CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kupitia kampeni ya Movement for Change (M4C), Kanda ya Ziwa, kimeandaa karamu ya chakula cha usiku kwa wadau, wanaharakati, wapenzi wa chadema na wananchi wapenda maendeleo, kwa lengo la kupata michango ya fedha zitakazowasaidia viongozi wa chama hicho vijijini.
Taarifa iliyotolewa na kiongozi wa M4C Kanda ya Ziwa, 'Kamanda' Alfonce Mawazo ilisema hafla hiyo itafanyika Aprili 28, mwaka huu jijini hapa na itahudhuriwa na wabunge mbalimbali wa Chadema hicho.
"Tunatarajia kupata wageni kutoka mikoa ya Kagera, Mara, Geita, Simiyu, Mwanza na Shinyanga ambao wote hawa ni kutoka kanda ya ziwa…fedha tutakazokusanya zitatumika kwa ajili ya kuleta ukombozi kwa wananchi wa Tanzania kwa kuiondoa madarakani CCM mwaka 2015," alisema Mawazo.
"Kwa hiyo, tunawaomba wadau, wanaharakati, wananchi, wana CCM, wapenzi na mashabiki wa CHADEMA na wapenda maendeleo wote waje tushiriki pamoja kufanikisha safari ya Chadema kuingia madarakani 2015", alisema Mawazo.
Alisema CHADEMA imeandaa kadi maalumu kwa watu wote wanaohitaji kushiriki hafla hiyo, pia alitoa wito kwa wananchi kuwasiliana na viongozi wa Chadema, ili wapate kadi hizo kwa ajili ya kushiriki kwenye hafla hiyo.
Kuhusu mafanikio ya M4C Kanda ya Ziwa, aliwapongeza viongozi na wanachama wa CHADEMA, kwa mshikamano mzuri wa kuongoza harakati za mageuzi katika kanda hiyo.
No comments:
Post a Comment