Monday, April 22, 2013

HOTUBA YA MSEMAJI MKUU WA KAMBI YA UPINZANI WIZARA YA KILIMO, CHAKULA NA USHIRIKA MHESHIMIWA ROSE KAMILI SUKUM (MB) KUHUSU MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA WIZARA KWA MWAKA WA FEDHA 2013/2014

(Inatolewa Chini ya Kanuni ya 99(9)toleo la mwaka 2013)
A.    DHANA YA KILIMO KWANZA

Mheshimiwa Spika, Kwa mujibu wa mpango wa serikali katika utekelezaji wa dhana ya kilimo kwanza, serikali ilijiwekea nguzo kuu kumi katika utekelezaji wa mpango huo, na pia iliweka ukomo wa utekelezaji wa mpango huo kuwa ni mwaka 2015. 
Mheshimiwa Spika, nguzo kuu kumi za utekelezaji dhana ya kilimo kwanza zilizopitishwa na serikali zilikuwa  kama ifuatavyo ;
i.                    Dira ya taifa ya kilimo kwanza : Hii ililenga kuhakikisha kuwa kilimo cha wakulima wadogo, wa kati na wakubwa kiwe cha kisasa na cha kibiashara ifikapo mwaka 2015
ii.                 Kugharamia kilimo kwanza: Hii ililenga kuongeza bajeti ya serikali kwa ajili ya kilimo, kuanzisha Benki ya Maendeleo ya Kilimo yenye mtaji wa kuanzia dola za kimarekani milioni 500 Desemba 2009, kuanzisha mfuko maalum wa fedha za kilimo kwanza.
iii.               Muundo mpya wa Taasisi kwa ajili ya usimamizi: Hii ilikuwa ni pamoja na kuanzisha utaratibu wa uhusiano na wizara nyingine zinazohusiana na maswala ya kilimo na kuimarisha vyama vya wakulima.
iv.               Mabadiliko ya mfumo wa kimkakati : Hii ilikuwa ni pamoja na kubainisha maeneo ya vipaumbele kwa ajili ya vyakula muhimu ili nchi ijitosheleze kwa chakula.
v.                 Ardhi kwa ajili ya kilimo kwanza: Hii ilikuwa ni pamoja na kurekebisha sheria ya Ardhi ya Vijiji Na 5 ya 1999 ifikapo 2010 ,kuharakisha mfumo wa upatikanaji ardhi, kuharakisha utatuzi wa migogoro ya ardhi, kutenga ardhi kwa ajili ya uwekezaji wa kilimo.
vi.               Vivutio kwa ajili ya kilimo kwanza : Hii ilikuwa ni pamoja na kuondoa vikwazo vya masoko kwa mazao ya kilimo, kuimarisha utumiaji wa vipimo na viwango halali katika biashara na kuboresha bei ya mazao.
vii.            Viwanda kwa ajili ya kilimo kwanza : Hii ilikuwa ni pamoja na kuanzisha viwanda kwa ajili ya kushughulikia mahitaji ya wazalishaji wa kilimo,kuongeza uzalishaji na matumizi ya mbolea,kuboresha uzalishaji wa mbegu na dawa za kilimo, uzalishaji wa zana na vifaa vya kilimo
viii.          Sayansi,Teknolojia na rasilimali watu: Hii ilikuwa ni pamoja na kuanzisha bodi ya usajili ya wataalamu wa kilimo,kulipia mikopo ya gharama zote za masomo kwa wanafunzi wa vyuo vikuu vya kilimo,kuanzisha vituo vya hali ya hewa katika ngazi ya kata.
ix.               Miundombinu kwa ajili ya kilimo kwanza : Hii ilikuwa ni pamoja na kujenga miradi ya umwagiliaji ya kutosha, kujenga vituo vya masoko kila kata,kupelekea umeme vijijini kwa ajili ya kuboresha kilimo
x.                  Uhamasishaji wa watanzania kwa ajili ya kilimo : Hii ilikuwa ni pamoja na kuhamasisha shule na vyuo kushiriki kwenye kampeni ya kilimo kwanza, viongozi wa ngazi zote kushiriki katika kilimo binafsi.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inayoongozwa na CHADEMA, inataka kupata majibu ya kina juu ya utekelezaji wa nguzo hizi kumi za kilimo kwanza na hasa ikizingatiwa kuwa huu ni mwaka 2013 na kwa maana hiyo, imebaki  miaka miwili tu ili utekelezaji wa nguzo hizi uwe umekamilika.

B : BENKI YA KILIMO
Mheshimiwa Spika, ili kuwezesha shughuli za Kilimo, Serikali ilikuwa na mpango wa kuanzisha Benki ya Kilimo, ambapo kulikuwa kunahitajika mtaji wa shilingi bilioni 750 kwa ajili ya kuanzisha benki hiyo. Hata hivyo, mpango huu umekuwa ukisuasua na matokeo yake benki hiyo imekuja kuanzishwa na mtaji wa shilingi bilioni 60 kinyume na mpango wa awali wa  mtaji wa shilingi bilioni 750.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kutoa majibu ya kina kama fedha   hizi zitatosha kulingana na mpango wa utekelezaji. Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inataka kujua kama mtaji huu wa shilingi bilioni 60 ni sehemu ya marejesho ya fedha za EPA kama Bunge lilivyokuwa limeelezwa kuwa fedha za EPA zitaelekezwa kwenye kilimo.

Kuendelea Bonyeza Read More



C : MWENENDO WA KILIMO NCHINI
Mheshimiwa Spika, Tangu mwaka 1996 hadi 2012 uchumi wa Tanzania umekuwa  ukikua kati ya  asilimia 3.5 hadi 7.8, na kwa kipindi cha mwaka jana inaonyesha kuwa uchumi ulikuwa kwa asilimia 6.5[1]  Aidha, Kasi ya ukuaji katika sekta ya kilimo ambayo inaajiri takribani asilimia 75 ya nguvukazi nchini ilipungua, kutoka asilimia 4.2 mwaka 2010 hadi 3.6 mwaka 2011. Ni ukweli uliowazi kuwa taarifa hiyo ya ukuaji wa uchumi haiendani na hali halisi ya maisha ya wananchi. Mafanikio yanayotajwa yameshindwa kuondoa umasikini kwa wananchi hasa wale wanaoishi vijijini.
Mheshimiwa Spika, Tanzania bara ina jumla ya eneo la hekta milioni 29.4 linaloweza kufanya uzalishaji kwa umwagiliaji, lakini ni karibu eneo la hekta laki 330,000 tu (sawa na 1.1% tu ya eneo linalofaa kwa umwagiliaji) ndilo kwa sasa linafanya uzalishaji kwa umwagiliaji.
Mheshimiwa Spika, Kilimo ni biashara kama zilivyo biashara nyingine, hivyo ili kiweze kupiga hatua ni lazima mazingira ya kufanyia biashara hiyo ya kilimo yaboreshwe ili wakulima wadogo na wale ambao wasiojihusisha na kilimo wavutiwe kufanya biashara hiyoKatika mazingira ya nchi yetu, wakulima wadogo ndio wadau wakubwa wa kilimo, hivyo basi changamoto za kuongeza tija ndio kikwazo cha kuifanya sekta hiyo kukua na kuondoa au kupunguza umasikini.
Mheshimiwa Spika, Mfumuko wa bei unauhusiano wa moja kwa moja na maisha ya watanzania wengi. Kupanda kwa bei za vyakula kwa zaidi ya asilimia 50%  maana yake  ni kushuka kwa uwezo wa manunuzi(Kipato) kwa wananchi masikini waishio mijini kwa asilimia 25%(Kwa kutilia maanani kuwa familia hizo hazizalishi chakula).
Sambamba na hilo ni kuwa kipato kikubwa kwa kipindi hicho kinatakiwa kiende kwa wakulima wazalishaji wa chakula[2].
Mheshimiwa Spika, changamoto kubwa kwa kilimo  ni jinsi ya kuongeza tija kwa eneo dogo la ardhi inayotumiwa na wakulima wadogo kwa kulinganisha na nguvu kazi inayojihusisha katika kilimo. Changamoto hii inaweza kuondolewa kirahisi kama mahitaji muhimu katika kufanikisha kilimo yatapatikana  yakiwa na ubora na kwa wakati, mahitaji hayo ni huduma za ushauri, pembejeo bora (mbegu,madawa) miundombinu ya umwagiliaji, huduma za kibenki, masoko ya uhakika n.k
Mheshimiwa Spika, Serikali hii ya CCM inajuua kwamba bila kuwekeza kikamilifu katika Kilimo, umasikini utaendelea kulitafuna taifa hili, lakini bado sioni dhamira ya dhati ya Serikali kuwekeza katika Kilimo. Nasema hivi kwa sababu mwezi Agosti, 2010, aliyekuwa Waziri wa kilimo wakati huo, Mhe. Stephen Masatu Wassira, alisema kwamba; Msingi wa maudhui ya azma ya KILIMO KWANZA, ni kukiri kwamba, haiwezekani kukuza uchumi wa Tanzania na kiwango cha kupunguza umaskini kwa Watanzania walio wengi bila kuwekeza kwa kiwango cha kuridhisha katika Sekta ya Kilimo.”
Mheshimiwa Spika, nikumbushe  Bunge hili kuwa Tanzania iliridhia na kujiunga na mpango wa maendeleo kusini mwa Afrika, CAADP, tangu ulipoasisiwa mwaka 2003. Pamoja na malengo mengine mpango huu ulilenga kuongezwa kwa bajeti kwa sekta ya Kilimo hadi 10% ya Pato ghafi la Taifa (GDP). Hii inajulikana zaidi kama azimio la Maputo-Msumbiji,  ambalo lilizitaka nchi zote mwanachama wa African Union (AU) kutenga asilima 10 ya bajeti zao kila mwaka kwa ajili ya kilimo.
Mheshimiwa Spika, Tanzania imekuwa na mipango mingi ya kilimo na kwa sasa tayari kuna mpango mpya uitwao TAFSIP- (Tanzania Agriculture Food Security Investment Plan)  ambao ni Mpango wa miaka 10 ijayo wenye lengo la kukifanya kilimo kiweze kuchangia katika ukuaji wa uchumi, kuongeza pato la mkulima na taifa kwa ujumla na kuhakikisha kwamba taifa linajitosheleza kwa chakula na lishe.
Mheshimiwa Spika, Mpango huo umeandaliwa kwa kuzingatia yaliyomo katika miongozo na mifumo ya kutekeleza Dira ya Maendeleo yaani Vision 2020 na 2025, Programu za kitaifa yaani MKUKUTA, KILIMO KWANZA, ASDP na Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2011/2012- 2015/16).

Mheshimiwa Spika, TAFSIP imeainisha maeneo makuu saba (7) ya uwekezaji ili kufikia lengo la asilimia 6 ya ukuaji wa sekta kila mwaka na kwamba Serikali itaongeza bajeti yake hadi kufikia asilimia 10 kama Mpango wa Kuendeleza Sekta ya Kilimo Barani Afrika yaani Comprehensive Africa Agriculture Development Programme (CAADP)  inavyoelekeza.
Mheshimiwa Spika, gharama za kutekeleza mpango kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka wa fedha 2011/2012 – 2015/16 ni shilingi za kitanzania trilioni 8.7 au dola za kimarekani bilioni 5.3. Wastani wa mahitaji ya fedha kwa mwaka ni shilingi trilioni 1.7

D : MPANGO WA KUKUZA KILIMO KATIKA UKANDA WA KUSINI MWA TANZANIA  (southern agricultural growth corridor of tanzania – SAGCOT).
Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa ikihamasisha na kuvutia uwekezaji wa Sekta Binafsi  katika kilimo na kujenga dhana ya kibiashara biashara kama ilivyoainishwa katika nguzo ya pili ya KILIMO KWANZA ambayo pia umeanza kutekelezwa kupitia Mpango wa Kukuza Kilimo katika Ukanda wa Kusini mwa Tanzania (Southern Agricultural Growth Corridor of Tanzania – SAGCOT). Mpango huo unalenga zaidi kuvutia uwekezaji katika kilimo kwa ushirikiano baina ya wakulima wakubwa na wadogo katika maeneo husika.
Mheshimiwa Spika, uwekezaji wowote ambao unalenga kuondoa njaa bila ya kuondoa umasikini kwa wakulima, huo ni mpango mwingine wa kutuharibia ardhi yetu na unatakiwa ukaribishwe kwa tahadhari kubwa katika nchi yetu. Hii inatokana na ukweli kwamba uwekezaji katika kilimo unatakiwa ufanywe kwa wakulima wadogo na wa kati kwani ndio sehemu kubwa ya jamii inayojihusisha na kilimo.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kuwekeza zaidi kwenye kada hizo mbili za wakulima. Aidha, tunaitaka Serikali kuchagua aina ya kilimo kitakacho harakisha kuondoa umasikini kwa wananchi wetu.
Mheshimiwa Spika, ujio wa SAGCOT hapa nchini, unapata uhamasishaji mkubwa kutoka ndani na nje, kwa dhana kuwa ndio mkombozi wa tatizo la njaa hapa nchini. Ujio huo unakuja pia na washirika wake ambao ni makampuni makubwa Duniani yanayozalisha Mbolea na  Mbegu pamoja na madawa yakiwa kama washirika katika mpango huo wa uwekezaji mkubwa kwenye kilimo.
Mheshimiwa Spika, makampuni hayo washirika katika mpango huo, sio kwamba itakuwa ni mara ya kwanza hapa Tanzania bali washirika hao wamefanyakazi mataifa mengi hapa Duniani. Moja ya nchi hizo ni India.
Maandiko na taarifa mbalimbali kuhusiana na mpango kama huu wa SAGCOT kwenye nchi ya India zinaonyesha kuwa wakulima wadogo na wakati wamekuwa ni majeruhi wakubwa wa makampuni hayo yanayozalisha mbegu, madawa na kutoa mbolea. Makampuni ya mbegu hasa za pamba yamesababisha wakulima kujiua.
Mheshimiwa Spika, kutokana na utafiti uliofanywa na Wizara ya Kilimo nchini India iliishauri Serikali ya nchi hiyo kusitisha uuzwaji wa mbegu za pamba aina ya Bt-Cotton zilizokuwa zinazalishwa na kusambazwa na Kampuni ya Monsanto, ambayo ilitumia fedha nyingi kuwashawishi wakulima kuachana na mbegu zao za asili na kutumia mbegu zilizokuwa zinazalishwa na Kampuni hiyo.  Mbegu hizo zilionyesha ni ghali sana kwa asilimia 100 kulinganisha na mbegu za asili za Pamba, mbali ya ughali huo mbegu hizo zilionekana kuwa hazina uwezo wa kuota katika msimu unaofuata, jambo ambalo linazidisha kuongeza matatizo kwa wakulima.
Mheshimiwa Spika, ukweli uliotolewa na Wizara ya Kilimo ya India ni kwamba  zaidi ya wakulima wadogo  1,000  wanajiua kila mwezi kutokana na kukidhiri kwa madeni yanayo limbikizwa kutokana na mbegu zizalishwazo na Monsanto.  Hilo limepelekea  wakulima wadogo zaidi ya 125,000  kujiua[3].
Mheshimiwa Spika, kitendo chochote kitakachopelekea wakulima wadogo kununua mbegu ambazo haziwezi kutunzwa na kuoteshwa zaidi ya msimu mmoja, Kambi Rasmi ya Upinzani inauweza kukiita kitendo hiki kuwa ni hujuma. Taarifa  hiyo inaendelea kusema kuwa uzalishaji mkubwa ni kwa miaka mitano ya mwanzo tu, na baada ya kipindi hicho maafa yanafuatia.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kufanya tathmini ya kina kuhusu ujio wa makampuni hayo ya mbegu kwani kwa historia na maandishi niliyoyaweka hapo juu ni janga lingine linalokuja kwa wakulima wadogo na  kilimo chetu kwa ujumla.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inataka kujua mpango huo ni maeneo gani ambayo yako wazi kwa ajili ya uwekezaji zaidi ya kunyang’anya wakulima wadogo mashamba yao (land grabbing) ambayo ndipo tunapoelekea. Aidha, wizara ya kilimo imekuwa ikihamasisha uwekezaji katika kilimo kupitia vijarida vyake vikiainisha maeneo yenye fursa ya kilimo (Investment potential and opportunities in agriculture).
Mheshimiwa Spika, fedha zilizotengwa  na kuidhinishwa mwaka jana  kwa ajili ya SAGCOT ni shilingi bilioni 6.567  kwa mwaka huu zimetengwa  kwa ajili ya uendeshaji wa mradi huo ni shilingi bilioni 3.827,  hizi sio  za uwekezaji na ni fedha za ndani. Hoja ni kwanini fedha hizi za ndani zimetengwa kidogo kwa kulinganisha na mwaka jana ? Je ni kweli Mradi huo ni kipaumbele cha Taifa kama inavyodaiwa ? Mwaka wa fedha unaomalizika  fedha zilizotolewa na hazina ni shilingi bilioni 1.75 lakini zilizotumika hadi Machi 2013 ni asilimia 77 tu. Je na hizo zilitumika katika uendeshaji badala ya uwekezaji? Na wakulima wadogo na wa kati wamenufaika vipi katika mgawo wa awamu ya kwanza ya fedha hizo za SAGCOT?
Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani inataka kuelewa ni maeneo gani yaliyoanishwa yako wazi na hayatumiki kwa shughuli nyingine zaidi ya kilimo kwani tumekuwa tukiambiwa serikali inaandaa land bank. Kambi inataka kujua ni maeneo gani yaliyoainishwa kwa ajili ya matumizi mbalimbali ikiwemeo kilimo, mifugo na makazi kuondokana na migogoro inayoendelea hivi sasa.
Mheshimiwa Spika, mjumuiko wa asasi za kiraia  ulikaa na kutoa ushauri kwa Serikali katika bora kutekeleza  mpango wa SAGCOT ili vijiji vinavyotoa ardhi kwa ajili ya uwekezaji wa mpango huo vinufaike na uwekezaji huo katika chapisho lao[4]. Ushauri huo ni kama ifuatavyo :
1)   . Kuweka wazi jinsi gani upatikanaji wa ardhi na mchakato mzima wa uwekezaji na jinsi wazalishaji wadogo na wa kati wanaozunguka maeneo ya uwekezaji  watakavyopata mitaji.
2)   Matumizi bora ya ardhi katika vijiji ambavyo vitatoa ardhi kwa ajili ya uwekezaji wa SAGCOT yawekwe chini ya uangalizi huru ili kuepuka mgongano wa kimaslahi.
3)   Eneo la ardhi ya vijiji litakalotolewa kwa msingi wa uwekezaji wa SAGCOT  libaki kama eneo la vijiji kwani baada ya mradi kumalizika lirudi katika umiliki wa vijiji badala ya  eneo hilo kutwaliwa na Serikali kuu.
4)   Vijiji vinavyotoa ardhi ya uwekezaji ni lazima vipatiwe washauri waelekezi ambao ni huru ili watoe tathmini  huru isiyoegemea upande wowote.
5)   Mpango mkubwa wa uwekezaji wa SAGCOT katika umwagiliaji ni lazima ulazimike  kutoa huduma hiyo kwa jamii za wakulima wanaozunguka mradi huo.
6)   Umwagiliaji ujikite katika kuhakikisha makubaliano ya matumizi bora ya maji na ufuatiliaji wa mara kwa mara unafanyika.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kulieleza Bunge na watanzania wote utekelezwaji wa ushauri huo wa ASASI za kiraia hadi sasa umefikia wapi?
E : HALI YA CHAKULA NCHINI
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa mpango wa maendeleo wa miaka mitano unaonyesha kuwa kipaumbele cha pili ni kuwekeza katika Sekta ya Kilimo kwa tafsiri pana ambayo inajumuisha Sekta ya Kilimo cha mazao ya chakula na biashara,  Sekta ya Mifugo, Uvuvi, Ufugaji wa Nyuki na Rasilimali za Misitu. Shabaha Kuu ya kuendeleza Kilimo ni kuleta Mapinduzi ya haraka ya Kilimo yatakayotuwezesha kuongeza uzalishaji na tija ili kujitosheleza kwa chakula na kuuza ziada nje.
Mheshimiwa Spika, Kiwango cha ukuaji katika kilimo hakijafikia lengo lililowekwa na serikali la kufikia ukuaji wa asilimia 10 kwa mwaka kuanzia 2008 – 2015; na ukosefu wa chakula bado ni tatizo kwa watu wengi. Kiasi kikubwa cha kaya zisizokuwa na chakula cha kutosha zipo vijijini ambapo kilimo kinatagemewa sana kama chanzo cha kipato
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa taarifa ya Bwana Philipe Egger[5]  kwenye Jarida la ILO la mwezi Februari,2013 inaonyesha kuwa Africa inaagiza chakula chenye thamani ya karibu dolla za kimarekani bilioni 50 kwa kila mwaka kwa ajili ya kulisha wakaazi wa miji inayokuwa kwa haraka sana. Inakisiwa kiasi hiki ni karibu sawa na misaada ya maendeleo inayotolewa na nchi zilizoendelea.

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Tanzania uingizaji mkubwa wa chakula kutoka nje hufanywa si kwa sababu Tanzania haina chakula cha kutosha kuweza kukidhi mahitaji ya wananchi bali ni mkakati unaotumiwa na baadhi ya watendaji kuhakikisha kuwa nguvu za wakulima hazitoi matunda na wakulima wazidi kuwa masikini. Mfano mzuri ni uingizaji wa mchele kutoka ‘Thailand’ wakati wakulima wa mikoa ya Morogoro na Mbeya wakikosa soko la kuuza mchele wao. Kambi ya Upinzani inaliona hili kuwa ni hujuma kwa wakulima wa Tanzania.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kuwaeleza wakulima ni kwanini inatoa vibali vya kuingiza nchini mchele wakati mchele upo mwingi kwa wakulima?
Mheshimiwa Spika, naomba kunukuu sehemu ya hotuba ya mhe Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-Mipango  ya mwaka 2012/2013 aliyoitoa hapa Bungeni Mheshimiwa Spika, katika kukabiliana na mfumuko wa bei, Serikali ilichukua hatua zifuatazo: kuhakikisha usambazaji wa chakula katika maeneo yenye uhaba wa chakula; kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula; kuendelea kuimarisha hifadhi ya chakula kwa kuongeza ununuzi wa mazao ya chakula;…….’. Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali iwaeleze watanzania  ni wapi inapozalishia chakula ! Hoja ni kwamba hata chakula kilichonunuliwa kutoka kwa wakulima, kilinunuliwa kwa mkopo, mfano ni wakulima wa Halmashauri ya Nkasi  mkoani Rukwa  ambao wanaidai wakala ya Hifadhi ya chakula  ya Taifa zaidi ya shs milioni 500[6].
Mheshimiwa Spika, huu ni mwaka wa pili wa utekelezaji wa mpango wa maendeleo wa miaka mitano, kwa masikitiko makubwa ni kwamba bado tatizo kubwa la ukosefu wa chakula limeripotiwa kutokea katika wilaya mbalimbali za nchi yetu kutokana na kutokuwepo kwa mfumo mzuri wa usambazaji wa chakula kutoka kinapozalishwa kwa wingi, baadhi ya wilaya hizo ni : Kilindi, Meatu, Iringa, Handeni  kati ya August hadi februari 2013 kaya  zaidi ya 780 wilayani humo  zikakabiliwa na njaa. Kwa kipindi hicho, wananchi wapatao 81,769 wa kata 12 wilaya ya moshi mkoani Kilimanjaro walihitaji chakula cha msaada tani 14,634.6 ili kukabiliana na tatizo la njaa ambalo limeonekana kuathiri shughuli nyingi za kimaendeleo.
Mheshimiwa Spika, Kwa ujumla hali ya chakula nchini sio nzuri  na Serikali haionekani kuchukua hatua stahiki kumaliza tatizo hilo, kutokana na ukweli kwamba mamlaka zilizopewa jukumu la kuhakikisha wahanga wanapewa msaada wa dharura haraka badala yake mamlaka hizo zinafanyakazi hiyo kwa kuangalia itikadi za wanasiasa katika maeneo ya wahanga. Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kuhakikisha kuwa mamlaka husika zisiingiliwe na watendaji wa kisiasa jambo linalopelekea mamlaka hiyo kupoteza uhalali wa kuitwa kitengo cha maafa.
F : UHUSIANO KATI YA MGAWO WA BAJETI NA UHABA WA CHAKULA NCHINI

Mheshimiwa Spika, kwa nchi zilizo makini na mipango yake suala la mgawanyo wa rasilimali za nchi hasa zihusuzo chakula ni lazima ujikite kwenye maeneo ambayo yana athirika mara kwa mara na tatizo la njaa.  Utafiti ulioendeshwa na ‘Food Security Information Team (FSIT)’, uligundua kuwa jumla ya mikoa 10 ndiyo inayokumbwa na tatizo la uhaba wa chakula mara kwa mara. Mikoa hiyo ni : Arusha, Kilimanjaro, Lindi, Manyara, Mara, Mwanza, Mtwara, Shinyanga, Singida, and Tabora.

 Mheshimiwa Spika, utafiti uliofanywa kuona kama mikoa hiyo inapata kipaumbele cha kupata zaidi katika mgawo wa fedha za DADG  au la ? Matokeo ya utafiti huo yalionyesha kuwa, kwa mwaka wa fedha  2009, mikoa hiyo 10 ambayo inaidadi ya watu asilimia  46.2 (karibu 50%) ya watu wote hapa nchini (National Bureau of Statistics (NBS)[7] –Mikoa hiyo ilipatiwa asilimia  30.2% ya fedha zote za   bajeti ya DADP  kwa 2009/10 (jedwali chini linaonyesha).

Mheshimimiwa Spika, kwa ushahidi huo inaonyesha kuwa mipango ya Serikali mbali na kufanya tafiti haipangwi kutatua matatizo yanayojirudia rudia badala yake inaonyesha kuwa matatizo hayo ni neema kwa watendaji hao wapangaji. Kambi Rasmi ya Upinzani inauliza inakuwaje  mikoa yenye idadi karibu nusu ya watanzania wote na inayokabiliwa na uhaba wa chakula mara nyingi, na serikali inaelewa lakini haipewi kipaumbele katika kuhakikisha tatizo la ukosefu wa chakula linaisha ? Au kwa ufupi ni kuwa mgawanyo wa bajeti ya kilimo haiangalii maeneo yenye uhaba wa chakula, Watawala wamechoka kutawala !!!!!!!!!!!  hivyo walalahoi hawathaminiwi tena katika mipango yao.

Chanzo: Ofisi ya Waziri Mkuu,Serikali za mitaa na Tawala za mikoa

Mheshimiwa Spika, katika taarifa ya Serikali kwenye kamati ya kudumu ya fedha na uchumi mwezi Januari 2013, Serikali ilinasema inauza mahindi kwa wafanyabiashara binafsi toka katika hifadhi ya taifa ya chakula (labda kwa bei ya chini kuliko ile ya soko). Wafanyabiashara binafsi wanasaga na kuuza kwa wananchi.  Lakini wafanyabiashara hao hao hulangua wanunuzi wa mahindi au unga kwa kutengeneza vocha mbili na kuwasainisha wanunuzi bei tofauti.
 Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali iwaeleze watanzania  inadhibiti vipi bei ya unga au mahindi unaouzwa na wafanyabishara walionunua mahindi toka katika hifadhi ya chakula (kwa bei ya chini) ukilinganisha na bei ya soko ambayo ni wafanyabishara walionunua unga toka sehemu nyingine? Ni namna gani bei za soko zitaratibiwa kiasi kwamba wafanyabiashara  waliopewa vibali vya kununua mahindi toka hifadhi ya chakula  kuuza unga na mahindi kwa bei ya chini kuliko bei ilivyo sokoni ?
G: PEMBEJEO ZA KILIMO
Mheshimiwa Spika, kilimo ili kibebe dhana inayokusudiwa katika sera yake ya mwaka 1997 ya kuwa endelevu, chenye tija na cha kibiashara ni lazima kubadili zana zilizokuwa zinatumika hapo kale. Takwimu zinaonyesha kuwa : Maksai wanaotumika katika kilimo wamekuwa wanaongezeka kutoka 320,000 mwaka 1970 hadi kufikia 1,542, 000 mwaka 2010 ambapo majembe yanayokokotwa na maksai yameongezeka kutoka 140,000 hadi kufikia 620,000 katika kipindi hicho. Kwa mwaka 1960 kama nchi ilikuwa na Matrekta makubwa 2,580 yaliyotumika katika kilimo na mwaka 2010 yameongezeka hadi 7,825[8].  Aidha kwa mwaka 2010 idadi ya matrekta ya mkono ilikuwa 4,571[9]
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani kwa kuangalia takwimu hizo za zana za kilimo, inaonyesha wazi itachukua kipindi kirefu sana kukibadilisha kilimo kwani ongezeko la maksai na majembe ya kukokotwa na maksai hayaendani na ongezeko la matrekta licha ya uwepo wa mipango na mikakati mingi ya kuinua kilimo. Hizo zinaonyesha kuwa ni ngonjera za muda mrefu ambazo zinaendelea hadi sasa.
Mheshimiwa Spika, Matumizi ya mbegu bora, mbolea, dawa za mimea na dawa za kuulia wadudu yanakwamishwa na upatikanaji mdogo na bei za juu za pembejeo. Tatizo la umbali toka kijijini hadi maduka ya pembejeo nalo ni changamoto. Wananchi husafiri umbali wa takribani kilomita 25 hadi 56 katika wilaya ya Lindi Vijijini, na kati ya kilomita 25 hadi 70 katika wilaya za Mtwara Vijijini na Iringa Vijijini na kati ya kilomita 12 hadi 80 katika wilaya ya Hanang’  kuifuata huduma ya pembejeo.
Mheshimiwa Spika, kuhusu matumizi ya pembejeo za kilimo na udhibiti wa ubora wa pembejeo hasa mbegu, mbolea na viuatilifu. Kambi ya upinzani inapenda kujua serikali imechukua hatua gani kuhusu malalamiko ya wakulima wengi kuhusu mbegu wanazouziwa kutoota, mbolea kutokuwa na tija yeyote kwenye mazao na viuatilifu kushindwa kuua visumbufu vya mimea na mazao. Aidha, pamoja na serikali kuajiri maafisa ugani wengi, lakini bado wakulima hawapati huduma hiyo hasa kuhusu matumizi bora ya pembejeo za kilimo na kilimo biashara (farming as business). 
Mheshimiwa Spika, mgawo wa shilingi bilioni 75  kwa ajili ya vocha za pembejeo (mbolea), kutokana na hali halisi ilivyo, fedha hizi zinaweza kutumika kifisadi kama ambavyoimekuwa kwa miaka ya nyuma. Hivyo basi, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali fedha hizo kupelekwa Idara ya Umwagiliaji ili kuondoa adha ya ukame ambalo limekuwa kikwazo kikubwa cha uzalishaji. Kilimo cha kutegemea mvua kumeleta hasara na umasikini kwa wakulima hata wale wanaopatiwa pembejeo za ruzuku.


