Monday, April 15, 2013

Mbowe afichua ‘njama’ Tume ya Uchaguzi


Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imeishutumu Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kufanya mkakati wa siri wa kuandaa utambuzi wa wapigakura kwa kutumia mfumo uitwao ‘biometric’ ulioshindwa Kenya na Zimbabwe.
Hayo yalibainishwa juzi na Kiongozi wa Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe wakati akitoa maoni ya kambi hiyo kuhusu Hotuba ya Bajeti ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.
Alisema, “Kwa mujibu wa taarifa tulizo nazo, tayari Tume ya Taifa ya Uchaguzi imeshaanza maandalizi mengi ya msingi bila hata vyama vya siasa kujua... mchakato huu unaofanywa kwa siri kubwa na unaokisiwa kutumia zaidi ya Dola za Marekani 200 milioni tayari umeanza kutafutiwa fedha.”
Alisema teknolojia hiyo kwa siku za karibuni imetumika katika chaguzi nchini Ghana na Kenya na kote huko ilishindwa na chupuchupu ingeyaingiza mataifa hayo katika vurugu kubwa za uchaguzi.
Mbowe alisema mataifa hayo yalilazimika kurudia mfumo wa upigaji na uhesabuji kura kwa njia ya kawaida, hali iliyosababisha hofu kubwa.
Hata hivyo, Mbowe  alisema pamoja na kambi rasmi kuafiki  matumizi ya teknolojia mpya kurahisisha na kuboresha mfumo mzima wa uchaguzi, inatambua athari kubwa zinazoweza kutokea iwapo zoezi hilo halitafanywa katika misingi ya uwazi na ushirikishwaji wadau muhimu kama vyama vya siasa.
“Ni kwa sababu hizi basi, tunaitaka Serikali kutoa maelezo ya kina kuwa ni sheria gani iliyotungwa na bunge inayoruhusu uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura kwa mfumo huu na  ni bajeti ipi inatumika kutekeleza mpango huo? Ni kwa nini mpango huo unafanyika kwa siri,” alihoji.
Mbowe ambaye pia ni mwenyekiti wa Chadema, alisema kuwa Serikali haioneshi dhamira ya dhati ya kusukuma mchakato wa kuleta marekebisho ya Sheria ya Uchaguzi ili kuondoa ukomo wa kuboresha Daftari la Kudumu la Wapigakura (wa mara mbili kwa kipindi cha miaka mitano) ili daftari hilo liwe huru wakati wote kuandikisha wapigakura wapya.
Alisema kwa sasa utaratibu wa kurekebisha au kuboresha yaliyomo katika daftari hilo hauendi sawia na haki ya raia kupiga kura na  mahitaji makubwa ya kukuza demokrasia katika chaguzi hapa nchini.
Mfumo wa ‘biometric’ hutumika kumtambua mpigakura kwa alama za mwili kama alama za vidole na au mboni ya jicho.
Mwananchi

No comments:

Post a Comment