Monday, April 15, 2013

Bumbuli waanza kuikimbia CCM


KADA wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Shaban Omari Shemzize, amekihama chama hicho na kujiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).
Shemzize ambaye pia alikuwa Kamanda wa Vijana wa CCM Kata ya Baga, iliyopo Jimbo la Bumbuli, alikabidhiwa kadi ya CHADEMA  jana na Mratibu wa  kampeni wa chama hicho Mkoa wa Tanga, Jonathan Bahweje.
CCM ilianza kupata pigo siku chache zilizopita baada ya CHADEMA kuibuka mshindi katika uchaguzi wa Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Kwekitui ambapo chama hicho kilikuwa ngome yake.
Shemzize alisema ameamua kukihama chama hicho kutokana na kushindwa kubeba mzigo mzito usiokuwa na mwisho mwema, zaidi ya kupata lawama.
Alisema ameamua kuachia nafasi zote ndani ya CCM baada ya msimamizi wa uchaguzi huo, Erick Muhumbo kutangaza matokeo yaliyoipa ushindi CHADEMA.
Katika kinyang’anyiro hicho ambacho awali CCM iligomea matokeo na kulazimika uchaguzi kurudiwa, mgombea wa CHADEMA Miraji Mussa aliibuka mshindi dhidi ya mgombea wa CCM, Ally Nyangasa.
Aidha, Shemzize alidai kuchoshwa na pengo kubwa lililopo baina ya CCM na wananchi hasa walalahoi licha ya kuwa ndiyo wanaotunisha misuli ya kukibeba kwenye chaguzi zote.

No comments:

Post a Comment