Monday, April 22, 2013

Dodoma waapa kuing’oa CCM 2015

Pichani Mwenyekiti wa Chadema Mh. Freeman mbowe akipandisha bendera kuashiria uzinduzi wa Kanda ya Kati, mkoani Dodoma.

WAKAZI wa Mji wa Dodoma wameapa kuking’oa Chama cha Mapinduzi (CCM) madarakani kutokana na kushindwa kutatua matatizo ya umaskini kwa zaidi ya miaka 50 sasa.
Wakazi hao walionyesha msimamo wao juzi katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya Wajenzi mjini hapa wakati wa uzinduzi wa Vuguvugu la Mabadiliko (M4C) Kanda ya Kati na kuhutubiwa na Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, Freeman Mbowe.
Walisema wamechoshwa na umaskini, uonevu pamoja na ufisadi wa rasilimali zinazoibwa na watu wachache serikalini huku wakiendelea kulindana badala ya kuwajibishana.
Akizungumza katika mkutano huo, Mbowe alisema kwa sasa chama kimelazimika kushusha madaraka hadi ngazi ya kitongoji.
Alisema lengo ni kuhakikisha kila Mtanzania hata aliye kijijini anaelewa sera na madhumuni ya chama, ili kukiwezesha chama hicho kushika dola mwaka 2015 ikiwa ni kuanzia ngazi ya matawi katika uchaguzi wa mwaka 2014.
Aidha, alisema kamwe CCM haiwezi kumkomboa Mtanzania, kwani viongozi ndani ya serikali wamekuwa ndio wanaotawala mali nyingi na ndiyo maana kuna watu wachache wana maisha mazuri na kundi kubwa la watu ni maskini.
“Mali zote za Tanzania zinamilikiwa na kundi la watu wachache ambao wanajiita Baraza la Mawaziri, kundi hilo ndilo linakaa na kuwapangia Watanzania zaidi ya milioni 44, waishije na rasilimali za nchi ziwafae au waendelee kuwa maskini.
“Hali hii kamwe haiwezi kuvumiliwa; ni lazima makamanda wa CHADEMA kujipanga na kushika dola, ili Watanzania wanufaike na rasilimali za nchi,” alisema Mbowe.
Mbowe alisema katika kipindi cha miaka 22 tangu CHADEMA ilipoanzishwa, ina mbunge mmoja wa kuchaguliwa, Tundu Lissu wa Singida Mashariki, na watatu wa viti maalumu Suzan Kiwanga, Christowaja Mtinda na Christina Lissu katika kanda hiyo inayojumuisha mikoa ya Singida, Dodoma na Morogoro.
Alisema hali hiyo ilitokana na chama kutofika ngazi ya chini, lakini mpango huo unalenga kupoka madaraka ya chama kutoka makao makuu ya Dar es Salaam, kuyafikisha ngazi ya kanda, wilaya, kata vijiji hadi chini.

No comments:

Post a Comment