga alisema wananchi wengi wanaoipigia kura CCM ni sawa na mifagio na makarai, hivyo hawana budi kuondokana na giriba wakati wa uchaguzi.

No comments:

Post a Comment