Saturday, April 20, 2013

Kero nzito za Muungano zaibuka Bungeni


Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni, imeibua kero nzito dhidi ya Muungano zinazohusu majimbo madogo ya Zanzibar kupewa mafungu mawili ya mfuko wa jimbo wakati ya Tanzania bara yakibakiwa na fungu moja.
 
Nyingine ni Watanganyika kunyimwa haki ya kumiki ardhi visiwani na Wazanzibari kujazana kwenye Bunge la Muungano wakati Watanganyika hawaruhusiwi kuingia kwenye Baraza la Wawakilishi.
 
Kambi hiyo imepinga kuyapatia majimbo ya uchaguzi ya Zanzibar fedha za ruzuku za mfuko wa maendeleo ya jimbo zinazotolewa na Serikali ya Muungano Tanzania pamoja na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ).
 
 Maoni ya Msemaji  Mkuu wa Kambi ya Upinzani Ofisi ya Makamu wa Rais, yaliyosomwa na David Silinde (Chadema- Mbozi Magharibi), yalisema:
 
“Katika kurekebisha hali ya utata iliyojitokeza kwenye majimbo ya Zanzibar,  SMZ imeamua kuanzisha mfuko wa maendeleo wa jimbo kwa  wajumbe wa baraza hilo na kufanya hoja hii kuhitaji kupatiwa ufumbuzi.”
 
Iliongeza: “Hii ni kwa sababu sasa kila jimbo la uchaguzi la Zanzibar litapata mafungu mawili ya fedha za mfuko wa maendeleo ya jimbo , wakati majimbo ya Tanzania Bara  yakipata fungu moja.”
 
Silinde alisema majimbo hayo madogo na yenye idadi ndogo ya watu sasa yatapata fedha za mfuko wa maendeleo ya jimbo kutoka Serikali ya Muungano na ya Mapinduzi  Zanzibar wakati majimbo ya Bara makubwa na yenye watu wengi yakipata fedha kutoka chanzo kimoja.
 
Kambi hiyo iliitaka serikali ilieleze Bunge  kama ni halali kwa fedha za umma kuendelea kutoa ruzuku mifuko ya maendeleo ya majimbo  ya Zanzibar  wakati sasa  itakuwa inapata  fedha kutoka  Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

UBAGUZI DHIDI YA WATANGANYIKA
Upinzani ulisema Watanganyika wanakerwa na ubaguzi unaoendeshwa dhidi yao na Zanzibar ukitaja umiliki wa ardhi  ambao Wabara wanaoishi na kufanya kazi Visiwani hawaruhusiwi kumiliki ardhi visiwani wakati Wazanzibari walioko Bara wana haki ya kumiliki ardhi.
 
Hili linaacha ladha mbaya katika mahusiano ya wananchi wa pande hizo kwani inaonekana kuwa Wazanzibari wanapendelewa na Watanganyika wanabaguliwa.
 
UWAKILISHI USIO WA UWIANO
Kambi ya Upinzani ililalamikia uwakilishi usio na uwiano wa wabunge wa Zanzibar katika Bunge la Jamhuri ya Muungano.
 
“Hivyo basi wakati Bunge la sasa mbunge mmoja anawakilisha watu 157,000, mbunge mmoja wa Zanzibar anawakilisha wastani wa watu 16,000.”
 
Maoni ya upinzani yalieleza kuwa  katika Bunge la sasa kuna Wazanzibari 83 kati ya wabunge wote 357 .
 
Upinzani ulisema kinachodhihirika leo ni kauli  ya Mwanasheria Mkuu wa kwanza wa Zanzibar Wolfgang Dourado, alichosema  akimnukuu Rais wa kwanza wa Zanzibar, hayati Abeid Amani Karume akisema,  “msiwe na wasiwasi sisi tuna haki ya kuwakilishwa katika Bunge lao lakini wao hawana haki ya kuwa kwenye Baraza letu la Mapinduzi.”   
 
 CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment