CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA kimesema kimeanza mkakati kuhakikisha kinakuwa na mabalozi wa nyumba kumi kwa kila eneo. Hatua hiyo ni katika kukiimarisha chama hicho kuanzia ngazi ya taifa hadi kitongoji .
Katibu Mkuu wa Chama hicho, Dk Wilbrod Slaa alisema hatua hiyo imeanza kwa kutoa mafunzo kwa viongozi wa ngazi ya taifa ya chama hicho.
Alikuwa akifungua mafunzo ya kuwajengea uwezo viongozi wa taifa waweze kwenda kutoa mafunzo ngazi ya kanda ambao nao wataendelea kutoa elimu hiyo kwenye jimbo kata hadi vijiji.
Lengo la chama hicho ni kuhakikisha kinajiimarisha na kuwa na viongozi wenye kufuata maadili na misingi ya chama na kujiandaa kushika dola kwa kuwa na uongozi wenye weledi wa hali ya juu, alisema.
“Sisi hatutaki mwanachama anunue shashada ya kura, tunajiandaa tunapeleka silaha ya kujiandaa kushika dola na ndiyo maana tunawaandaa kuhakikisha tunaposhika dola, tunakuwa tayari na viongozi wenye weledi mkubwa,” alisema Dk. Slaa.
Dk. Slaa aliwashangaa watu wanaodai kuwa M4C imekufa.
Alisema watu hao hawajui kuwa Chadema imejipanga na ina mbinu za utawala ambazo hazina hila kama baadhi ya vyama vingine vinavyofanya.
“ Navishangaa vyama vingine vinasifika kwa hila badala ya kuijenga Tanzania na wananchi wake… serikali za mitaa hadi wilaya ni wizi mtupu sisi tunatengeneza wataalamu wenye uchungu wa kulinda rasilimali zao,” alisema.
Mkurugenzi wa Oganaizesheni wa chama hicho, Benson Kigaula alisema inategemewa watafundishwa wakufunzi 30,606 ambao watavifikia vitongoji vyote nchini.
Alisema hadi Oktoba mwaka huu vijiji 18,000 vitakuwa vimefikiwa na kupewa walimu na wakufunzi hao.
No comments:
Post a Comment