H : KILIMO CHA UMWAGILIAJI
Mheshimiwa Spika, katika fursa ya kujihusisha na kilimo cha umwagiliaji Tanzania ni ya pili katika bara la Afrika nyuma ya Nchi ya DRC kwa kuwa na hazina kubwa ya maji. Takwimu zilizopo zinaonyesha kuwa  kati ya eneo lote lifaalo kwa kilimo cha umwagiliaji la hekta millioni 29.4 ni asilimia 1% inayotumika.

Mheshimiwa Spika, Kwa sasa nchi yetu ina maeneo makubwa ya ardhi yenye rutuba  na mito mikubwa  pamoja na maziwa makubwa kama vile Viktoria, Nyasa, Tanganyika na Rukwa bila ya kusahau mabonde makubwa ya mito, hii asilimia moja sio kwamba ni ukosefu wa maji ya umwagiliaji ila ni kukosekana kwa utashi wa kisiasa na jinsi tunavyopanga vipaumbele vyetu katika matumizi ya raslimali fedha.  

Mheshimiwa Spika, Fursa katika uwekezaji katika kilimo cha umwagiliaji ni kubwa mno hapa nchini, lakini kuna tatizo kubwa la raslimali watu yenye ujuzi katika nyanja ya umwagiliaji kwenye ngazi ya Halmashauri kwa ajili utekelezaji kwenye uwekezaji huo. Nyaraka zinaonyesha kuwa kikundi kazi kilichoundwa mwaka 2010 August na ‘the Basket Fund Steering Committee’ ili kuchunguza chanzo cha fedha nyingi za miradi ya umwagiliaji kupelekwa mwaka wa fedha unaofuata kiligundua kuwa, kati ya Halmashauri 132, kuna mainjinia 32 tu, na mafundi mchundo wa umwagiliaji (irrigation technicians) 107. Katika ngazi ya mkoa, kuna mainjinia wa umwagiliaji 17 tu. Baya zaidi ni kwamba hata wale mafundi mchundo waliopo ni kwamba hawana vitendea kazi. La mwisho lakini la umuhimu ni ukiritimba uliokithiri katika Halmashauri zetu ambao ni kikwazo kikubwa katika uwekezaji wa miradi kwenye shughuli za kilimo[10].
I : VYAMA VYA USHIRIKA NA BODI ZA MAZAO
Mheshimiwa Spika, Shabaha kuu ya Vyama vya Ushirika vilipoanzishwa, ilikuwa kuuza mazao ya wanachama kwa bei nzuri na wakati huohuo kuondoa unyonyaji wa wafanyabiashara ambao walikuwa wakinunua mazao hayo kwa bei ya chini na kuuza kwa bei ya juu na pia kutayarisha mazao kusudi yawe katika hali bora inayotakiwa na wanunuzi. Aidha, kukusanya mazao kutoka kwa wakulima, na kufanya mipango ya kusafirisha mazao hayo toka kwa wakulima hadi “mikononi” mwa Halmashauri za Mazao au mpaka katika masoko ya dunia[11]. Pia Vyama vya Ushirika vikiwemo vya Akiba na Mikopo (SACCOS) na vile vya kilimo na masoko (AMCOS) vimedhihirisha kuwa nguzo muhimu katika kuwapatia maisha bora Watanzania.
Mheshimiwa Spika, Ushirika unaonyeshwa kuwa ni njia mojawapo ya kuboresha maisha ya wananchi wa Tanzania walio wanyonge kiuchumi[12].  Hoja ni kuwa kweli maisha bora yaliyokusudiwa wakati wa uanzishwaji wa vyama hivyo yanaweza kupatikana ? wakati bei kwa mkulima anaambiwa ni nguvu za ushindani wa soko?
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kutoa tathmini ya utendaji mzima wa AMCOS na imesaidia vipi hizo AMCOS kupata mikopo kutoka taasisi za fedha kwa maendeleo ya wakulima ?
J : BODI YA NAFAKA NA MAZAO MCHANGANYIKO
Mheshimiwa Spika, Nafaka ni mazao makuu ya chakula ambayo hutumiwa na watanzania wote waishio mijini na vijijini. Nafaka zinaweza kuhifadhiwa kwa muda mrefu kuliko mazao mengine ya chakula na mara nyingi nafaka huzalishwa mara moja au mbili kwa mwaka. Kwa hiyo ili iweze kupatikana na kutumika kwa wakati wote ni lazima kuhifadhi.
Mheshimiwa Spika, aidha, ili kuweza kuwa na bidhaa zenye thamani ni lazima kusindika. Jitihada zimekuwa zikifanywa na serikali kuongeza tija na uzalishaji wa mazao hayo. Uzalishaji wa mazao ya nafaka unakadiriwa kufikia wastani wa tani 3,897,500 kwa mwaka. Pamoja na ongezeko la uzalishaji, teknolojia zinazotumika katika uvunaji, utayarishaji na hifadhi ni duni na husababisha upotevu mkubwa wa mazao hayo. Wastani wa tani 1,559,000 za mazao ya nafaka hupotea kila mwaka[13].
Mheshimiwa Spika, sheria iliyotungwa na bunge kwa ajili ya kuanzisha chombo hiki ilikuwa ni kwa ajili ya kuwapatia wakulima huduma muhimu ikiwemo kuwapatia bei nzuri itakayokidhi gharama za uzalishaji mazao yao ambayo hayana chombo maalum ya kuyasimamia.
Mheshimiwa Spika, kwa masikitiko makubwa ni kwamba chombo hiki kimeshindwa kabisa kuwasaidia wakulima kuwahakikishia ununuzi wa mazao yao kwa bei inayoweza kurejesha gharama za uzalishaji, mbali na bodi yenyewe kuingia katika mchakato wa ununuzi wa mazao hayo.
Mheshimiwa Spika, kwa kadri Serikali inavyochelewa kutimiza wajibu wake kwa mujibu wa sheria zilizopo, mkulima anazidi kuwa fukara na kilimo kinazidi kukosa tija kwa mkulima na pale pale mfanyabiashara anazidi kuneemeka na kilimo hicho, hivyo mnyororo wa biashara isiyoakisi hali halisi baina ya pande mbili husika inazidi kushamiri, jambo ambalo ni hatari na linapingana na sera yetu ya kilimo.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzania inasema kuwa, muda umefika sasa kwa mkulima na kilimo kuonekana kuwa sio chaguo la mwisho katika orodha ya kazi za ajira kwa vijana wa nchi hiii. Jambo hili linaweza kufikiwa sio kwa mikakati iliyo kwenye makaratasi na kufungiwa makabatini bali kwa kuangalia gharama halisi ya utoaji ruzuku na gharama halisi kama mkulima akipatiwa bei dira inayoweza kufuta gharama za uzalishaji. Aidha, ruzuku ikaingizwa kwenye uanzishwaji wa viwanda vya kuongeza thamani za mazao.

K: MUHOGO

Mheshimiwa Spika, zao la muhogo ambalo linalimwa karibu na wakulima wote hapa nchini, linachangia takriban asilimia 15 kwenye kapu la uzalishaji wa chakula  hapa nchini. Ni zao la pili nyuma ya mahindi abalo ni zao kuu la chakula hapa nchini. Mikoa inayolima muhogo ni Mtwara, Pwani, Mwanza, Kigoma, Tanga, Morogoro, Mara, Ruvuma, Shinyanga na Lindi. Ila kiwango cha kilimo cha zao hilo ndicho kinachotofautiana kati ya mkoa na mkoa[14]. Kitendo kilichofanywa na Serikali kwa wakulima wa zao la muhogo wa Mtwara Mikindani la kuwalipa shilingi 130 kwa shina, ni kitendo cha kudhalilisha mkulima na kilimo kwa ujumla wake. Wakulima wa Mtwara Mikindani kwa nyakati tofauti walilamikia kiwango hicho.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inataka Serikali itoe maelezo, kwa njia hii ya uthamanishaji wa shina la muhogo kwa shilingi 130, je kilimo kinaweza tumika kama nyenzo ya kuondoa umasikini ? Au hii ni kiini macho kwa wakulima?
Mheshimiwa Spika, kutokana na takwimu hizo za uzalishaji wa muhogo hapa nchini na umuhimu za zao hilo katika uchangiaji kwenye kapu la chakula hapa nchini, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali iwaeleze wananchi ni mkakati gani uliopo wa kuhakikisha kuwa kilimo cha mihogo hapa nchini kinaleta tija kwa wananchi na Taifa katika kuondoa umasikini na kukuza uchumi?

L: NGANO

Mheshimiwa Spika, Uzalishaji wa ngano kwa Tanzania sio kipaumbele kwa maendeleo ya sekta ya kilimo. Hii inatokana na ukweli kwamba zao la ngano halina sera wala halimo kwenye vipaumbele vya kuliendeleza (masoko na viwanda vya kuongeza thamani).
Mheshimiwa Spika, Kwa Tanzania matumizi ya ngano katika orodha ya vyakula ni ya nne nyuma ya mahindi, muhogo na mchele. Hii inaonyesha ni jinsi gani zao la ngano lilivyo na umuhimu kwa nchi yetu. Matumizi ya ngano kwa maeneo ya mijini ni takribani asilimia (83%) na vijijini ni takriban asilimia (17%) (Kilima, 2006).
Mheshimiwa Spika, maendeleo ya zao hili yameachwa mikononi mwa sekta binafsi iliyonunua mashamba makubwa na inamiliki viwanda vya usagishaji wa zao hilo. Jambo hili linapelekea wakulima wadogo ambao wametawanyika sana kumezwa na wafanyabiashara wakubwa. Hata hivyo Tanzania inauwezo wa kuzalisha zaidi ya tani 164,000 kwa mwaka kama Serikali itaweka sera madhubuti ya kuhakikisha hata wakulima wadogo wanauza ngano yao kwa bei inayoweza kuwa na tija kwao, kama ilivyokuwa hapo awali wakati wakiuza kwa NMC.
Mheshimiwa Spika, kwa sasa ngano ya kawaida iliyopetwa kilo moja inauzwa kati ya shilingi 800/- hadi 900/- Wakati bidhaa zitokanazo na ngano (Mkate, chapati, Keki, maandazi n.k) bei zake zimekuwa zikipanda kila kukicha. Mkate wa gramu 500 unauzwa kati ya shilingi 1200/- hadi 1700/-. Na kwa upande wa chapati zinauzwa kati ya shilingi 200/- hadi 500/-.
Mheshimiwa Spika, bidhaa hizi za ngano ni muhimu sana kwa jamii ya watanzania waishio mijini, swali la msingi ni namna gani Serikali inahakikisha wakulima wadogo wa zao hilo na wao wananufaika na umuhimu wa zao hilo kwa jamii ziishizo mijini?
Mheshimiwa Spika,  bei ya ngano kwa miaka miwili ya nyuma ilipanda kwa asilimia 65% kutokana na kutokuwepo kwa uhakika wa uzalishaji toka kwa nchi za Bulgaria, Georgia, Romani, Russia, Turkey na Ukraine (Black Sea Countries)[15]. Uagizaji wa ngano toka nje umeendelea kupanda na sasa inakadiriwa kuwa ni tani 1milioni wakati uzalishaji wa ngano kwa mwaka ni tani 100,000. Tofauti na uzalishaji na mahitaji ni kubwa sana na hii inaonyesha ni jinsi gani fursa kwa wakulima wetu ilivyo kubwa sana.
Mheshimiwa Spika, mbegu ya ngano kilo moja inauzwa kwa shilingi 5,000/- na gunia la kilo 100 linauzwa kwa shilingi 500,000/-. Na kwa kawaida kilo 100 za mbegu zinatosha kupanda hekta 2 tu. Hoja ni kwamba kwa bei hiyo ya mbegu ni kweli mkulima mdogo ili aweze kunufaika na kilimo cha ngano alime hekta ngapi? Na bodi ya nafaka na mazao mchanganyiko inafanya nini kwenye zao hili muhimu kusudi liongeze tija?

M: ZAO LA KOROSHO
Mheshimiwa Spika, zao hili kwa muda mrefu limeachwa na wakulima wake wameachwa kana kwamba wao hawazalishi zao lenye faida kubwa kwa taifa hili na hasa katika kulipatia taifa letu fedha nyingi za kigeni ambazo badala ya kuelekezwa kwenye kuimarisha viwanda vya kubangua korosho vimeachwa vife na wakulima waendelee kuuza korosho ghafi nje ya nchi na hivyo
hawapati faida kama ilivyotakiwa kuwa, mifano halisi ni kama ifuatavyo hapa chini ya viwanda vilivyouwawa ;
Mheshimiwa Spika, mojawapo ya malalamiko au changamoto zinazotolewa na bodi ya korosho ni kuwa nanukuu, “ukosefu wa bei ya uhakika ya kuuzia korosho ghafi. Utegemezi wa soko la nje la korosho ghafi. Zaidi ya asilimia 95 ya korosho ghafi tunayozalisha nchini inategemewa kununuliwa na nchi za nje. Zaidi ya asilimia 90 ya korosho ghafi hununuliwa na wamiliki wa makampuni ya ubanguaji kutoka India, hivyo soko la korosho ghafi kuu kwa ujumla lina wanunuzi kutoka nchi moja wakati wauzaji ni wengi. Kwa sababu hiyo ni wazi kwamba wanunuzi hao wana nafasi kubwa ya kukaa pamoja na kupanga bei. Kwa ujumla hakuna ushindani wa bei”.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa nukuu hiyo ya Bodi ya Korosho inaonyesha kuwa India imehodhi soko la korosho na hivyo wanapanga bei wao.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa tafiti nilizozifanya zinaonyesha kuwa Vietnam nayo ni nchi inayonunua na kuuza Korosho ndani na nje kwa msimu wa mwaka 2011 ilinunua korosho ghafi takriban tani 450,000 na hizo zilitoka Africa ya Mashariki, Afrika ya Magharibi na Indonesia Australia, Uarabuni, Russia, Uchina na Nchi za Scandnavia[16].
Mheshimiwa Spika, kurudishwa kwa Viwanda vya Korosho vilivyouzwa na vikashindwa kufanyakazi iliyotarajiwa ndio ufumbuzi wa kudumu kwa Serikali kuingia kwenye masoko ya nchi wanunuzi nilizozitaja hapo juu.
Mheshimiwa Spika, mbali ya matatizo hayo ya soko naomba kunukuu kauli ya Mhe Naibu Waziri kwenye taarifa rasmi za Bunge ya tarehe  4 February 2013,wakati akijibu swali la Nyongeza la Mhe Mwijage, “Mheshimiwa Naibu Spika, lakini bado Korosho kwa kiasi kikubwa inabanguliwa India. Sasa tatizo tulilokuwa nalo ni kwamba Korosho ya Tanzania ndiyo Korosho premium duniani, lakini hatujaifanyia branding kwa sababu kwenye hali ya kukandamiza hii hali ya Korosho kuna maslahi kwa watu wengi ambayo inawakandamiza wakulima”.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kulieleza Bunge hili maslahi ya watu wengi ambayo yanawakandamiza wakulima na watu hao wengi tunaitaka Serikali iwataje watu hao ili Bunge kwa liweze kuishauri Serikali vizuri jinsi ya kushughulika na kundi hilo linalokandamzia maslahi ya wakulima.
Mheshimiwa Spika, ubinafsishaji wa mashamba, viwanda na mashirika ya umma hapa nchini hasa vilivyokuwa kwenye sekta ya kilimo vimekuwa na changamoto mbalimbali ikiwemo kuzalisha chini ya kiwango na kutoendelezea kabisa. Kambi ya upinzani inashauri kuwa mashamba yote hasa yale ya NAFCO BASOTU, KAPUNGA na ya CHAI-TUKUYU yaendeshwe chini ya ushirika kama ilivyo kwa maeneo mengine ya Mbarali na Mvomero wananchi kuondokana na umaskini na kupunguza idadi kubwa ya Watanzania wasiokuwa ajira
Mheshimiwa Spika, naomba ninukuu taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma KWA MWAKA WA FEDHA UNAOISHIA JUNI 30, 2010 kama ilivyo wasilishwa hapa Bungeni tarehe 17 April 2012  kuhusu tathimini ya viwanda vya Korosho.
i.                     Kiwanda cha Korosho cha Likombe.
Mheshimiwa Spika, Kiwanda hiki kipo mjini Mtwara na kilijengwa mwaka 1980 kwa kutumia teknolojia ya Kijapani. Kwa Mwaka 2004,kiwanda kiliuzwa kwa kampuni ya Micronix System Limited kwa bei ya shilingi milioni 100 ambayo alikwishalipa.
Mheshimiwa Spika, Kiwanda hakijawahi kuzalisha tangu kilipobinafsishwa mwaka 2004. Mwekezaji hajafanya ukarabati wowote wa mashine zilizokuwepo kiwandani ila amenunua mashine nne mpya za  upakiaji ambazo ni mixing, packing, drying na humidifier machines. Aidha ilibainika kuwa Mwekezaji amekodisha sehemu ya ghala kwa kampuni binafsi ambayo inaendesha zoezi la kutunza korosho kwa mtindo wa stakabadhi gharani na pia amekodisha sehemu ya Kiwanda kwa Kampuni ya Olum ambayo inafanya shughuli za Ubanguaji wa Korosho kwa kiasi kidogo.
ii.                Kiwanda cha Korosho cha Mtama
Mheshimiwa Spika, Kiwanda kipo Lindi vijijini na kilijengwa mwaka 1978 kikiwa na uwezo wa kubangua tani 5,000 za korosho kwa mwaka. Kiwanda kiliuzwa kwa kampuni ya Lindi Farmers Company Limited mwaka 2005 kwa bei ya shilingi milioni 30.0 ambayo amekwishalipa. Hadi kinabinafsishwa kiwanda kilikuwa katika hali nzuri na kwamba yalihitajika matengenezo madogo madogo.
iii.              Kiwanda cha Korosho cha Lindi
Mheshimiwa Spika, Kiwanda kipo mjini Lindi na kilijengwa kuanzia mwaka 1977 kwa kutumia teknolojia ya Kitaliano na kilikuwa na uwezo wa kubangua tani 10,000 za korosho kwa mwaka. Kiwanda kilifanyiwa majaribio mwaka 1978 na kuendelea kufanya kazi hadi mwaka 1996, kiliposimama. Mwaka 2004 kiwanda kiliuzwa kwa kampuni ya Bucco Investment Holdings Limited kwa bei ya shilingi milioni 50.0.
Mheshimiwa Spika, Mwekezaji alitakiwa kuwekeza kiasi cha dola za kimarekani 600,000 kwa ajili ya ukarabati wa kiwanda. Mwekezaji amefanya ukarabati kwa gharama ya shilingi milioni 250. Maeneo yaliyofanyiwa ukarabati ni boiler, mashine za kukatia korosho na grading. Kiwanda kimesima kwa kukosa mtaji wa uendeshaji. Ni wazi kuwa Mwekezaji amevunja Mkataba wa Mauzo kwa kushindwa kufufua kiwanda.
iv.               Kiwanda cha Korosho Newala II
Mheshimiwa Spika, Kiwanda kipo wilaya ya Newala mkoa wa Mtwara. Ujenzi wake ulianza mwaka 1977 na kukamilika mwaka 1980 kwa kutumia tekinolojia ya kijapani na kilikuwa na uwezo wa kubangua tani 10,000 za korosho kwa mwaka. Kiwanda kilifanya kazi kwa muda wa mwaka mmoja na kisha kusimama kutokana na uhaba wa korosho ghafi.
Mheshimiwa Spika, Mwaka 2004 kiwanda kiliuzwa kwa kampuni ya Micronix Sytems Ltd. kwa bei ya shilingi milioni 75.0. Mwekezaji alikwishalipa fedha zote na kukabidhiwa kiwanda. Hadi wakati kiwanda hiki kinabinafsishwa, sehemu kubwa ya kiwanda ilikuwa katika hali nzuri ukiacha matengenezo ya sehemu kadhaa kutokana na kukaa kwa muda mrefu bila ya kufanya kazi.
Mheshimiwa Spika, Kulingana na Mpango wa uwekezaji, mnunuzi alitakiwa kuwekeza kiasi cha Dola za Marekani milioni 3.64 katika ukarabati wa kiwanda kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka 2006 mpaka 2010 kama ilivyoainishwa kwenye Mkataba wa Mauzo. Mwekezaji alieleza kuwa amewekeza kiasi cha shilingi milioni 150 katika ukarabati wa kiwanda kwa kununua mashine za kutumia teknolojia ya mkono. Ukarabati huo ulifanyika mwaka 2009. Mashine za zamani zimekusanywa na kurundikwa sehemu moja kwa kile mwekezaji anachodai kuwa teknolojia yake imepitwa na wakati.


v.                 Kiwanda cha Korosho Newalla I
Mheshimiwa Spika,Kiwanda kipo mjini Newala, mkoa wa Mtwara,kilijengwa mwaka 1976 na kufanyiwa majaribio mwaka 1981 na hakikufanya kazi baada ya majaribio ya awali. Kiwanda hiki kilijengwa kwa mitambo ya teknolojia ya Kitaliano yenye uwezo wa kubangua tani 10,000 kwa mwaka. Aidha kwa maelezo ya Uongozi wa Shirika Hodhi la yaliokuwa Mashirika ya Umma (CHC), Mwaka 2004 kiwanda kiliuzwa kwa kampuni ya Agrofocus Limited kwa bei ya shilingi milioni 75.0. Mwekezaji alikwisha kamilisha malipo. Hadi wakati kinabinafsishwa, mitambo na mashine ya kiwanda vilikuwa katika hali nzuri ukiacha sehemu chache za umeme na mikanda ya kusafirishia korosho. Aidha, majengo ya kiwanda yalikuwa katika hali  nzuri isipokuwa sehemu kadhaa za paa ambazo zilihitaji ukarabati ili kuzirejesha katika hali ya kawaida.
Mwekezaji amewekeza kiasi cha shilingi milioni 718.0 katika ukarabati wa kiwanda. Mashine zote zimekarabatiwa na zinafanya kazi. Kiwanda kipo katika hali nzuri, mazingira ni safi na majengo yote yamepakwa rangi. Mashine pia zipo katika hali nzuri.
Mheshimiwa Spika, baada ya Tathmini, Kamati haijaridhishwa kabisa na zoezi la ubinafshishaji wa Mashirika ya Umma katika Sekta Ndogo ya  Viwanda vya Korosho (Mamlaka ya Korosho). Viwanda vyote vya kubangua korosho vilivyojengwa kwa Mkopo wa Benki ya Dunia vyenye thamani ya Dola milioni 284 havifanyi kazi, wawekezaji waliovinunua wamevigeuza kuwa maghala ya kuhifadhia korosho na Nchi inaendelea kupata hasara kubwa kwa kusafirisha korosho ghafi.”
Mheshimiwa Spika, Baada ya Kamati ya Hesabu za Mashirika ya Umma kutoa tathmini hiyo kama nilivyo inukuu, ilitoa mapendekezo yake ambayo Bunge hili liliridhia na baadae kuwa ni azimio rasmi la Bunge, naomba kunukuu azimio hilo la Bunge kama lilivyo kwenye taarifa ya kamati ya POAC ya 17 April 2012,
  “Mheshimiwa Spika, kwa kuwa katika tathmini yake ya viwanda vilivyobinafsishwa vya ubanguaji Korosho, imebainika kuwa baadhi ya wawekezaji wamekiuka kwa makusudi mikataba ya uendeshaji wa Viwanda hivyo, na kwa kuwa kwa kufanya hivyo wamesababisha Taifa kuendelea kusafirisha korosho ghafi kwenda Nje ya Nchi na hivyo kuondoa fursa ya wakulima kupata faida ya kutosha na kupunguza ajira Nchini, kwa hiyo Kamati inapendekeza kuwa Serikali ichukue uamuzi wa kuvirejesha viwanda vyote vya kubangua Korosho vilivyobinafsishwa na wawekezaji wake kushindwa kuviendeleza ili kuona namna bora ya kuwekeza kwenye ubanguaji wa korosho ikiwa na pamoja na Serikali kusisitiza umuhimu wa kuuza Korosho iliyobanguliwa Nje ya Nchi kwa kuwajengea uwezo wakulima wa kubangua Korosho”.

Mheshimiwa Spika, Kambi ya upinzani inataka kupata majibu utekelezaji wa azimio hili umefikia wapi mpaka sasa kwani kutokutekelezwa kwa azimio hili ni kuendelea kuwaumiza wananchi wetu ambao ni wakulima na ambao hawapati pembejeo kwa wakati, dawa na sasa hata bei nzuri hawapati .

N : KAHAWA
Mheshimiwa Spika, Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB) ni Taasisi ya Umma iliyoundwa kwa sheria ya bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya bodi za mazao namba 23 ya mwaka 2001, pamoja na majukumu mengine lakini ya msingi yakiwa ni:
• Kusimamia sekta ya kahawa Tanzania
• Kuishauri serikali mambo ya msingi juu ya mikakati ya kuendeleza
kilimo na biashara ya kahawa
Mheshimiwa Spika, dira ya bodi inasema kuwa “Kuwezesha mazingira muafaka kwa maendeleo endelevu ya sekta ya kahawa nchini Tanzania”. Kwa kadri iwezekekanavyo  maendeleo endelevu katika sekta ya kahawa hayawezi kufikiwa ikiwa bei anayopata mkulima wa Kahawa haiwezi kuzidi gharama za uzalishaji. Hii ni kudanganyana na kumfanya mkulima aendelee kuwa tegemezi na maendeleo endelevu kwa sekta hayawezi kupatikana.
Mheshimiwa Spika, pamoja na uwepo wa bodi hii zao hili la kahawa limeendelea kudidimia siku hadi siku kutokana na wakulima kukosa pembejeo kama madawa, mbegu bora na wataalamu wa kutosha .Aidha viwanda vya kubangulia kahawa vilivyojengwa wakati wa utawala wa Mwl.Nyerere leo hii viko hoi bin taabani.
Kambi ya Upinzani, inataka kupata majibu kuna mkakati gani na mpango gani endelevu wa kulifufua zao hili pamoja na viwanda vya kubangua na kusindika kahawa ili kuliwezesha taifa kupata faida kutokana na kilimo cha zao hili.
O : PAMBA
Mheshimiwa Spika, Pamba ni zao kuu la biashara na ni la pili kwa kuingiza fedha za kigeni baada ya kahawa. Pamba inachangia asilimia 24 ya mauzo yote ya bidhaa za kilimo nje ya nchi na inachangia asilimia 4 ya mauzo yote nje ya nchi. Takribani hekta  400, 000 zinatumika kwa ajili ya kilimo cha pamba kwenye wilaya zaidi ya 40 za mikoa  13 ya Tanzania Bara.
Mheshimiwa Spika, Takwimu zinaonyesha kuwa uzalishaji wa zao la pamba nchini, umeongezeka kutoka kilo milioni 168 msimu wa mwaka 2010/11 hadi kufikia kilo million 224 katika msimu wa mwaka 2011/12
Mheshimiwa Spika, wakati Akiongea na wawekezaji kutoka Algeria ambao pia ni wafanyabiashara mashuhuri duniani,  Waziri wa Kilimo Chakula na Ushirika  wakati huo, Mh. Prof. Jumanne Maghembe  alisema msimu huu uzalishaji wa Pamba umeongezeka kwa kiasi kikubwa ambacho hakijawahi kutokea  kwa kipindi cha miaka 50 iliyopita”
Kauli hiyo ya waziri iliongezewa nguvu na Mkurugenzi wa Bodi ya Pamba nchini, kwa kusema kuwa “ongezeko hilo limechangiwa na serikali kwa kutoa ruzuku za pembejeo. Aidha alisema pia kuyumba kwa bei ya pamba   ambayo ni kati ya sh 1,100 mpaka sh 800 kwa kilo kunachangia wakulima kutoongeza bidii ya kilimo cha zao hilo”.
Mheshimiwa Spika, ni ukweli kuwa Tanzania ina uwezo wa kuzalisha kiasi kikubwa cha pamba kuliko nchi nyingine zilizopo Kusini na Mashariki mwa Bara la Afrika. Hivi sasa asilimia 70 ya pamba, inauzwa nje huku viwanda vya ndani vikitumia asilimia 30. Na matumizi haya ya asilimia 30 siyo kwa ajili ya kutengeneza nguo bali ni kwa asjili ya kusokota nyuzi kwa ajili ya kupeleka nje ya nchi. Huu ni uzembe mkubwa au hujuma kwa watanzania jambo linalopelekea kuendelea kuagiza mitumba toka nje na kuwa nchi ya wachuuzi.
Mheshimiwa Spika, pamoja na wakulima wetu kujitahidi kuzalisha kwa wingi kiasi hicho ambacho kimevunja rekodi ya uzalishaji kwa miaka 50 ila bado bei ya Pamba imekuwa ni ndogo sana ukilinganisha na uhalisia wa gharama halisi za uzalishaji kama vile mbegu, madawa na gharama nyingine za uzalishaji wa zao hilo.

PAMBA NA KILIMO CHA MKATABA
Mheshimiwa Spika, kilimo hiki cha mkataba kimekuwa ni sumu kubwa sana kwa wakulima wa Pamba na hivyo kupelekea wakulima kuona kuwa ni afadhali waachane na kilimo wajihusishe na shughuli zingine. Ili kilimo hiki kiwe na manufaa kwa mkulima inabidi uzalishaji kwa hekari uongezeke. Na katika kufikia hilo Ginneries ndizo ziwe na jukumu la kuhakikisha kuwa matatizo ya mkulima yanatatuliwa, lakini mkataba huo wa mkulima na hizo Ginneries umwache huru kuuza pamba yake kwa mnunuzi yeyote atakayetoa bei nzuri, ila imlazimu mkulima kulipa gharama zote zilizotumiwa na Ginneries katika kumfanya azalishe.
Mheshimiwa Spika, katika kuwekeana mikataba inabidi bei dira iwekwe  katika mkataba na pia ielezwe kuwa uwepo uthamanishaji halisi ya nguvu za mkulima katika mchakato mzima wa uzalishaji. Katika hali hiyo mkataba uwe sawa kwa wakulima walioko kwenye maeneo/ wilaya moja.
Mheshimiwa Spika, wote ni mashuhuda katika mdororo wa uchumi hasara iliyotokea, iliangukia kwa mkulima na mfanyabiashara alipata fidia toka Serikalini. Hivyo basi Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali pale hasara inapotokea mkulima awe wa kwanza kupatiwa fidia badala ya mfanyabiashara.
Mheshimiwa Spika, Hoja sio kuendelea kuongeza ruzuku za PEMBEJEO au bei za MALIGHAFI Ukifanya marginal analysis (price - unit cost) ya mazao uliyoorodhesha, utakuta kwamba mkulima anapata kama 12% ya total margin katika value chain wakati mwenye kiwanda anapata zaidi ya 50%. kwa mazao ambayo hayaendi viwandani, mkulima hupata kama 30% na mfanyabiashara hupata zaidi ya 60%

Mheshimiwa Spika, Mfano: Leo mkulima wa kule Mwanza anauza 1kg ya pamba kwa Tshs 600/=. Kilo hii inatoa mashati manne na  kila shati moja la pamba halisi likiuzwa kwa dolla 50 ni sawa na Tshs 80,000/=  Hivyo kwa kilo moja ni sawa na shilingi 320,000/-. Mwenye kiwanda (mzungu) anatumia Tshs 10,000/= tu kwa kilo kama gharama za ununuzi, usafirishaji (kupeleka pamba ulaya na kurudisha shati Mwanza) na uchakataji kiwandani. Faida yake ni Tshs 310,000/= kwa kilo moja. Hata kama angechukua Tshs 10,000/= zingine akatupatia "msaada" wa kutujengea barabara kutoka Dodoma hadi Mwanza ili akunyonye vizuri zaidi kwa kupunguza gharama za usafirishaji, bado ana faida ya Tshs 300,000/[17]=
Mheshimiwa Spika, kwa uchambuzi huo, tunaitaka Serikali kwa kushirikiana na wadau wa Pamba kujenga kiwanda cha Pamba katika mojawapo ya mikoa inayolima Pamba ambacho kitakuwa na jukumu la kuongeza thamani ya Pamba yetu.
Kambi ya Upinzani, inataka kupata majibu ya kina kuwa serikali ina mpango gani wa kuinua wakulima wa zao hili muhimu hapa nchini na hasa katika kuwapatia bei nzuri ya Pamba inayoendana na gharama halisi za uzalishaji wa kilo moja ambayo sasa imekuwa kubwa sana, wakati inatafakari uanzishwaji wa kiwanda cha Pamba.

P:  MIWA
Mheshimiwa Spika, katika uwekezaji unaotakiwa kufanyika katika mpango wa SAGCOT ni katika sekta ya sukari au ulimaji wa miwa. Kilimo cha miwa kimetawaliwa na kuhodhiwa kwa kiasi kikubwa na viwanda vinavyozalisha sukari kwani viwanda hivyo ndivyo vinavyopanga bei na muda wa kununua miwa toka kwa wakulima wanaozunguka viwanda hivyo. Katika mchakato huo wa kikiritimba anayeumia ni mkulima. Hoja ni kwa vipi tunamnasua mkulima katika mtego huo wa wenye viwanda? Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali itoe ufumbuzi wa suala hilo.
Mheshimiwa Spika, kanuni zinazowataka wakulima wanaozunguka kiwanda cha sukari waliondani ya kilometa 40 kutoka kilipo kiwanda cha sukari wanalazimishwa kuuza miwa yao kwenye kiwanda, japokuwa kanuni hiyo walidhani wanamsaidia mkulima kusafirisha miwa yake kufika kiwandani, lakini ukweli ni kwamba ni ujanja wa kuvilinda viwanda na ushindani unaoweza kujitokeza.
Mheshimiwa Spika, kanuni hii inazidisha ukiritimba kwa viwanda na kuwanyika haki ya msingi kwa wakulima ambao kwa kutumia ushirika wao wanauwezo wa kuanzisha kiwanda kikubwa au kidogo cha kutengeneza sukari.  Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kuangalia upya kanuni hiyo ili iendane na mazingira yaliyopo sasa. Aidha, tunaitaka Serikali kupitia SIDO kuanzisha viwanda vidogo ambavyo vitakuwa na ubia na wazalishaji wadogo wadogo (Cane outgrowers) katika maeneo mbalimbali yazalishayo miwa hapa nchini. Hii itaondoa tatizo kubwa la sukari linaloikabili nchi yetu na pia ni njia mojawapo ya kuondoa umasikini wa kipato kwa wakulima na kukuza uchumi wa nchi yetu.
Q: MAPITIO YA BAJETI YA KILIMO

Mheshimiwa Spika, Licha ya mabadiliko yaliyotokea katika mfumo wa uchumi katika miaka ya karibuni ambapo sekta za madini, utalii na huduma zimekua kwa kasi Sekta ya Kilimo inatoa mchango mkubwa katika kuwapatia ajira Watanzania zaidi ya asilimia 70 na inachangia wastani wa asilimia 95 ya chakula kinachohitajika nchini.  Katika kipindi hicho, Sekta ya Kilimo ilikua kwa wastani wa asilimia 4 na ilichangia asilimia 26 ya Pato la Taifa.

Mheshimiwa Spika, toka mwaka 2001/02 bujeti ya kilimo imekuwa ikiongezeka taratibu mwaka huo mgawo ulikuwa shilingi bilioni 52.1 , ambayo ilikuwa sawa na asilimia 3.0 ya bajeti ya mwaka 2001/02, toka hapo bajeti imekuwa mara dufu hadi kufikia asilimia 7.8 ya bajeti kwa mwaka  2010/11, Lakini kwa mwaka 2011/2012 ilishuka na kuwa asilimia  6.9.
Mwaka
Jumla ya Bajeti ya Kilimo
Bajeti ya Serikali
% ongezeko/punguzo la bajeti ya kilimo
Bajeti ya Kilimo kama % ya Bajeti ya Serikali
% ya badiliko la mgawo wa bajeti
2001/02
52.1
1764.7

3.0

2002/03
84.5
2219.2
62.2
3.8
0.8
2003/04
148.6
2607.2
75.9
5.7
1.9
2004/05
157.7
3347.5
6.1
4.7
-1.0
2005/06
233.3
4035.1
48.0
5.8
1.1
2006/07
276.6
4788.5
18.5
5.8
0.0
2007/08
372.4
6000.0
34.6
6.2
0.4
2008/09
440.1
7216.1
18.2
6.1
-0.1
2009/10
666.9
9500.0
34.0
7.0
0.9
2010/11
903.8
11610.0
26.2
7.8
0.8
2011/12
926.0
13500.0
2.7
6.9
-0.9
Chanzo:Idara ya takwimu ya wizara ya kilimo,chakula na ushirika
Mheshimiwa Spika,Takwimu zinaonyesha kuwa kwa kipindi hicho cha 2001/02 -2012/13 kumekuwa na uhusiano usiorodhisha kati ya bajeti ya maendeleo na bajeti ya matumizi ya kawaida. Bajeti ya matumizi ya kawaida imekuwa ikiongezeka wakati ile ya maendeleo imekuwa ikishuka, kwa mfano kwa mwaka 2001/02 bajeti ya matumizi ya kawaida ilikuwa asilimia 39.5 ya bajeti nzima ya wizara na mwaka 2008/09 ilipanda hadi kufikia asilimia 82.4 na mwaka 2011/12 ilipungua na kuwa asilimia 59.0.Wakati bajeti ya maendeleo mwaka 2001/02 ilikuwa asilimia 60.5 na mwaka 2011/12 ilishuka hadi kufikia asilimia41.0.
 Chanzo: Vitabu vya bajeti na hotuba za Wizara

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani, kwa tafakuri ya takwimu hizo inaona ni wazi kuwa Serikali haina  nia ya dhati ya kuwekeza katika kilimo kwani hata bajeti inayokwenda kwenye wizara sehemu kubwa ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida tu.
Mheshimiwa Spika, mbali na kupanda na kushuka kwa bajeti inayotengwa kwa kilimo hapa nchini bado kuna tatizo la utoaji wa fedha pungufu kulinganisha na zile zinazopitishwa na Bunge.
Jedwali lifuatalo linaonyesha Fedha zilizopitishwa na fedha zilizotolewa
Mwaka
Fedha zilizopitishwa
(TSh. Billion)
Fedha zilizotolewa
(TSh. Billion)
Upungufu
Asilimia ya Upungufu kwenye zilizopitishwa
2000/01
26.1
13.3
-12.8
-49
2001/02
25.5
23.4
-2.1
-8
2002/03
34.8
30.2
-4.6
-13
2003/04
73.0
60.4
-12.6
-17
2005/06
133.5
97.4
-36.1
-27
2006/07
122.2
86.3
-35.9
-29
2007/08
131.9
124.1
-7.8
-6

Chanzo: Takwimu za Wizara ya Kilimo na Ukokotoaji binafsi


Mheshimiwa Spika, aidha takwimu zinaonyesha kwamba katika kipindi cha mwaka wa fedha 2010/11 kwa upande fedha za ASDP. Hazina ilitoa Shilingi bilioni 107.1 kwa wizara zinazojihusisha na kilimo (Agriculture Sector Lead Ministries) kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya sekta ya kilimo. Lakini kati ya fedha hizo, ni kiasi cha shilingi bilioni 77.9 (72.8%) ndizo zilizotumika hadi mwisho wa mwaka huo wa fedha.
Mheshimiwa Spika, Hii maana yake nini kwa nchi ambayo mara zote taarifa zinatolewa kuwa miradi imekwama kutokana na ukosefu wa fedha, ni dhahiri kuwa inawezekana tatizo la utoaji wa fedha za miradi nje ya muda bado linaendelea pia uwezo mdogo wa watendaji katika utumiaji wa fedha. Ujumla wa haya yote ni kukifanya kilimo kuendelea kudumaa na kushindwa kutoa tija inayokusudiwa.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inayoongozwa na CHADEMA inasema kama mipango hiyo ipo tayari kwenye makaratasi tatizo ni utekelezaji. Serikali ya CCM haiwezi kutekeleza mipango hiyo kwani imekuwa ikifanya hivyo siku zote. Naomba kunukuu kauli iliyokwishatolewa hapa Bungeni kwamba “insanity is keeping doing the same thing expecting different results”
Mheshimiwa Spika, ukuaji wa miji kimekuwa ni kichocheo kikubwa cha mchakato wa maendeleo kutokana na uwepo wa “forward and backward linkages” kwa bidhaa nyingi za kilimo na viwandani. Njia hii imekuwa na mafanikio makubwa kwa nchi nyingi hasa zile zilizoendelea ikiwemo China na Korea ya Kusini na nyingine kama vile India,Thailand zimejikwamua kutoka kwenye umasikini wa kipato kupitia ukuaji wa miji midogo[18].
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kuangalia upya sera ya kilimo ili iweke mazingira wezeshi kwa wakulima wadogo waweze kunufaika na kukua na kuwa wakulima wakubwa.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Malengo ya Maendeleo ya Milenia (MDGs) yalikubaliwa na wakuu wa nchi mbalimbali duniani Septemba mwaka 2000, kwamba  Mwaka 2015 ni tarehe ya mwisho ya kufikiwa kwa malengo nane ambayo pamoja na mambo mengine, yanalenga katika, kuondosha umasikini wa kipato na njaa lengo linalohusu moja kwa moja sekta hii ya kilimo. Ukweli ni kwamba hata kipindi cha kukamilika kwa Malengo ya Maendeleo kingeongezwa, ni dhahiri tusingeweza kuondoa umasikini wa kipato na njaa kutokana na kushindwa kutambua kiini hasa cha matatizo ya wakulima na kilimo.
Mheshimiwa Spika, Maendeleo ya Nchi ya Thailand katika kupambana na kuushinda umasikini halikuwa jambo rahisi na la siku moja, bali ni matokeo ya uwekezaji makini na nia thabiti ya kisiasa ambayo ilichangiwa na mambo mengi ikiwemo uwekezaji wa nishati vijijini. Asilimia 97 ya wananchi waishio vijijini Thailand wanapata umeme wa uhakika, jambo hili linaenda sambamba na uzalishaji kwenye sekta ya kilimo wenye tija.

Mheshimiwa Spika, Ni kwa namna gani Tanzania tunaweza kufanya ulinganisho na wenzetu hao? Takwimu za bajeti ya kazi toleo la mwaka 2007 zinaonyesha kuwa ni asilimia 2.5 tu ya watanzania waishio vijijini ndio waliounganishwa na gridi ya taifa[19].
Aidha, Kwa mujibu wa taarifa ya Waziri wakati alipokuwa anazungumza na watanzania waishio Nchini Uingereza alisema kuwa “Asilimia 18.4 ndio wanaotumia umeme hapa Tanzania na kati ya hao ni asilimia 6.6 tu wako  vijijini.  Sambamba na hilo, kwa mujibu wa mtandao wa Ofisi ya  Makamu wa Rais ni kuwa “hapa nchini takriban asilimia 14 tu ya Watanzania ndio wanaotumia nishati ya umeme na kwamba hali ni mbaya zaidi vijijini wanakoishi takriban asilimia 80 ya Watanzania ambapo ni asilimia 2.5 tu ndio wanaotumia umeme kutokana na uwezo mdogo wa kifedha wa wananchi wakati upatikanaji wa nishati hizo nao hautoshelezi’.
Mheshimiwa Spika,  Akiwakilisha bajeti ya mwaka wa fedha 2009/2010 yenye kaulimbiu "Kilimo Kwanza", Waziri wa Fedha wakati huo, Mhe. Mustafa Haidi Mkulo alisema "Misingi na shabaha ya bajeti hii imezingatia Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2025 ambayo inalenga kuwa Tanzania iwe ni nchi yenye kiwango cha kati cha mapato… na hali bora ya maisha kwa wananchi, ilani ya uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2005, MKUKUTA, Mpango Maalum wa Maendeleo Tanzania…na Malengo ya Maendeleo ya Milenia," alisema Waziri Mkulo.
"Hatua zitachukuliwa kuhakikisha kuwa kilimo kinapatiwa rasilimali zaidi ikiwemo pembejeo na zana za kilimo
".
Mheshimiwa Spika, Kauli mbiu ya kilimo kwanza ambayo ni mwendelezo wa Sera ya Kilimo ya mwaka 1997 imeonyesha na inaelekea kushindwa kukidhi malengo kutokana na ukweli kama ulivyotolewa na Mkurugenzi mtendaji wa SAGCOT katika mahojiano yake na Gazeti la Kiingereza la Business Times kuhusiana na mada ya faida na hasara za Kilimo kwanza  alisema na nukuu  ‘It is true the Kilimo Kwanza initiative will bring fundamental changes in Tanzania, but this cannot happen overnight; there is a need to wait for other developments to support it, such as infrastructure, rural electrification and construction of enough warehouses, good market system for agricultural products[20]. Kwa tafisiri isiyo rasmi kuwa ni ukweli kwamba mpango wa kilimo kwanza utaleta mabadiliko ya msingi hapa Tanzania, lakini jambo hili halitatokea ghafla, hivyo ni muhimu kuwa na maendeleo mengine ya kusaidia mpango huu kama vile miundombinu,nishati ya umeme vijijini,ujenzi wa nyumba za kutosha, mifumo mizuri ya masoko kwa ajili ya mazao ya kilimo
Mheshimiwa Spika, kwa mtazamo huo na ukweli huo hadi kupatikane maendeleo kwenye sekta hizo wezeshi itatuchukua miaka mingine mingapi?
Mheshimiwa Spika, toka wakati huo hadi sasa watanzania hawaoni tofauti katika kilimo na kuna wanaoona kwamba kilimo kimeshuka kwa kulinganisha na miaka ya nyuma. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kuangalia jinsi ya kuendeleza shughuli mbalimbali zisizokuwa za kilimo (non farm activities) zinazofanywa na wakazi wa vijijini, ili kusaida kukuza hali ya kibiashara katika maeneo ya vijijini.
HITIMISHO
Mheshimiwa Spika, Kwa unyenyekevu mkubwa napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa Rehema na fadhila kwa kunijalia uhai, afya njema na kwa upendo wake anaotujalia kila mmoja wetu kwa nafasi yake.
Mheshimiwa Spika, kwa namna ya kipekee napenda kumshukuru Kiongozi wa Kambi ya Upinzani na Mwenyekiti wa Chama makini cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na Makamanda wenzangu wote kwa mchakato wa mwanzo wa kuifungua nchi yetu kwa kurudisha madaraka ya kiutendaji kwa wananchi kupitia M4C.
Mheshimiwa Spika, kama sitowashukuru wananchi wa Wilaya ya Hanang’ nitakuwa sijawatendea haki kwa ushirikiano mkubwa wanaonipatia katika kuhakikisha Wilaya yetu inakuwa kiongozi katika kupambana na ufisadi katika miradi ya maji na ile ya kilimo.
Mheshimiwa Spika, mwisho lakini kwa umuhimu mkubwa ni kwa familia yangu hasa wanangu Emiliana na Linus. Nasema tuendelee kuvumiliana kwa kipindi chote nitakachokuwa kwenye uhamasishaji wa M4C.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo kwa niaba ya Kambi Rasmi ya Upinzani, naomba kuwasilisha.

……………………………….
Rose K.Sukum(Mb)
Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani-
Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika.
22.04.2013




 [1] The world Bank, Tanzania Economic Update, 2nd Edition, November, 2012.
[2]Ibid.
[3]http://savingaplanetatrisk.org/links-farmer-suicides-to-monsanto/
"Climate change and the global food shortage crisis could end civilization as we know it today."

[4] Feedback and recommendations from Civil Society Organisations for the “Greenprint” strategy of the Southern Agricultural Growth Corridor of Tanzania Initiative
[5] Philippe Egger,  Director of the ILO Bureau of Programming and Management
[6] Gazeti la Serikali la Habari leo la 14 Januari 2013
[8] Wizara ya Kilimo na Ushirika-Maendeleo ya Kilimo na Ushirika kwa Kipindi cha miaka 50 ya uhuru wa Tanzania Bara (1961-2011)
10. Chanzo: Idara ya Zana za Kilimo na Halmashauri

[10] Analysis of Agriculture Budget Trends and Outcomes in Tanzania, by Dr. Damian M. Gabagambi of Sokoine University of Agriculture and Ms. Magreth Henjewele
[11] USHIRIKA TANZANIA, kimetungwa na Pius Ngeze
[12]  DR Anaclet Kashuliza, Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji wananchi Kiuchumi,Ufunguzi wa mkutano wa 19 wa SCCULT, SHINYANGA, 26 FEBRUARI 2012
[13] Teknolojia za Utayarishaji, Usindikaji na Hifadhi ya Mazao ya Nafaka baada ya Kuvuna.  Kitabu namba 1
[14] Agribusiness innovation in six african countries, The tanzanian experience, report prepared for the world bank institute. By Dr. J. J. Mpagalile, Prof. R. Ishengoma and Prof. P. Gillah Sokoine University of Agriculture P. O. Box 3000 Chuo Kikuu, Morogoro, Tanzania
[15] Southern Agricultural Growth Corridor of Tanzania Appendix IV: Value Chain and Market Analysis

[16] http://www.commodityonline.com/news/vietnam-cashew-nut-export-revenue-soars-37338-3-37339.html
[17] Nganga  N. B  mtafiti  na mchambuzi mshauri masuala ya Pamba
[18] http://www.worldbank.org/tanzania/economicupdate.
[19] Reducing  Poverty  through  Kilimo kwanza : What can we learn from the East ?y through

[20]  The pros and cons of 'Kilimo Kwanza'  written by TIMES  CORRESPONDENT, Friday, 29 June 2012



No comments:

Post a Comment