UTANGULIZI
Mheshimiwa Spika,
kwa mujibu wa Kanuni ya 99(9) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, toleo la 2013,
naomba kuwasilisha maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inayoongozwa na
CHADEMA, kuhusu mapitio ya utekelezaji wa Bajeti ya 2012/2013 na makadirio ya
mapato na matumizi ya Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma kwa mwaka
wa fedha 2013/2014.
Mheshimiwa Spika,
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inayoongozwa na CHADEMA, kipindi hiki itajikita
katika mambo machache mahususi katika Ofisi ya Rais - katika Utawala bora,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Mahusiano na Uratibu - ambayo tunayaona ni
mapungufu. Lengo la kufanya hivyo ni kuitaka Serikali ama ichukue hatua ya
kuyatokomeza mapungufu hayo kwa kutangaza hadharani nia yake ya kuyakomesha, kisha
ichukue hatua mwafaka, au ijiuzulu kwa kushindwa kuongoza dola.
- UTAWALA BORA
2.1.
Idara
ya Usalama wa Taifa – Ikulu
Mheshimiwa Spika, kwa
muda mrefu sasa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inayoongozwa na CHADEMA
imeitaka Serikali kuwachukulia hatua maafisa wa Idara ya Usalama wa Taifa –
Ikulu ambao wanatuhumiwa kujihusisha na vitendo vya kihalifu vya utekaji na
utesaji kwa watu wanaoonekana kuikosoa Serikali, lakini mpaka sasa hakuna hatua
dhahiri zinazochukuliwa ilhali matukio
hayo ya utekaji na utesaji yanazidi kuongezeka katika nchi yetu.
Mheshimiwa Spika, aliyetajwa
na Gazeti la Mwanahalisi kuhusika na
kitendo cha kinyama cha kumteka na kumtesa Dkt. Ulimboka mwezi Juni, 2012 ni afisa
wa Usalama wa Taifa, Ramadhani Ighondu Abeid. Tulitarajia Serikali, kupitia
Jeshi la Polisi, ingemkamata na kumhoji mtu huyu ili kujiridhisha na tuhuma
dhidi yake na kuchukua hatua kwa mujibu wa sheria za nchi, lakini mpaka leo
hakuna chochote kilichofanyika kuhusu uhalifu dhidi ya binadamu aliofanyiwa
Dkt. Ulimboka, jambo ambalo linaashiria kwamba Serikali iliridhika na
kilichotokea. Lakini jambo baya zaidi ni kwamba Gazeti la Mwanahalisi lililosaidia kugundua uhalifu huo lilifungiwa kwa muda
usiojulikana.
Mheshimiwa Spika, mazingira
ya kuteswa kwa Mhariri wa Shirika la Habari,
ndugu Absalom Kibanda yanafanana sana na yale ya kutekwa na kuteswa kwa Dkt.
Ulimboka. Aidha, aina ya utesaji (mfano kung’olewa kucha, meno na kutobolewa jicho)
unafanana sana na aina ya mateso aliyopata Dkt. Ulimboka. Hivyo, ushahidi wa
kimazingira unaonesha kwamba waliomteka na kumtesa Dkt. Ulimboka yumkini ni
walewale waliomteka na kumtesa Absalom Kibanda au mawakala wao.
Mheshimiwa Spika, katika
sakata la Dkt. Ulimboka, jeshi la polisi lilidai kuwa limemkamata mtu mmoja
lililodai kuwa ni raia wa Kenya ambaye hatima ya kesi yake haijulikani mpaka
sasa. Kwa tukio la Absalom Kibanda hadi sasa hakuna taarifa rasmi ya watu
walioshtakiwa kuhusu uhalifu huu dhidi ya binadamu. Dkt. Ulimboka ambaye
angeweza kutoa msaada kwa Polisi kuwakamata waliohusika na uhalifu huo, hajahojiwa
mpaka leo ingawa katika kiapo chake alichokiandika mbele ya mwanasheria wake
alimtaja afisa wa Usalama wa Taifa - Ikulu kuwa alihusika kumteka na kumtesa.
Inashangaza sana kwa nini Serikali haijataka kutumia maelezo ya Dkt. Ulimboka
mwenyewe kuwakamata wahalifu. Jambo jingine la kusikitisha ni kwamba kuna dalili
za wazi kwamba suala la kutekwa na kujeruhiwa vibaya kwa Absalom Kibanda
limesahaulika kabisa.
Mheshimiwa Spika, kwa
mujibu wa Kanuni ya Adhabu ya Tanzania (Penal Code), kuteka na kutesa ni makosa
ya jinai. Ni aibu kwa Idara ya Usalama wa Taifa iliyokabidhiwa jukumu kubwa na
la heshima kubwa la kuulinda usalama na usitawi wa nchi kutuhumiwa kujihusisha
na vitendo vya kikatili kama hivi. Kitendo cha kuhisiwa tu kwamba chombo hiki
cha usalama kinajihusisha na vitendo vya kijinai moja kwa moja kinakikosesha
sifa ya kufanya kazi ya usalama wa taifa. Na kwa kuwa chombo hiki kiko chini ya
mamlaka ya Rais moja kwa moja tayari ni
doa kubwa kwa Rais mwenyewe, Serikali
yake na hata kwa chama chake.
Mheshimiwa Spika, kwa
mujibu wa Sheria ya Ujasusi na Usalama ya Tanzania (Tanzania Intelligence and
Security Services Act) ya 1996, Idara ya Usalama wa Taifa hairuhusiwi kufanya
upelelezi wa ufuatiliaji - “ushushushu”
kwa watu wanaoipinga Serikali kwa
misingi ya kisheria na kikatiba (kwa maana ya vyama vya siasa, vyombo vya
habari na wanaharakati). Ibara ya 5(2),
kipengele ‘a’ na ‘b’ inasomeka hivi:
“It shall not be
the function of the Service :
a) to
enforce measures for security or;
b) to
institute surveillance of any person or category of persons by reason only of his or their involvement in
lawful protest or dissent in respect of any matter affecting the constitution ,
the laws or the Government of Tanzania”.
Mheshimiwa
Spika, kwa tafsiri isiyo rasmi, sheria inasema hivi:
“Haitakuwa kazi ya Idara
kufanya yafuatayo:
a) kutekeleza
hatua za usalama, au
b) kufanya
upelelezi wa ufuatiliaji wa mtu yeyote au kundi lolote la watu kwa sababu tu ya
kuhusika na kupinga au kushiriki maandamano halali kuhusiana na jambo lolote la
kikatiba, sheria au Serikali ya Tanzania”.
Mheshimiwa
Spika, nimelazimika kunukuu sheria hii kwa kuwa Kambi Rasmi ya
Upinzani inayoongozwa na CHADEMA, inao ushahidi kwamba maafisa wa Usalama wa
Taifa wamekuwa wakifanya upelelezi wa ufuatiliaji (surveillance) kwa watu
wanaoipinga Serikali kwa misingi ya Katiba na sharia - jambo ambalo ni kinyume na sheria iliyopo.
Mheshimiwa
Spika, ushahidi wenyewe ni kwamba baada ya Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa CHADEMA kutuhumiwa kwamba anahusika na ugaidi na video yake kurushwa
kwenye mitandao ya kijamii, Muhidin Issa Michuzi, ambaye ni mpiga picha wa
Rais, Ikulu, aliandika barua-pepe kwa Salvator Rweyemamu, Prosper Mbena, Hamis
Mwinyimvua, Liberatus Mulamula, Msafiri Marwa, Laurent Ndumbaro na wengine
ambao ni watumishi wenzake wa Ofisi Binafsi ya Rais akiwapongeza kwa kazi nzuri
na ya ziada waliyoifanya ya kutengeneza video ya Lwakatare, na kuwaeleza kuwa hiyo ni kete kubwa kwao hivyo lazima waipigie kelele sana.
Mheshimiwa
Spika, kuna ushahidi mwingine kwamba baadhi ya maafisa wa Idara
ya Usalama wa Taifa (TISS) wanawahonga kwa kuwalipa fedha watumishi wa CHADEMA
ili watoe ushahidi wa uongo dhidi ya kesi inayomkabili Mkurugenzi wa Ulinzi na
usalama wa CHADEMA. Miongoni mwa maafisa hao ni Sinbard Mwagha. Huyu ni ni afisa usalama wa taifa anayefanya kazi makao makuu ya idara hiyo.
Taarifa zilizopo ni kwamba ndiye anayetumika kuendesha michezo ya kuhonga
wanasiasa wa CCM na upinzani, na kwamba ndiye anayehusika pia kuwapanga wabunge wa CCM waongee nini bungeni
wakati wa vikao vya bunge kwa maslahi ya CCM.
Mheshimiwa
Spika, kwa mujibu wa Kanuni ya Adhabu (Penal Code),
kutengeneza ushahidi wa uongo (fabrication of evidence) ni kosa la jinai na
adhabu yake ni kifungo cha miaka saba gerezani. Hivyo, Kambi Rasmi ya Upinzani
inalitaka Jeshi la Polisi kumkamata haraka sana Sinbad Mwagha ambaye tuna imani
anafahamika na kumfungulia mashtaka ya kuhusika katika kutengeneza ushahidi wa
uongo dhidi ya kesi inayomkabili Mkurugenzi wa Usalama wa CHADEMA, Ndugu
Wilfred Lwakatare. Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali
kutoa maelezo ya kina juu ya hatua ilizochukua hadi sasa dhidi ya maafisa wa usalama
wengine ambao wanatuhumiwa kujihusisha na vitendo vya kihalifu.
Kuendelea Bonyeza Read More
2.2.
TAASISI
YA KUPAMBANA NA KUZUIA RUSHWA NA MWELEKEO WA MATUKIO YA RUSHWA NCHINI
2.2.1 Rushwa inavyodidimiza uchumi na
Maendeleo ya Taifa
Mheshimiwa Spika, rushwa na ufisadi bado ni tatizo
kubwa katika nchi yetu na kikwazo kikubwa katika kuleta maendeleo ya nchi
yetu. Bado hatujafanikiwa kupunguza tatizo hili kubwa linalodidimiza
uchumi wa nchi yetu na linalochangia katika kujenga matabaka ya matajiri haramu
na masikini waliosababishiwa umasikini na mfumo wa kifisadi.
Mheshimiwa
Spika, kwa sababu Serikali ina
kigugumizi kuhusu rushwa na ufisadi, baadhi ya taarifa zihusuzo mambo hayo
hufichwa. Kwa mfano, Serikali imekaa kimya kuhusu baadhi ya mikataba na ripoti
mbalimbali – jambo linalotafsiriwa kwamba ni mchakato wa kuwalinda watu
waliohusika na vitendo vya rushwa au ubadhirifu.
Mheshimiwa Spika, ripoti
kwa mfano za EPA, MEREMETA,
Uchunguzi na ukaguzi wa kituo cha mabasi Ubungo, ripoti ya ufisadi katika UDA,
ripoti ya sakata la aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini David
Jairo - ni baadhi tu ya ripoti ambazo bado ni siri.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa ripoti ya “The NATIONAL GOVERNANCE AND CORRUPTION SURVEY ya
mwaka 2009, Ubinafsi na tamaa hasa ya
viongozi wa Serikali inaongoza kwa
asilimia 95.5 kama kisababishi cha rushwa hapa nchini.
Mheshimiwa
Spika, kuna
aina ya rushwa anayonufaika nayo afisa wa Serikali kwa
kupewa mgawo wa kifisadi baada ya kutoa kandarasi kinyume na utaratibu au
upendeleo kwa kampuni fulani. Hivyo, fedha hizo za mgawo zinaelekezwa kwa
taasisi ambayo ana uhusiano nayo au kujengewa nyumba ilimradi fedha hizo za
kifisadi zisipitie kwenye akaunti yake binafsi.
Mheshimiwa Spika, hivi
karibuni kumetokea maafa ya kuanguka kwa majengo ya ghorofa na kuangamiza
maisha ya watu hapa nchini. Kambi Rasmi
ya Upinzani Bungeni inaamini kwamba maafa haya yalitokea kwa sababu ya mfumo wa
kifisadi na rushwa katika utendaji wa Serikali. Hii ni kwa sababu Serikali
ilishashauriwa na na tume ya uchunguzi iliyoundwa na aliyekuwa Waziri Mkuu,
Edward Lowassa kuwa maghorofa zaidi ya 100 Dar es Salaam yamejengwa chini ya
kiwango, lakini hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa, pamoja na Tume hiyo kutumia
mamilioni ya fedha za walipakodi kufanya uchunguzi na kuandika taarifa.
Mheshimiwa Spika, Kambi
Rasmi ya Upinzani Bungeni inashawishika kuamini kwamba ukimya wa TAKUKURU kwenye
maafa haya ya maghorofa kuporomoka ni kutokana na taasisi hiyo kuwa sehemu ya
mfumo wa kifisadi unaoitafuna nchi hii. Ukiukwaji wa makusudi wa kikomo cha
maghorofa (maghorofa 10) ulikuwa ni ishara tosha kuwa mradi huu uligubikwa na
ufisadi – na TAKUKURU ilipaswa kufanya kazi yake ili kubaini kwa nini maghorofa
yalizidishwa, na pia kwa nini hadi wakati huo taarifa za Tume ilikuwa haijatekelezwa.
Mheshimiwa Spika, sababu moja muhimu iliyotajwa katika
Taarifa ya Tume hiyo ni kukosekana
kwa usimamizi na uwajibikaji miongoni mwa watumishi wa serikali (86%), uwezo
mdogo wa kusimamia sheria na kuhakikisha zinatekelezwa na upungufu katika
utoaji wa adhabu kali kwa wanaojihusisha na vitendo vya rushwa (85.6%).
Mheshimiwa Spika, ili
tuweze kuimarisha mapambano dhidi ya rushwa, kwanza kabisa ni lazima tujenge
taasisi imara na huru na zenye kufanya kazi zake kwa weledi na umakini mkubwa.
Lazima taasisi hizi si tu ziwe huru; bali pia zionekane kuwa huru. Muundo
wa TAKUKURU ni vyema ukaangaliwa upya katika mchakato unaoendelea hivi sasa juu
ya kuandika Katiba mpya.
Mheshimiwa Spika, Mkurugenzi wa TAKUKURU ambaye ni
mteule wa Rais, ni vigumu sana kuwa huru na kuvichunguza vyombo vingine ambavyo
vipo chini ya mamlaka ya Rais. Kwa maneno mengine, ni vigumu kumchunguza
aliyekuteua na kuchukua hatua kali dhidi yake.
Katika mfumo uliopo, Rais huyo huyo ndiye Mwenyekiti wa chama tawala;
hivyo inakuwa ni vigumu sana kwa chombo hiki kuchukua hatua kali hata dhidi ya
chama; kwani kufanya hivyo kutakuwa pia ‘kumuadhiri’ mkuu wake wa kazi
aliyemteua ambaye kwa kofia yake nyingine ni Mwenyekiti wa chama. Lakini ni mara ngapi katika chaguzi za Chama
cha Mapinduzi tumesikia Rais ambaye ni Mwenyekiti wa CCM akilalamikia chaguzi hizo
kuwa ziligubikwa na rushwa, lakini hatujawahi kusikia kuwa wahusika wa matukio
hayo wamekamatwa na TAKUKURU japokuwa ushahidi unakuwepo.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Taarifa ya Hali ya Umasikini ya mwaka 2011 iliyotolewa Mei 2012, umma haujaridhika na juhudi
zinazofanywa na Serikali katika utendaji mzima wa Taasisi ya Kupambana na Kuzuia
Rushwa kutokana na sababu kuu kuwa watu
wengi waliokuwa wanahusika na rushwa
kubwa wameachiwa huru.
2.2.2.
Maazimio ya Kongamano la Wadau wa Rushwa
Mheshimiwa Spika, mnamo tarehe 03.05.2010 kulikuwa na Mkutano wa kutathmini maazimio ya Kongamano la Rushwa la mwaka 2009 ambalo lilihusisha wadau mbalimbali wa kupambana na rushwa nchini wakiwemo kutoka Ofisi ya Bunge na mgeni Rasmi katika kongamano hilo alikuwa Mheshimiwa Samwel Sitta ambaye alikuwa Spika wa wakati huo. Katika kongamano hilo, maazimio zaidi ya 30 ya jinsi ya kukabiliana na kupambana na rushwa katika taifa letu yalipitishwa.
Mheshimiwa Spika, miongoni mwa maazimio hayo ni pamoja na azimio namba (4) ambalo lilikuwa ni kuitaka TAKUKURU kuanzisha gazeti maalum litakalosambazwa mpaka vijijini lenye kuelimisha umma kuhusiana na masuala ya rushwa.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inayoongozwa na CHADEMA inaitaka Serikali kulieleza Bunge juu ya hatua iliyofikiwa katika mchakato wa kuanzishwa kwa gazeti hilo. Aidha, azimio namba 11 lilihusu viongozi kutangaza mali zao pindi wanapokuwa wanaondoka madarakani; utekelezaji wake umefikia hatua gani?
Mheshimiwa Spika, katika azimio namba 15 la Kongamano la Rushwa, TAKUKURU ilitakiwa kuhakikisha kuwa inawekeza zaidi katika fani ya habari za kiuchunguzi (investigative journalism) kwa ajili ya kuwajengea uwezo zaidi wanahabari katika kufichua na kuandika taarifa za rushwa hapa nchini. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inataka kujua utekelezaji wa azimio hili umefikia wapi na hasa ikizingatiwa kuwa gazeti la Mwanahalisi lililokuwa linaandika habari za kiuchunguzi kuhusiana na rushwa sasa limefungiwa kwa muda usiojulikana.
Mheshimiwa Spika, azimio la 27
la kongamano hilo liliitaka serikali iache mara moja utaratibu wa kuwahamisha
watumishi wa umma ambao ama ni wabadhirifu/walarushwa kama sehemu ya adhabu kutokana na kitendo cha
wizi na/au ubadhirifu wa mali ya umma kwenye ofisi za umma na badala yake
washughulikiwe kwa mujibu wa sheria za rushwa na za jinai zilizopo katika mfumo
wetu wa sheria hapa nchini. Kambi
Rasmi ya Upinzani Bungeni inataka
kupata majibu ni hatua gani serikali imefikia katika kutekeleza azimio hili
kama kweli tuna nia ya dhati ya kupambana na wabadhirifu wa fedha za umma na
walarushwa kwenye Ofisi za umma.
3.
MENEJIMENTI
YA UTUMISHI WA UMMA
3.1.
Utaratibu
wa Ajira kwa Mkataba kwa Watumishi
waliostaafu
Mheshimiwa Spika,
kwa mujibu wa sheria za Tanzania, watumishi wa umma hutakiwa kustaafu kwa hiari wakiwa na umri wa miaka 55, na
watimizapo miaka 60 hutakiwa kustaafu kwa lazima. Hata hivyo, baadhi yao
wamekuwa wakipewa mikataba ya kuendelea na kazi hata baada ya kutimiza umri wa
kustaafu kwa lazima.
Mheshimiwa Spika,
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni haipingi kumwajiri mstaafu kwa mkataba kama
mstaafu huyo ndiye pekee mwenye ujuzi na uzoefu wa kazi anayotakiwa kufanya. Ila kuna baadhi ya watumishi
waliotimiza umri wa kustaafu kwa lazima, wakapewa mikataba ya kuendelea na
utumishi Serikalini, bila kuwa na sifa iliyotajwa. Kambi Rasmi ya Upinzani
ilitegemea kwamba, Serikali ingeajiri watumishi wengine kushika nafasi hizo
baada ya mikataba hiyo kumaliza muda wake hasa ukizingatia tatizo kubwa la
ajira linalowakumba vijana katika nchi yetu. Serikali ya CCM imeendelea
kuwaacha wastaafu hao kuendelea na utumishi bila hata kutoa mikataba mipya
baada ya ile ya mwanzo kumalizika.
Mheshimiwa Spika,
Kambi Rasmi ya Upinzani inaomba iwataje baadhi ya wazee waliotimiza umri wa
kustaafu kwa lazima, wakapewa mikataba ya utumishi Serikalini, mikataba hiyo
ikamaliza muda wake, lakini bado wanaendelea na kazi:
1.
Ndugu
John Tendwa – Msajili wa Vyama vya Siasa Tanzania
Mheshimiwa Spika,
Mkataba wa Ajira wa Msajili wa vyama vya Siasa John Tendwa ulimaliza muda wake
tangu Novemba, 2012 lakini bado anaendelea na kazi bila ya mkataba mwingine.
Aidha, alipohojiwa na waandishi wa habari juu ya jambo hili alikiri kuwa ni
kweli mkataba umeisha lakini sababu za yeye kung’ang’ania ofisi alisema iulizwe
mamlaka ya uteuzi wake, yaani Rais. Hata hivyo, Ndugu Tendwa aliwakataza
waandishi wa habari kutoa taarifa hii katika vyombo vya habari kwa alichodai
kuwa ingeleta mgogoro na malumbano makubwa yasiyo na tija.
Mheshimiwa Spika,
Kambi Rasmi ya Upinzani haiamini hata kidogo kwamba John Tendwa ndiye mtu pekee
mwenye sifa za pekee za kuwa Msajili wa vyama vya Siasa miongoni mwa Watanzania.
Hatupendi kusema kuwa ufanisi wake umepungua wala hatupendi pia kusema kwamba
kuendelea kwake kubaki ofisini bila hata ya mkataba ni kutokana na
kujipendekeza kwake kwa Rais na uhodari wake wa kukipendelea chama tawala na
Serikali yake lakini tunapenda kusema
kuwa wapo watu wengine wenye sifa ya kuwa Msajili wa Vyama vya Siasa. Ni
jambo jema kuwapa wengine uzoefu, na ni jambo jema pia kuzingatia sheria na kanuni
zinazoelekeza masuala ya utumishi wa umma.
2.
Mkurugenzi
– Manispaa ya Moshi – Bernadeta Kinabo
Mheshimiwa Spika, Mkurugenzi
Mtendaji wa Manispaa ya Moshi, Bernadeta Kinabo, naye alishastaafu kazi,
akapewa mkataba kuendelea na kazi na mkataba huo uliisha muda wake tangu mwaka
2011, lakini bado yupo ofisini anaendelea na kazi. Kambi Rasmi ya Upinzani
Bungeni inaitaka Serikali itoe majibu, ni kwa nini Halmashauri na Manispaa
ziendeshwe na watumishi wa mkataba wakati kuna watumishi waandamizi katika
Halmashauri na Manispaa hizo ambao wangeweza kufanya kazi hizo?
3.2.
Nafasi na Haki za Walimu katika Sekta ya Utumishi wa Umma
Mheshimiwa Spika, kwa muda mrefu sasa walimu wamekuwa ni kada ya utumishi wa umma
ambayo haitendewi haki na Serikali. Nasema hivi kwa sababu kwa miaka mingi
walimu wamekuwa wakilalamika kuhusu mishahara
duni, lakini pia baadhi yao (wengi kiasi) wamekuwa hawalipwi stahili zao kwa mfano malimbikizo ya mishahara, fedha
za uhamisho, n.k. Mara zote walimu kupitia chama chao wanapolalamika kupata
maslahi yao Serikali imekuwa ikiwajibu kwa jeuri kuwa madai yao hayalipiki na
pia wanapotangaza mgomo halali kama njia ya kuifanya Serikali iwasikilize,
Serikali imekuwa na tabia ya kukimbilia mahakamani kuweka zuio la mgomo huo na
hivyo kuwaacha walimu njia-panda bila kujua la kufanya.
Mheshimiwa Spika, katika hotuba ya bajeti ya Elimu mwaka 2012/2013, Kambi Rasmi ya
Upinzani ilitoa angalizo kwamba Serikali isiwaburuze walimu wasije wakabaki na
kinyongo na kufanya mgomo baridi ambao matokeo yake huwa ni mabaya kuliko mgomo
halisi. Serikali hii ya CCM, kama kawaida yake, iliendelea kuziba masikio, na
matokeo yake tunaona jinsi ambayo elimu ya nchi hii inavyozidi kuporomoka. Kwa
mara ya Kwanza katika historia ya Tanzania, wanafunzi zaidi ya asiliami 60
waliofanya mtihani wa kidato cha nne kidato cha nne 2012 walipata daraja
sifuri. Bila shaka mojawapo ya sababu kubwa za anguko hili ni Serikali kupuuza
madai ya walimu kama Kambi Rasmi ya Upinzani ilivyodokeza mwaka jana.
Mheshimiwa Spika, hukumu ya mahakama juu ya mgomo wa walimu mwaka jana 2012, ni
kwamba Serikali ilitakiwa kukaa na chama cha walimu (CWT) na awepo msuluhishi
katika yao (third party) katika kutafuta ufumbuzi wa madai ya walimu dhidi ya
Serikali. Kwa kuwa mpaka leo hapajakuwepo na kikao cha usuluhishi kati ya
Serikali na Chama cha Walimu, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaliomba Bunge
sasa kama chombo cha uwakilishi lakini pia kama muhimili wa dola unaojitegemea
kuwa msuluhihishi kati ya Serikali na Chama cha Walimu ili haki itendeke kwa
pande zote mbili.
3.3.
Utaratibu
wa Kupima Utendaji Kazi katika Utumishi wa Umma
Mheshimiwa Spika,
mwaka 2004 Serikali ilitoa waraka wa
utumishi namba 2 wa mwaka 2004 kuhusu utekelezaji wa utaratibu na kupima
utendaji kazi wa watumishi kwa uwazi. Lengo na madhumuni ya waraka huu ni
kupima na kuongeza ufanisi kwa watumishi wa umma ili kuleta tija, na hivyo
kustawisha maendeleo ya nchi yetu. Zaidi ya hayo, waraka huu unaondoa utaratibu
wa zamani wa kupima utendaji kwa watumishi.
Mheshimiwa Spika,
Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali iliambie Bunge hili na wananchi wa
Tanzania kwamba ni mafanikio kiasi gani yamepatikana tangu kuanza kwa
utekelezaji wa waraka huu.
4.
MAHUSIANO NA URATIBU
4.1.
Mchakato
wa Katiba Mpya na Mapungufu yake
Mheshimiwa Spika, kwa
mujibu wa Hotuba ya Kiongozi wa Upinzani Bungeni, aliyoitoa kwenye mkutano huu
wa bunge tarehe 11 Aprili, 2013 ni kwamba kulikuwa na makubaliano kati ya
kamati maalum ya CHADEMA na Rais juu ya marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya
Katiba ya 2011. Kwa mujibu wa makubaliano hayo, marekebisho yalitakiwa kufanywa
kwa awamu tatu. Awamu ya kwanza ilifanyika katika Bunge la Februari, 2012.
Aidha, kwa mujibu wa makubaliano hayo, awamu nyingine mbili za marekebisho ya
sheria hiyo ya mabadiliko ya Katiba yalitarajiwa kukamilika kabla ya mwisho wa
mwaka jana, yaani 2012. Mwaka 2012 ulimalizika kabla ya makubaliano hayo
kutimizwa.
Mheshimiwa Spika,
katika hotuba yake ya kuukaribisha mwaka 2013, Rais Kikwete, alipokuwa
akilihutubia taifa kama ulivyo utaratibu wake wa kila mwisho wa mwezi alisema
hivi, nanukuu:
“Katika hotuba yangu ya mwisho wa
mwezi wa Februari, 2012, nilieleza kwamba katika mazungumzo baina ya Serikali
na vyama vya siasa na wadau wengine juu ya marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko
ya Katiba tulikubaliana tushughulikie marekebisho ya Sheria hiyo hatua kwa
hatua. Tulikubaliana kuanza na mambo yanayohusu Tume ya Kuratibu na Kukusanya
Maoni ya Wananchi ili Tume iundwe na ianze kazi. Baada ya hapo tuangalie
vipengele vinavyohusu Bunge Maalum na Kura ya Maoni.
Tulifanya hivyo kuhusu Tume ya
Katiba na sasa tunajiandaa kuanza mazungumzo kuhusu ngwe iliyobaki yaani, Bunge
Maalum na Kura ya Maoni. Kama mazungumzo yatakamilika mapema kunako Januari,
2013 mapendekezo hayo yatafikishwa katika Bunge la Jamhuri ya Muungano katika
kikao cha Februari kwa uamuzi. Vinginevyo itakuwa katika Bunge la Aprili, 2013.
Ndugu Wananchi;
Kuhusu Kura ya Maoni, Sheria ya Mabadiliko ya Katiba
inaelekeza kuwa Kura ya Maoni itatungiwa Sheria yake maalum. Ni matumaini yangu
kuwa matayarisho yake yataanza mapema iwezekanavyo. Nawasihi wananchi wenzangu,
viongozi wa vyama vya siasa na asasi za kijamii tuwe watulivu, tuendelee
kushirikiana katika mchakato huu wa Katiba mpaka tulifikishe jahazi ufukweni
salama kwa mustakabali mwema wa nchi yetu na watu wake”.
Mheshimiwa
Spika, ahadi ya Rais
kwamba Serikali ingeleta awamu zote mbili za marekebisho ya Sheria ya
Mabadiliko ya Katiba kabla ya mwisho wa mwaka 2012 haikutimizwa. Aidha ahadi
nyingine aliyotoa Rais wakati akitoa hotuba ya kuukaribisha mwaka 2013 kwamba
marekebisho hayo yangefanyika katika mwezi Februari 2013 au Aprili 2013 bado haijatekelezwa
na hatuoni dalili ya kufanya hivyo.
Mheshimiwa
Spika, nataka kuweka
kumbukumbu vizuri kwamba, madai ya Kambi Rasmi ya Upinzani kuhusu marekebisho
ya Sheria ya Mabadiliko ya katiba siyo ya kuokoteza. Ni makubaliano halali kati
ya wadau mbalimbali kama vile vyama vya siasa, asasi/mashirika n.k. na Rais.
Kambi Rasmi ya Upinzani inamtaka Rais asimamie ahadi zake, na taifa lina haki
ya kujua nini kilitokea mpaka ahadi hizi kushindwa kutekelezwa.
Mheshimiwa
Spika, jana tarehe
16.04.2013, Waziri Mkuu, wakati akihitimisha hotuba yake alitoa ahadi kuwa “huenda
serikali ikawasilisha Muswada wa Marekebisho ya Sheria hiyo kwenye Bunge hili
la Aprili kama muda ukipatikana kwa ajili ya kusomwa kwa mara ya kwanza”. Kwa
maelezo hayo, ni wazi kuwa Waziri Mkuu hana
hakika na kutekelezeka kwa ahadi ya Rais katika Mkutano wa Bunge wa Kumi.
Mheshimiwa
Spika, Kambi Rasmi
ya Upinzani, kwa kutambua kwamba mambo haya yako chini ya Ofisi ya Rais, tunaitaka serikali itamke mbele ya bunge hili
ni lini marekebisho hayo yatafanyika. Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, inayoongozwa na CHADEMA inarudia tena,
kwamba: haitakuwa tayari kuendelea na mchakato wa katiba mpya endapo marekebisho
ya sheria hiyo hayatafanyika pamoja na utekelezaji wa mambo ambayo tuliyasema
wakati wa hotuba ya Waziri Mkuu.
4.2.
Tume
ya Mipango na Majukumu yake
Mheshimiwa
Spika,
jukumu kubwa la Tume ya Mipango, pamoja na mambo mengine, ni kuratibu
utekelezwaji wa Mpango wa Taifa wa Maendeleo. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni
haina mgogoro na utendaji kazi wa tume hii, ila inashangazwa na uundaji wa
chombo kingine chini ya Ofisi ya Rais ambacho kimsingi kazi zake zingepaswa
kufanywa na Tume ya Mipango.
Mheshimiwa Spika, Waziri Mkuu, katika hotuba yake ya bajeti alisema kwamba: “Serikali imeona ni muhimu kuongeza
kasi ya utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo kwa kuanzisha mfumo imara zaidi wa
kupanga vipaumbele, kufuatilia na kutathimini utekelezaji wa miradi ya kimkakati
ya maendeleo. Mfumo huo ambao utasimamiwa na Chombo maalum (President’s
Delivery Bureau) chini ya ofisi ya Rais, Ikulu, unazingatia uzoefu wa nchi ya Malaysia”.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inayoongozwa na CHADEMA inatambua kwamba Serikali imeuchukua mpango huu kutoka Malaysia, kutokana na mkutano wa kimataifa wa 'Langkwi' uliofanyika mwezi Juni 2011 ambao Rais Jakaya Kikwete alishiriki kwenye “mkutano wa tafakuri” 'Putrajaya' ambapo Waziri Mkuu wa Malaysia Mhe. Dato' Razak aliuelezea mpango huu kuwa ulileta mabadiliko ya kiuchumi katika nchi yake. Katika mkutano huo wa tafakuri, Waziri Mkuu wa Malysia alisema kwamba mafanikio ya mpango huo ulitokana na misingi ifuatayo:
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inayoongozwa na CHADEMA inatambua kwamba Serikali imeuchukua mpango huu kutoka Malaysia, kutokana na mkutano wa kimataifa wa 'Langkwi' uliofanyika mwezi Juni 2011 ambao Rais Jakaya Kikwete alishiriki kwenye “mkutano wa tafakuri” 'Putrajaya' ambapo Waziri Mkuu wa Malaysia Mhe. Dato' Razak aliuelezea mpango huu kuwa ulileta mabadiliko ya kiuchumi katika nchi yake. Katika mkutano huo wa tafakuri, Waziri Mkuu wa Malysia alisema kwamba mafanikio ya mpango huo ulitokana na misingi ifuatayo:
i.
Uongozi shupavu na ulio tayari
kwa mabadiliko ya kuipeleka nchi mbele.
ii.
Kuweka mipango ya kimaendeleo kwa kuzingatia
vipaumbele vya kitaifa
iii.
Nidhamu katika utendaji na
utekelezaji
iv.
Uwajibikaji wa serikali na kuwa tayari kukiri
madhaifu yake.
Mheshimiwa Spika, mpango huu wa kuanzishwa kwa idara hii ambayo inajitegemea kwenye
Ofisi ya Rais tayari umeshaanzishwa kama alivyokiri Waziri Mkuu katika hotuba
yake na kwamba Rais tayari ameshazindua
awamu ya kwanza ya maabara tangu tarehe 22.02.2013,
na vipaumbele ambavyo vimepitishwa ni sita
kama ifuatavyo: Nishati, Uchukuzi,
Kilimo, Elimu, Maji na Ukusanyaji wa Mapato.
Aidha, kwa mwaka huu wa fedha mpango huo umeweka bayana kuwa kwa upande wa Nishati lengo ni kuongeza uzalishaji wa nishati kutoka Megawati 1,438 hadi kufikia Megawati 2,780. Katika usafirishaji kipaumbele ni kufungua korido ya kati kwa kufikia uwezo wa kusafirisha tani milioni 5 ifikapo 2015 na hatimaye tani milioni 8 ifikapo mwaka 2025. Kwa upande wa elimu kipaumbele ni kuboresha elimu ya msingi na sekondari na kuhakikisha kuwa kiwango cha ufaulu kinafikia asilimia 70. Kwenye kilimo mkakati kipaumbele ni kufungua mashamba ya kibiashara wakati upande wa maji ni kuhakikisha kuwa asilimia 67 ya Watanzania wanapata maji safi na salama. Kwa upande wa ukusanyaji wa mapato, lengo ni kuhakikisha kuwa tunaongeza mapato kwa kiwango cha asilimia 50.
Mheshimiwa Spika, Serikali tayari imeshatenga fedha kwenye bajeti ya mwaka huu wa 2013/2014 kiasi cha shilingi bilioni 8 na imeomba fedha kutoka kwa wafadhili wa nje kiasi cha shilingi bilioni 30 kwa ajili ya kitengo hiki kipya chini ya Ofisi ya Rais Ikulu. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inayoongozwa na CHADEMA inaitaka Serikali kutoa majibu kwa Watanzania juu ya mambo yafuatayo:
Aidha, kwa mwaka huu wa fedha mpango huo umeweka bayana kuwa kwa upande wa Nishati lengo ni kuongeza uzalishaji wa nishati kutoka Megawati 1,438 hadi kufikia Megawati 2,780. Katika usafirishaji kipaumbele ni kufungua korido ya kati kwa kufikia uwezo wa kusafirisha tani milioni 5 ifikapo 2015 na hatimaye tani milioni 8 ifikapo mwaka 2025. Kwa upande wa elimu kipaumbele ni kuboresha elimu ya msingi na sekondari na kuhakikisha kuwa kiwango cha ufaulu kinafikia asilimia 70. Kwenye kilimo mkakati kipaumbele ni kufungua mashamba ya kibiashara wakati upande wa maji ni kuhakikisha kuwa asilimia 67 ya Watanzania wanapata maji safi na salama. Kwa upande wa ukusanyaji wa mapato, lengo ni kuhakikisha kuwa tunaongeza mapato kwa kiwango cha asilimia 50.
Mheshimiwa Spika, Serikali tayari imeshatenga fedha kwenye bajeti ya mwaka huu wa 2013/2014 kiasi cha shilingi bilioni 8 na imeomba fedha kutoka kwa wafadhili wa nje kiasi cha shilingi bilioni 30 kwa ajili ya kitengo hiki kipya chini ya Ofisi ya Rais Ikulu. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inayoongozwa na CHADEMA inaitaka Serikali kutoa majibu kwa Watanzania juu ya mambo yafuatayo:
i.
Je, vipaumbele vya Mpango wa
Taifa wa Maendeleo wa miaka mitano uliopitishwa na Bunge hili mwaka 2011 ndio
vimeachwa au vitatekelezwa sambamba na vipaumbele hivi vipya?
ii.
Je, Kwa nini Serikali imeanzisha
kitengo kipya cha Performance Management and Delivery Unit (PEMANDU) (Kitengo
cha Usimamizi na Ufanisi wa Utendaji) chini ya Ofisi ya Rais wakati kuna Tume
ya Mipango ambayo kimsingi ndiyo yenye wajibu wa kusimamia vipaumbele vya Taifa
na Mpango mzima wa Maendeleo wa Taifa?
iii.
Je, ikitokea tena, Rais
akakaribishwa kwenye “mkutano mwingine wa tafakuri” kama uliofanywa na kiongozi
wa Malaysia, na kukuta mipango mizuri zaidi, Serikali italazimika tena kupanga
upya vipaumbele vya Taifa na Mpango wa utekelezaji kama inavyofanya sasa?
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inayoongozwa na CHADEMA, ni mdau mkubwa wa
maendeleo na inauheshimu mpango wa Taifa wa Maendeleo lakini namna Serikali
inavyotekeleza Mpango huo hatuna hakika kama malengo ya Mpango huu yatafikiwa.
Kambi Rasmi ya Upinzani haioni sababu yoyote ya msingi ya kuanzisha kitengo
kipya cha usimamizi wa mpango wa maendeleo wakati Tume ya Mipango ipo.
Kinachoonekana dhahiri ni kwamba Serikali hii ya CCM kila kukicha inatafuta
mbinu mbalimbali za kutumia fedha za walipa kodi wa Tanzania bila kujali sana
matatizo ya Watanzania. Nasema hivi kwa sababu kitengo hiki kipya
kilichoanzishwa bila sababu ya msingi, hivi punde kitaanza nacho kuomba
mabilioni ya fedha kwa ajili ya uendeshaji wake wakati tayari kuna Tume ya
Mipango ambayo ndio mratibu na msimamizi wa Mpango wa Maendeleo.
4.3.
MAHUSIANO
YA MADHEHEBU YA DINI NA SERIKALI
Mheshimiwa Spika, Kiongozi
wa Kambi Rasmi Bungeni alieleza vizuri tatizo la udini katika hotuba yake
aliyoitoa hapa Bungeni tarehe 11 Aprili, 2013. Hapa itatosha tu kusema kuwa
katika miaka ya hivi karibuni, kumekuwepo matukio ambayo yanaashiria udini.
Baadhi ya matukio hayo ni:
·
Kushambuliwa kwa viongozi wa dini, na
wengine kuuawa
·
Kuchomwa moto nyumba za ibada
·
Mgogoro wa nani achinje
Yapo
matukio mengine; na haya yote yamesababisha taharuki, vilio, na utovu wa amani
na usalama miongoni mwa wananchi walioguswa na matukio haya.
Mheshimiwa Spika, wakati
watu wakizidi kuathirika na matukio yanayoashiria udini, serikali haijachukua
hatua kali kukomesha matukio hayo.
Mheshimiwa
Spika, kitendo cha
Serikali kushindwa kukemea au kusuluhisha kwa haraka migogoro wa kiimani
uliotokea hapa nchini, umesababisha kutolewa kwa matamko makali na madhehebu ya
dini ambayo kimsingi yanaonesha jinsi mahusiano kati ya Serikali na taasisi za
dini yanavyozidi kudorora.
Mheshimiwa
Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani
Bungeni inaamini kuwa kati ya migogoro yote ya kijamii hakuna mgogoro mkubwa na
tete kama ule wa kiimani, kwani mgogoro huo hauna itikadi za kisiasa na kwa
maana hiyo athari zitakazotokana na mgogoro wa kidini unaathiri jamii nzima. Ni
jukumu la Serikali kuwaeleza Watanzania ni hatua gani za maksudi zinachukuliwa
katika kutatua mgogoro huo unaoelekea kusambaratisha amani na mshikamano wa
Taifa letu?
Mheshimiwa
Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani
Bungeni
inaishauri Serikali yetu na vyombo vyake vya usalama, sheria na amani kuchukua
hatua mara moja bila kuchelewa dhidi ya watu au vikundi vyovyote vinapoanza
uchochezi wa kidini. Tabia ya kuachia uchochezi wa kidini kuendelea pasipo
hatua madhubuti kuchukuliwa ni udhaifu mkubwa wa uongozi na uwajibikaji wa
Serikali ambayo jukumu lake la kwanza ni kulinda usalama wa nchi na watu wake.
5.
MASUALA
MENGINE
5.1. Utawala Bora Ngazi za Halimashauri,
Kata na Vijiji
Mheshimiwa Spika, kwa muda mrefu sasa dhana ya
utawala bora imekuwa ikionekana kuwa inapaswa kutekelezwa kwenye ngazi ya
serikali kuu. Katika ngazi ya serikali za mitaa utawala bora kwa jumla umeachwa
bila kuwekewa msisistizo. Ni muhimu serikali ihakikishe kuwa utawala bora unakuwa
ni sehemu ya utendaji wa kila siku kwenye ngazi zote – kitongoji, kijiji, kata,
wilaya na mkoa. Ni muhimu Serikali ihakikishe kuwa waliopewa wajibu wa
kusimamia hilo wanatimiza wajibu wao kikamilifu.
Mheshimiwa Spika, hali ya utawala bora imezorota sana
kwenye ngazi ya serikali za mitaa, na hasa ikizingatiwa kuwa Wakuu wa Wilaya na
Mikoa mbalimbali nchini wamekuwa na utamaduni wa kuingilia maamuzi mbalimbali
yanayofanywa na vikao halali vya Halimashauri za Manispaa na Wilaya. Sasa hivi Wakuu wa Wilaya na Mikoa wamekuwa wakiingilia na hata kushurutisha
maamuzi mbalimbali na hivyo kukwamisha
utekelezaji wa maamuzi yanayofanywa na vikao hivyo na kuathiri utendaji kazi wa
Halimashauri hizo.
Mheshimiwa Spika, tabia ya kutokuheshimu utawala bora
kwenye ngazi ya Halimashauri umekua na kusambaa mpaka kwenye ngazi za Kata na
Vijiji kwani sasa watendaji wa vijiji na Kata wamejigeuza na kuwa wao ni
Polisi, Mahakama na Magereza. Viongozi hawa wamekuwa wakiwanyanyasa sana wananchi kwa kuwakamata, kuwahukumu
na hata kuanzisha magereza kama ambavyo wengi wanavyoweza kushuhudia kuwa yapo
baadhi ya maghala ya mazao ambayo sasa yamekuwa ndio mahabusu kwa wananchi wa
vijijini.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya
Upinzani Bungeni inaitaka
Serikali kutoa majibu ya kina kuhusiana na suala la utawala bora kwenye ngazi za
Halimashauri, kata na vijiji. Ni hatua gani Serikali imewachukulia viongozi wa
Halmashauri, Kata na Vijiji wanaowanyanyasa wananchi kutokana na itikadi zao za
siasa na sababu nyingine? Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani inauliza: Wananchi wachukue
hatua gani ili kuukomesha uonevu wa aina hiyo pindi unapotokea ?
5.2.
Ukosefu
wa Ajira na Ongezeko la Umasikini kwa Wananchi
Mheshimiwa Spika, kwa
mujibu wa jarida la “The African Executive” toleo Na. 415 la tarehe 3-10
Aprili, 2013, ni kwamba: tatizo kubwa kabisa la binadamu kwa siku hizi ni
umasikini. Ili kuondokana na umasikini huo, hitaji la msingi kabisa ni kupata
kipato kizuri ambacho chanzo chake
kikubwa ni ajira. Kwa hiyo njia madhubuti ya kupambana na kutokomeza
umasikini ni kutengeneza nafasi nyingi za ajira iwezekanavyo na kuwapatia watu
ujuzi na utaalamu ili kujaza nafasi hizo.
Mheshimiwa Spika,
jarida hilo linaelezea pia kwamba, kutengeneza nafasi za ajira bila kuwajengea
wananchi ujuzi na utaalamu wa kufanya kazi hizo ni kazi bure kwa kuwa kazi hizo
zitafanywa na wataalam kutoka nje na hivyo kutowanufaisha wananchi wetu. Kwa
hiyo kama Serikali inawapa watu wake elimu bora na kuwajengea watu wake ujuzi
na utaalamu na kama Serikali inaweka
mazingira mazuri ambayo watu wanaweza kufanya biashara na kupata fedha, basi
watu hao watajinufaisha wenyewe, watawanufaisha wengine na wanaweza kuisaidia
Serikali kuondokana na umasikini. Hivyo uwezo wa watu kupata ajira na kipato
unategemea sana jitihada za Serikali.
Mheshimiwa Spika,
tatizo la ukosefu wa ajira hapa nchini linazidi kuwa kubwa na Serikali ya CCM
imeshindwa kabisa kutatua tatizo hili. Tangu mwaka 2005 Rais kikwete aliwaahidi
Watanzania Maisha Bora kupitia kaulimbiu yake ya “Maisha Bora kwa Kila
Mtanzania”. Hiki ni kipindi cha pili cha
utawala wake na maisha ya Mtanzania yanazidi kusinyaa, umasikini unazidi
kuongezeka, na tatizo la ajira linazidi kuongezeka.
Mheshimiwa Spika, pamoja
Serikali hii ya CCM kushindwa kutoa ajira za kutosha tofauti na ilivyoahidi
bado imekuwa ikiwakejeli wananchi kuwa eti hata kufungua visoda ni kazi.
5.3
Kufukuzwa
Kazi kwa Kuonewa
Mheshimiwa Spika, baadhi
ya waajiri wa serikali wamekuwa wakinyanyasa na kuwanyanyapaa watumishi wa umma
kutokana na itikadi za kisiasa. Unyanyapaa huu umechukua sura mpya kiasi
ambacho mtumishi anapotoa mawazo mazuri ambayo ni ya kukosoa mfumo wa
uendeshaji wa taasisi ya umma ili ufanye kazi vizuri zaidi anaitwa kuwa ni
pandikizi la CHADEMA. Jambo hili linawavunja moyo watumishi wa umma kufanya
kazi kwa ufanisi kwa kuogopa kuitwa ni wapinzani na matokeo yake utendaji
katika sekta ya umma unazidi kudorora.
Mheshimiwa Spika,
katika hali ya kusikitisha, Ndugu Emmanuel V. Gwalanje, ambaye ni Afisa Mifugo
Msaidizi daraja la II katika Halmashauri ya Mufindi, alifukuzwa kazi kwa mashtaka dhidi yake kwamba anajihusisha na
masuala ya siasa wakati wa kazi. Katika utetezi wake, Emmanuel V. Gwalanje
alieleza bayana kuwa hajawahi kujihusisha na mambo ya siasa akiwa kazini na wafanyakazi
wenzake ni mashahidi; pia rekodi yake ya mahudhurio kazini ni nzuri lakini
amesingiziwa hivyo kwa kuwa alihudhuria mkutano wa siasa baada ya saa za kazi.
Mheshimiwa Spika, mchakato
wa kumfukuza Ndugu Emmanuel V. Gwalanje ulikuwa mfupi sana. Notisi ya Mashitaka
iliandikwa tarehe 18.03.2013, utetezi uliwasilishwa tarehe 21.03.2013, barua ya
kufukuzwa kazi tarehe ilitoka tarehe 28.03.2013. Kambi Rasmi ya Upinzani
inashawishika kuamini kwamba uamuzi wa kumfukuza kazi Emanuel Gwalanje haukuwa
wa haki ikizingatiwa kwamba hakuwahi kupewa onyo hata moja kama kweli alikuwa
akijihusisha na kazi ya siasa wakati wa kazi. Aidha, muda mfupi wa mchakato wa
kufukuzwa kwake unatia shaka kama kuna uchunguzi wa kina uliofanyika kubaini bila shaka yoyote kuwa Emmanuel
Gwalanje kweli alihusika na kazi ya siasa wakati wa saa za kazi.
Mheshimiwa Spika,
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inayoongozwa na CHADEMA inamtaka Kaimu
Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Mufindi, E. Kaduma, pamoja na Afisa wake wa
Mamlaka ya Nidhamu kuwasilisha mchakato na hukumu ya mashitaka dhidi ya
Emmanuel Gwalanje kwa Waziri wa Utumishi wa Umma ili kubaini uhalali wa
mchakato mzima.
Mheshimiwa Spika,
nimetolea mfano shauri la Emmanuel Gwalanje wa halmashauri ya Mufindi, lakini
yapo matukio mengi ya watumishi wanaofukuzwa kazi kiholela katika halmashauri
na taasisi za Serikali kutokana na chuki binafsi na unyanyapaa wa kisiasa.
Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kukemea tabia hii.
5.4
Huduma
kwa Watumishi wa Umma wanaoishi na VVU
Mheshimiwa Spika, mwaka 2006 Serikali ilitoa Waraka wa utumishi wa umma namba 2 wa
mwaka 2006 kuhusu huduma za watumishi wa umma wanaoishi na virusi vya ukimwi.
Chini ya waraka huu waajiri wa watumishi wa umma wanapaswa kuhamasisha
watumishi kupima VVU, na kutoa huduma muhimu kwa wale watakaokuwa wameathirika.
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali itoe taarifa katika bunge
hili kuwa ni kwa kiwango gani waraka huu
umetekelezwa na ni gharama kiasi gani
imetumika mpaka sasa katika kuwahudumia watumishi wa umma wanaoishi na VVU kwa
maana ya lishe broa, madawa, nauli za kuhudhuria matibabu na stahili nyingine?
________________________________________________
PROF.
KULIKOYELA KANALWANDA KAHIGI (MB)
MSEMAJI
MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI
OFISI
YA RAIS -
MENEJIMENTI
YA UTUMISHI WA UMMA, UTAWALA BORA NA
MAHUSIANO
NA URATIBU
17
APRILI, 2013
KAMA KUNATUME YA MIPANGO AMBAYO IPO KISHERIA KUNA AJA GANI YA KUUNDA TUME NYINGINE YA MIPANGO, INAMAANA HIYO YA MWANZO HATUHIAMINI BASI KAMA HATUHIAMINI BASI TUIVUNJE,KWANI HAKUNA SABABU YA KUWA NA TUME MBILI ZOTE ZINAFANYA KAZI MOJA, KUHUSU SWALA LA ELIMU TUSILIPUUZE KABISA KWANI KIWANGO CHA UFAURU NI KIDOGO HAIJAWAHI KUTOKEA KABISA KWA NCHI YETU, WAALIMU WASILILIZWE NA MADAI YAO YAFANYIWE KAZI HARAKA,VINGINEVYO KIHAMA KINAKUJA CHA KUFERI WANAFUNZI ITAKUWA MARA MBILI YA 65%,WAALIMU HAO WANAONEKANA WANAKINYONGO, CHADEMA NAOMBA MFATILIE MIKATABA YA GESI ILI NA SISI WANANCHI TUFAHAMU KUHUSU GESI YETU, CHADEMA BILA NYINYI WANANCHI HAWTAFAMU MIKATABA YA NCHI HII MSICHOKE KUPIGA KELELE ILI WANANCHI WAFAHAMU GESI YAO. (PEOPLE'S POWER)
ReplyDelete