Monday, April 22, 2013

Mbowe amliza Chami


Maendeleo ya ujenzi wa barabara ya lami katika Jimbo la Hai yamemliza  Mbunge wa Moshi Vijijini (CCM), Dk. Cyril Chami na amelalamika rasmi kwa Wizara ya Ujenzi.

Chami, ambaye alikuwa Waziri wa Viwanda na Biashara hadi mabadiliko yaliyotokea mwaka jana, amelalamikia maendeleo hayo ya Jimbo la Hai linalopakana na la kwake akisema yanazidi kuwapa wananchi nguvu ya kuchagua upinzani.

Jimbo la Hai linaongozwa na Freeman Mbowe (Chadema), ambaye pia ni Mwenyekiti wa chama hicho na Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni.

Katika barua yake kwenda kwa Naibu Waziri wa Ujenzi, Injinia Gerson Lwenge ya Februari 4, mwaka huu, Chami anatoa mfano wa barabara ya Rau Madukani-Mamboleo-Kishumundu iliyopo Kata ya Uru Mashariki iliyojengwa na Serikali ya Tanu kwa kiwango cha lami mwanzoni mwa miaka ya 1970.

Chami alisema barabara hiyo tangu wakati huo, ikiharibika haikarabatiwi kwa kurudishia lami bali hujazwa kifusi, kitu ambacho anadai ni kinyume kabisa na taratibu za ukarabati wa barabara za kiwango cha lami.

Alisema hali hiyo ni tofauti katika barabara ya Machine Tools kwenda Machame iliyopo Jimbo la Hai iliyojengwa miaka ya 1950 ambayo Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) Mkoa wa Kilimanjaro kila inapoharibika hukarabatiwa kwa kurudishia lami.

“Tanroads Mkoa wa Kilimanjaro hufanya ukarabati wa barabara ya lami inayoanzia Machine Tools kwenda Machame iliyojengwa miaka ya 1950 kwa kurudishia lami kila inapoharibika, na ni vigumu kuelewa sababu ya kutokufanya hivyo kwa barabara ya Rau Madukani-Mamboleo-Kishumundu,” alilalamika Chami katika barua yake hiyo.

Chami katika barua yake hiyo ambayo nakala ameipeleka kwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Leonidas  Gama na kwa Meneja wa Tanroads mkoa huo, alisema kinachoongeza kutoelewa ni ukweli kwamba barabara ya Machine Tools-Machame iko katika Jimbo la Hai ambalo linaongozwa na Chadema.

Katika barua hiyo ambayo NIPASHE imefanikiwa kuona nakala yake, alisema kutokana na hali hiyo, viongozi wa Chadema wanawakejeli wananchi wa Moshi Vijijini walioichagua CCM kuwa barabara yao (watu wa Hai) ya Machame inakarabatiwa kwa lami kwa sababu wao waliichagua Chadema na kwamba kinachoifanya barabara hiyo ya Moshi Vijijini ijazwe kifusi ni kwa sababu waliichagua CCM. 


Bonyeza Read More Kuendelea
 




“Mheshimiwa, nakuomba uingilie kati ili Tanroads Mkoa wa Kilimanjaro wawajibike na barabara hii ya Rau Madukani-Mamboleo-Kishumundu, kama wanavyowajibika kwa ile ya Machine Tools-Machame,” alieleza Chami katika barua hiyo. Chami amebainisha kuwa kutokufanya hivyo ni kutoa taswira kuwa maeneo yanayoongozwa na Chadema  yanapewa kipaumbele zaidi na Serikali ya CCM kuliko maeneo yanayoongozwa na CCM yenyewe.

Alisema visingizio kuwa barabara hiyo ya Rau Madukani-Mamboleo-Kishumundu (ya miaka 1970) iko chini ya usimamizi wa Halmashauri ya Wilaya ya Moshi, havina mashiko maana kama hiyo ni halali, wananchi wanauliza kwa nini basi barabara hiyo ya Machame (ya miaka ya 1950) nayo isirudishwe Halmashauri ya Wilaya ya Hai.

Mbali na barabara hizo, Chami pia amekumbushia barabara ya Kibosho Shine-Kwa Rafael-International School  yenye urefu wa kilomita 43, ni ahadi ya Rais wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa 2005 na 2010.

Alisema hadi sasa ni kilomita 19 tu za barabara hiyo zimejengwa kwa viwango mbalimbali na kwamba kinachomtia hofu ni pale alipoongea na Meneja wa Tanroads Mkoa wa Kilimanjaro ambaye ni mgeni, alielekea kutokuwa na uhakika wa urefu wa barabara hiyo.

“Hofu yangu ni kwamba tusipokumbushana ahadi hii kwa ukamilifu, kuna uwezekano zikishakamilika hizo kilometa 19 ikachukuliwa kuwa kazi imekamilika, jambo ambalo si sahihi. Mheshimiwa Waziri, barabara hii iko kwenye llani ya Uchaguzi ya CCM (2010-2015) na endapo haitakamilika mwaka 2015, wapinzani watakipa CCM wakati mgumu sana katika Jimbo la Moshi Vijijini,” alisema Chami.

Alisema barabara nyingine ambayo ipo katika ahadi ya Rais ni ya Rau Madukani-Mawella-Njari aliyoahidi kuwa itajengwa kwa kiwango cha lami ambayo ina urefu wa kilomita 12.5, zinazojengwa kwa sasa ni kilomita tisa na kwamba kilomita tatu hazijaguswa kabisa.

Barabara ya Old Moshi inayoanzia barabara kuu iendayo Dar es Salaam kupitia Kiboriloni Primari, kijiji cha Kikarara, kijiji cha Tsuduni hadi kijiji cha Kidia (km 19.8) katika Kata ya Old Moshi Mashariki, pia ni ahadi nyingine ya Rais aliyoitoa wakati wa kampeni za 2010 eneo la Tsuduni na imeingizwa kwenye Mpango wa Maendeleo wa 2011-2016, alisema Chami.

“Inaelekea ahadi ya barabara hii hata haifahamiki kabisa, kwa sababu hata katika taarifa mbalimbali kwa viongozi wa kitaifa wanaotembelea Kilimanjaro haisikiki. Kumbe nimeona niukumbushe uongozi wa Tanroads mkoa na wa Wizara ya Ujenzi juu ya barabara hii, japo natambua uwapo wa mawasiliano kati ya Mama Anna Mkapa (mzaliwa wa Kijiji cha Kikarara) na Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi Dk. John Magufuli juu ya ujenzi wa barabara hii,” alieleza Chami.
Chami alisema amemua kuyaleta hayo si kama mashitaka kwa uongozi wa Mkoa wa Kilimanjaro bali kama njia ya kukumbushana na kuwaomba viongozi wa ngazi zote washirikiane ili ahadi hizo za Rais zitekelezwe kwa wakati, na pia pale palipo na kasoro parekebishwe.

Chami alipotafutwa kwa simu yake ya mkononi kwa kupigiwa mara kadhaa ilikuwa haipatikani na hata alipotumiwa ujumbe mfupi wa simu (sms), hakuujibu.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Leonidas Gama, alipoulizwa kuhusu barua hiyo ya Chami alisema alikuwa safarini mkoani Dodoma na kwamba kama ameiwasilisha ofisini kwake ataiona leo (Jumatatu).

Gama alisema wakati akiwa mjini Dodoma alikutana na Chami na kumjulisha suala la barua hiyo kuhusiana na barabara hizo na itabidi aangalie kama kweli barabara hizo zinazolalamikiwa na mbunge zipo katika ahadi ya Rais.

Malalamiko ya Chami kuhusu barabara hizo yamekuja katika kipindi ambacho kumebakia takriban miaka miwili kufanyika kwa uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment