Wednesday, April 17, 2013

''Uchaguzi mabaraza ya Katiba urudiwe'


Tume ya Mabadiliko ya Katiba imetakiwa kurudia upya mchakato wa kuwapata wajumbe wa mabaraza ya kata, mkoa wa Dar es Salaam kwa madai kuwa, ulikuwa na kasoro nyingi.

Rai hiyo ilitolewa jana jijini Dar es Salaam na Katibu wa jukwaa la wazi la semina ya jinsia na maendeleo (GDSS) linaloratibiwa na Mtandao wa Jinsia na Tanzania (TGNP), Badi Darusi, katika mkutano na waandishi wa habari.

Alisema kutokana na hali iliyojitokeza ni dhahiri kuwa tume ilishindwa kusimamia ipasavyo kanuni na taratibu za uchaguzi kwa kuwaachia wanamaendeleo ya kata, ambao ni wanasiasa, yaani Madiwani na Wenyeviti wa Mitaa.

Darusi alisema mchakato huo uligubikwa na vitendo vya kisiasa, rushwa, vitisho, unyanyasaji na ubaguzi wa kijinsia, hali iliyopelekea baadhi ya watu waliokuwa na sifa kuwa wajumbe wa mabaraza hayo kuenguliwa kimakosa kutokana na utashi pamoja na maslahi binafsi ya watu wachache.

“Tume ya Katiba ingalie hili suala kwa makini na ilifanyie kazi kwa kuwa kasoro hizo siyo nzuri hata kidogo kwani itapelekea kuwapo kwa katiba ya watu wachache wenye maslahi yao binafsi," alisema Darusi. Alifafanua kwamba Katiba inatakiwa kuwa ya watu wote bila ubaguzi wowote kama kisiasa au kijinsia. Aidha, aliitaka tume kufanya tathimini ya zoezi zima la upatikanaji wa wajumbe wapya katika mikoa yote ambayo kasoro zimebainika ili iweze kupata wajumbe halali wa mabaraza hayo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa GDSS, Janeth Mawinza aliitaka Tume hiyo kuwa makini kwa hatua zitakazofata ikiwamo zoezi la kuwapata wawakilishi wa Bunge la Katiba.

Pia aliitaka Tume itambue mchango wa wanahabari katika mchakato mzima wa uundaji wa Katiba mpya na kuhahakikisha wanashirikishwa kikamilifu katika hatua za uundaji wa mabaraza ya Wilaya, Mkutano Mkuu wa katiba na kupewa nafasi katika Bunge maalum la katiba.

Chaguzi zilizotawaliwa na kasoro nyingi jijini Dar es Salaam ni katika Kata ya Mabibo ambako uchaguzi ulisitishwa na Kata ya Wazo Hill ambako uchaguzi ulifanyika katika mazingira ya kutatanisha.


Bonyeza Read More kuendelea


Mabaraza ya Katiba yazidi kuwa mwiba



Zoezi la mchakato wa kuandika Katiba mpya limeibua mvutano bungeni kati ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na Kiongozi wa Kambi ya Upinzani bungeni, Freeman Mbowe.

Mvutano huo ulitokea wakati Pinda alipokuwa akijibu hoja za wabunge waliochangia kwenye hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka 2013/14.

Katika hotuba yake, Mbowe alitahadharisha kwamba Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kitasusia mchakato wa Katiba unaoendelea kwa kuwa inaonekana kwamba mabadiliko yaliyokusudiwa yanaelekea kuilinda CCM na Serikali yake na kuendeleza baraka za “Status Quo” yaani hali iliyoko sasa.

Alisema ushahidi wa mwanzo unaonyesha kwamba utaratibu wa kupata mabaraza ya katiba ni mabaraza ya CCM na siyo mabaraza ya Watanzania; kutokana na Wajumbe hao kuchaguliwa na kamati ya maendeleo ya kata.

Akijibu, Pinda alisema katika kuwapata wajumbe wa mabaraza ya katiba ya wilaya, Tume ilitumia muundo wa serikali za mitaa na taratibu za mikutano katika ngazi hizo ikiwa ni katika vijiji, mitaa na kata.

Alisema muundo huo siyo ubunifu wa Tume bali umeainishwa katika Sheria za Serikali za Mitaa.

Alisema katika ngazi ya kata, chombo kinachotambuliwa kisheria kutoa maamuzi kwa niaba ya wananchi, ni kamati ya maendeleo ya mtaa na kwamba maamuzi ya kutumia chombo hicho yana msingi katika Sheria za Serikali za Mitaa.

"Propaganda zinazoeleza kuwa mabaraza hayo ni ya CCM, na si mabaraza ya katiba ya Watanzania wote, siyo za kweli, bali zimelenga kujenga chuki na kupotosha umma wa Watanzania.  Uanachama au kutokuwa mwanachama wa chama cha siasa haikuwa sifa mojawapo ya kuchaguliwa kuwa mjumbe wa baraza la katiba la wilaya," alisema.

Alisema madai ya Mbowe yamelenga kupotosha umma kwa kuwa wananchi walitakiwa kuomba kwenye ngazi za vijiji na mitaa kwa Tanzania Bara na shehia kwa Zanzibar.

Alisisitiza kwamba haitawezekana wajumbe wa mabaraza ya katiba ya wilaya kuchaguliwa na wananchi moja kwa moja katika ngazi ya kata.

Aidha, Pinda alisema wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba hawatokani na wana CCM peke yake bali ni mchanganyiko wa vyama mbalimbali kikiwamo Chadema na kwamba ni mchanganyiko wa watu waliopendekezwa kutoka vyama vya siasa vyenye usajili wa kudumu, jumuiya za kidini, asasi za kiraia, jumuiya au taasisi zisizo za kiserikali na makundi ya watu wenye malengo yanayofana.

"Hivyo, siyo kweli kwamba Tume inaelekea kutengeneza Katiba itakayoilinda CCM," alisema.

Pinda alisema kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Sura ya 83, mchakato wote wa kupatikana kwa Katiba Mpya umekuwa ukiwahusisha na utaendelea kuwahusisha wananchi katika hatua zote.

Alisema siyo kweli kwamba CCM inabebwa japokuwa ndiyo yenye madiwani, wenyeviti wa mitaa na vijiji.

"Mchakato huo unashirikisha wananchi wa vyama vyote na wasiokuwa na vyama. Siyo sahihi kusema kuwa mabadiliko ya katiba yataendelea kuibeba CCM.  Yote yanayofanywa na yatakayofanywa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba ni kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba inayoainisha mchakato ambayo ilipitishwa na Bunge hili na kisha kuwekwa mezani katika Baraza la Wawakilishi Zanzibar," alisema Pinda.

Alisema tume imekusanya maoni ya wananchi kutoka mikoa yote na kwamba hoja ya utaratibu wa hovyo unaoelezwa na kambi ya upinzani haina mashiko kwa kuwa utaratibu uliotumika ni mzuri.

Pinda alisema: "Tunastahili kuipongeza (tume) kwa kazi inayofanya na siyo kuanza kuishambulia, kuishutumu na kuibeza kwa kazi ambayo tuliwatuma kupitia sheria tuliyoipitisha sisi wenyewe."

Alisema tume hiyo inajumuisha wajumbe makini, wenye uzoefu, weledi na wengine ni maprofesa.

Hata hivyo, baada ya maelezo hayo, Mbowe alisimama kwenye fungu la mshahara wa Waziri Mkuu na kuonya kwamba Chadema itasusia mchakato huo kama marekebisho ya uchaguzi wa mabaraza hayatafanywa.

Alisema katika mchakato huo, Watanzania wanatakiwa kuwa wamoja na kushikamana na kwamba majibu ya Pinda yameonekana kuwagawa Watanzania.

Mbowe ambaye pia ni mbunge wa Hai na Mwenyekiti wa Chadema, alisema kwa ujumla uchaguzi wa mabaraza ya kata umeghubikwa na utata na kwamba unalenga kuwagawa Watanzania kuanzia ngazi ya chini.

Baada ya Pinda kumaliza kujibu hoja mbalimbali za wabunge na wabunge kuhojiwa, Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika, alisimama na kutaka muongozo wa spika juu ya maelezo ambayo alidai siyo sahihi yaliyotolewa na Waziri Mkuu kuhusu muundo wa mabaraza ya kata.

Mnyika alisema kuwa Waziri Mkuu hakusema ukweli alipolieleza Bunge kuwa katika Sheria ya Katiba Mpya iliyopitishwa na Bunge, muundo wa mabaraza ya kata ulipitishwa.

Aidha, alisema kuwa Waziri Mkuu pia hakusema ukweli alipoeleza kuwa Chadema hawakupeleka maoni yao juu ya muundo huo, kwani yeye (Mnyika) akiwa Naibu Katibu Mkuu wa Chadema ndiye aliwasilisha maoni ya chama hicho kwa tume, lakini yakapuuzwa.
Spika Anne Makinda alisema kuwa atatoa mwongozo wake leo.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment