MBUNGE wa Viti Maalumu Cecilia Pareso (CHADEMA) amewashangaa wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kukaa bungeni bila kujua maana halisi ya umuhimu wa vyama vya upinzani.
Alitoa kauli hiyo jana alipokuwa akichangia mjadala wa hotuba ya bajeti ya Waziri Mkuu na kusema kuwa kazi ya vyama vya upinzani bungeni ni kuikosoa serikali pale inapotenda kazi zake kinyume na si kuitetea.
Mbali na hilo alieleza kushangazwa na serikali kushindwa kuwachukulia hatua watumishi ambao wanasababisha halmashauri kupata hati chafu badala yake halmashauri hizo kupewa asilimia 25 ya fedha za maendeleo.
Alieleza kuwa kitendo cha kutowawajibisha watumishi ambao husababisha hasara kwa halmashauri na kutoa adhabu kwa halmashauri kwa kunyimwa ama kupunguziwa fedha za maendeleo ni dalili mbaya kwa serikali kwa kushindwa kusimamia majukumu yao ya kulinda mali ya umma.
“Haiwezekani mtu ambaye anatenda kosa kubwa kama hilo anaachwa na badala yake anayepewa adhabu ni mtu mwingine ambaye ni mwananchi, asiyekuwa na hatia, kutokana na hali hiyo ndiyo maana wabunge wa vyama vya upinzani wanapiga kelele na kuhoji lakini kutokana na wabunge wa CCM kutokuwa na weledi kuhusu maana ya vyama vya upinzani wanabaki kushangaa na wao kujifanya sehemu ya serikali badala ya kuikosoa serikali na kuisimamia ili itende mambo ambayo ni manufaa kwa Watanzania,” alisema Pareso.
Mbali na hilo alisema kuwa serikali imekuwa na mipango mingi lakini ni kama imewasahau madiwani kwa kushindwa kuboresha masilahi yao na serikali iangalie uwezekano wa kuwaongezea posho madiwani na kuwaruhusu kufanya ziara kwa jili ya kujifunza.
“Suala hilo lilikuwepo hapo awali lakini wazri mkuu alilifuta jambo hilo hivyo kutokana na umuhimu wa madiwani namtaka waziri mkuu kuangalia upya jinsi ya madiwani kuwaongezea posho pamoja na kuwaruhusu ili waweze kufanya safari kwa ajili ya kujifunza,” alisema Pareso.
Pamoja na mambo mengine aliitaka serikali kubadili uendeshaji wa mchakato wa utungaji wa sheria ndogo kwani mchakato huo una mlolongo mkubwa ambao hufanywa na halmashauri husika na baadaye kupeleka kwa waziri mkuu na huko hukaa kwa muda mrefu bila kupitishwa.
Hatua hiyo ya kutopata sheria hiyo kwa muda mrefu husababisha halmashauri kushindwa kutekeleza majukumu yake, hivyo aliitaka kubadili utaratibu huo kwani umekuwa na usumbufu mkubwa.
No comments:
Post a Comment