Tuesday, April 23, 2013

Lissu: Fujo zitakoma bungeni Spika akiacha upendeleo


Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu, amesema fujo zitaisha bungeni ikiwa Spika wa Bunge, Naibu na Wenyeviti watafuata na kusimamia kanuni za Bunge bila kupendelea upande wowote.

Lissu, ambaye pia ni Mnadhimu Mkuu wa Kambi ya Upinzani bungeni, aliyasema jijini Dar es Salaam jana wakati akihojiwa na kituo cha televisheni cha ITV.

Alisema fujo hazitaisha kama watu hawatafuata kanuni na Spika kusimamia na kuzingatia mamlaka yake bila ya upendeleo wowote.

“Tatizo kubwa Spika anafanya kazi bila kufuata kanuni za Bunge. Kuna mambo mengine anayatolea maamuzi bila kufuata kanuni za Bunge. Mfano suala letu la adhabu tuliyopewa wabunge watano wa Chadema ya kutohudhuria vikao vitano. Hakuna katika kanuni za Bunge. Spika alipaswa kupeleka majina yetu katika Kamati ya Maadili ili ichunguze na kupendekeza adhabu kisha ipeleke taarifa bungeni na Bunge ndilo litoe adhabu," alisema. 

Alisema kama utaratibu ndani ya Bunge unakiukwa, Chadema wataendelea kupinga hata kama watafukuzwa kila mara kwani wasipofanya hivyo athari yake itakuwa kubwa hapo baadaye.

“Hata kama watu wote watasema niache kuongea, nasema siwezi kuacha mimi ni mbunge na sehemu yangu kubwa ya kazi ni bungeni. Hivyo nikifika huko lazima nitazungumza, kama sitazungumza ndani ya Bunge, nitazungumza nje na nikirudi tena ndani nitalizungumza,” alisema.

Lissu aliongeza kuwa hulka ya Bunge ni kelele na  hii si hapa nchini tu, bali hata nchi nyingine, ila tatizo la Watanzania ni uchanga wa mfumo wa vyama vingi na ndiyo maana wanaona mambo hayo kama ni mageni.
CHANZO: ALASIRI

Bonyeza Read More Kuendelea


Kiti cha Spika kitazua makubwa-Wabunge


Wabunge wanne kati ya sita wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ambao wiki iliyopita walifukuzwa bungeni kwa utovu wa nidhamu, wamesema Watanzabia watarajie kutokea mwa mambo mamkuwa ikiwa kiti cha Spika kitaendelea kuwabeba wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kuwanandamiza wa Upinzani.

Kauli hiyo ilitolewa jijini Mwanza juzi jioni katika  mkutano wa hadhara uliofanyuika kwenye Shule ya Msingi Mbugani.

Wabunge hao Mchungaji Peter Msigwa (Iringa Mjini), Joseph Mbilinyi maarufu kama “Sugu” (Mbeya Mjini), Highness Kiwia  (Ilemela) na Hezekiah Wenje (Nyamagana).

Hata hivyo, wenzao wawili Tundu Lissu (Singida Mashariki) na Godbless Lema (Arusha Mjini) hawakudhuria mkutano huo kwa kuwa jana walitakiwa kuhudhuria mahakamani katika kesi ya kupitia rufani dhidi ya ushindi wa Lema katika Mahakama ya Rufani, jijini Dar es Salaam.

Alisema kwamba walishangaa kuona kiti cha Spika kilishindwa kumfukuza bungeni Mbunge wa Kigoma Mjini (CCM), Peter Serukamba, ambaye asubuhi yake alikuwa ametoa tusi zito ambalo haliwezi kutamkwa hadharani, lakini kikamtoa Lissu ambaye alikuwa anaomba mwongozo kwa mujibu wa kanuni.

“Tumekuja kuwaambia kwa nini tulikwenda kuzuia kiongozi wetu kuondolewa bungeni kwa sababu alikuwa anatimiza wajibu wake, lakini pia kwa sababu kiti cha Spika kilishindwa kumfukuza Serukamba ambaye siku hiyo asubuhi alitukana tusi zito ambalo siwezi kulisema hapa hadharani,” alisema Mbilinyi.

Aliongeza kwamba wao wanatambua kuwa wananchi hawakuwatuma kwenda bungeni kugonga meza na kusaini posho, isipokuwa kupigania maslahi yao hasa pale yanapoonekana kukiukwa kwa makusudi na kulindwa na kiti cha Spika.

Aliongeza kwamba ingawa kiti cha Spika kimewafukuza wabunge sita wa Chadema, lakini wakae wakijua kuwa waliobaki wataendeleza moto ule ule hadi kitakapoeleweka.

Sugu pia alimuonya Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya, Athuman Diwani, ambaye inadaiwa kuwa  anataka kuzuia mkutano kama huo unaotarajiwa kufanyika mkoani humo kesho kwa kusema kwamba lazima ufanyike hata kama watapigwa mabomu.

“Nasikia eti RPC wa Mbeya amezuia mkutano wetu usifanyike, sasa natoa salamu kwake, tunakwenda kufanya mkutano Jumatano kama ulivyopangwa, tunaomba mtuombee kwa sababu tuko tayari kwa lolote,” alisema.

Mchungaji Msigwa alisema kwamba wamekubali kuhatarisha maisha yao kwa kusema maovu ya serikali na viongozi wa CCM bila uoga wowote.

Kiwia alisema kabla ya kuwa mbunge, alikuwa akiwaona wabunge wa CCM wenye umri mkubwa na wakiwa wamevaa suti akafikiri labda wana busara.

Hata hivyo, alisema amegundua kuwa wabunge wengi wa CCM wameamua kuwageuka wananchi wao kwa kushindwa kutetea maslahi yao bungeni.

“Wabunge wa CCM wanakaa kujadili jinsi ya kutumia fedha zilizorejeshwa na serikali ya Uingereza katika kashfa ya ununuzi wa rada badala ya kujadili namna ya kuwaadhibu wale wote waliosababisha hasara hiyo, ndipo masuala mengine yafuate,” alisema.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment