Mahakama ya Rufaa Tanzania, leo imefanya mapitio ya hukumu ya mahakama hiyo iliyomrejeshea ubunge, Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (CHADEMA) na kutupilia mbali rufani iliyowasilishwa na makada watatu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kuomba ifanye hivyo kutokana na kutoridhishwa na hukumu hiyo.
Mbali na kutupilia mbali maombi hayo majaji watatu waliosikiliza rufaa hiyo, Engili Kileo, Salum Massati na Bernard Luanda walitamka kuwa Lema ni Mbunge halali wa Arusha Mjini na kuamuru kwa mara nyingine, wakata rufaa walipe gharama zote za kesi hiyo.
Makada hao, waliwasilisha maombi hayo Februari 13, mwaka huu, chini ya hati ya dharura wakiomba yasikilizwe mapema.
Jopo la majaji watatu wa Mahakama ya Rufani, watakaokaa kufanya mapitio hayo ni Jaji Nathalia Kimaro, Jaji Salum Massati na Jaji Bernard Luanda.
Wanachama hao ambao ni Mussa Mkanga, Happy Kivuyo na Agnes Mollel, walifungua kesi dhidi ya Lema katika Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, kupinga ushindi wake alioupata katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010.
Walidai katika kampeni zake mwaka 2010, Lema alikuwa akitumia lugha za matusi, kejeli na ubaguzi wa kijinsia dhidi ya aliyekuwa mgombea wa CCM, Dk. Batilda Buriani.
Makada hao, waliwasilisha maombi ya mapitio ya rufani ambayo Mahakama ya Rufani, ilimrejesha bungeni Lema ikiwa ni miezi tisa tangu alipovuliwa wadhifa huo na Mahakama Kuu, Kanda ya Arusha.
Mahakama hiyo ilimrejesha Lema bungeni, baada ya kushinda rufani yake ya kupinga hukumu ya Mahakama Kuu ya Arusha iliyotolewa Aprili 5, mwaka jana.
Hukumu hiyo iliyomrejesha bungeni, Lema ilisomwa na Naibu Msajili wa Mahakama ya Rufani, Elizabeth Mkwizu ambapo mahakama hiyo ilitamka kwamba imemtambua Lema kuwa mbunge halali wa Arusha Mjini na kuwaamuru wajibu rufani kumlipa gharama za rufaa hiyo.
No comments:
Post a Comment