ASEMA CHADEMA NI IMARA KULIKO SERIKALI YA CCM
KATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willbrod Slaa amesema kuwa uchochezi unaofanywa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) dhidi yao umewapa mori na hari ya kwenda kuchukua dola mwaka 2015.
Alisema fitna zinazofanywa na Serikali ya CCM dhidi ya CHADEMA zinatokana na ujumbe mzito kutoka kwa wananchi, hasa katika uitikiaji wa matukio mbalimbali.
Dk. Slaa alitoa kauli hiyo jana jijini Dar es Salaam wakati wa kumkaribisha Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, Freeman Mbowe kufungua kikao cha Kamati ya Uzinduzi wa Kanda ya Pwani utakaofanyika leo mjini Kibaha.
Alisema kuwa kwa sasa wana taarifa zote za kutosha kuonesha kwamba CCM ni chama cha kigaidi, ambao chimbuko lake ni serikali yenyewe.
Dk. Slaa alisema kuwa CCM inafanya propaganda na porojo ikiwa ni pamoja na kuwabambika tuhuma za ugaidi wafuasi wa CHADEMA, akiwemo Mkurugenzi wao wa Ulinzi na Usalama, Wilfred Lwakatare ambaye anakabiliwa na kesi.
“Tunafurahi sasa hivi wanapotuchokoza kwa uendawazimu wao, propaganda na porojo zao, sisi tunakwenda mbele kuchukua dola. Hiki ndicho kichocheo kikubwa cha kutupa mori na ari.
Alifafanua kuwa baada ya Mbowe kutoa hotuba yake bungeni na kugusia suala la ugaidi, wale wanaojihusisha na vitendo hivyo wamejionesha.
“Jana magaidi wamejionesha bungeni. Lakini tuko imara kuliko Serikali ya CCM, tuko imara kuliko hata Usalama wa Taifa na tuko imara kuliko hata CCM yenyewe,” alisisitiza.
Dk. Slaa aliongeza kuwa umakini huo ndio utawapeleka Ikulu na si kutegemea nguvu ya vyombo vya dola kama CCM wanavyotaka.
Alifafanua kuwa kwa sasa wana taarifa zote za kutosha za kuonesha jinsi Serikali ya CCM inavyowarubuni baadhi ya maofisa wa CHADEMA kwenda kutunga kesi ya Lwakatare.
“Na serikali yenyewe ndiyo chimbuko la ugaidi, wala isingetumia maofisa wangu wa makao makuu kwenda chumba namba 223 kwenye jengo la usalama kutunga kesi dhidi ya Lwakatare,” alisema.
Huku akisisitiza kuwa vitendo hivyo vimewapandisha hasira na ari ya kufanya kazi, Dk. Slaa alisema baada ya mkakati wa Serikali ya CCM kubambikia wapinzani kesi kuelekea kubainika, wameamua kuwatumia watu wa usalama kutengeneza ushahidi wa uongo.
Alisema kuwa kauli ya Mbowe bungeni imetingisha baadhi ya watu ambapo watenda uhalifu wametikisika na sasa wanaanza kuonekana bungeni wakijitetea.
Bonyeza Read More kuendelea
Mbowe afyatuka
Akifungua kikao hicho, Mbowe alisema Rais Jakaya Kikwete asitafute mchawi katika suala zima la chokochoko za udini unaoanza kumea nchini kwa kile alichoeleza suala hilo liliasisiwa Ikulu.
Alisema vikundi vya kidini vimekuwa vikiratibiwa kutoka Ikulu na kupewa fedha za kueneza kauli alizoziita propaganda dhidi ya vyama vya upinzani, huku CHADEMA wakiwa walengwa wakuu.
Alibainisha kuwa ni ajabu kuona mtu anatafuta madaraka kwa kuwatenga Watanzania kwa imani zao, mikoa yao na kanda wanazotoka pasipo kuangalia athari zitakazojitokeza.
“Hakuna haja ya kumung’unya maneno, Kikwete ndiye aliyeasisi hili na vikundi vya kidini vinaratibiwa kutoka Ikulu na fedha wanapewa. Kuna siku tutawataja hadharani,” alisema.
Mbowe aliitaka serikali isimame na kuwakemea viongozi wa dini wa pande zote mbili kwa kile alichosema mchezo huo hauna mwisho mwema kwa Watanzania.
Kuhusu Mkurugenzi wao wa Ulinzi na Usalama, Mbowe alisema baada ya kukutana naye akiwa gerezani Segerea, alimpa hongera na kuwataka wengine watakaokamatwa kwa tuhuma za kupangwa wasife moyo.
Alisema yeyote ndani ya CHADEMA atakayekamatwa, ahakikishe akiwa mahabusu au gerezani anaeneza sera za chama, na kwamba njia hizo ndizo walizopitia wapigania haki mbalimbali duniani.
“Nilimwambia Lwakatare kwa sasa amekuwa ‘Prison Graduate’, na kwamba aendelee kufanya kazi ya chama huko alipo kwa kuwa hiyo ndiyo njia iliyochaguliwa na serikali kupambana na umma ulioamka,” alisema.
Akielezea sababu za kuwa na kanda, Mbowe alisema lengo ni kushusha mamlaka kwa wananchi badala ya kusubiria uongozi wa makao makuu.
Alisema Serikali ya CCM imekuwa na desturi ya kushindana na CHADEMA kwa kufikiri ipo makao makuu peke yake, hivyo akawataka watakaokuwa katika kanda mbalimbali wahakikishe wanafanya kazi ya kukijenga chama.
Katika hatua nyingine, Mbowe alisema ameshangazwa na uamuzi wa wafuasi wa chama hicho kuingia katika mkutano unaowahusu kwa kiingilio badala ya kutegemea kupewa posho.
Katika mkutano huo, kila mjumbe aliyeingia alitakiwa kuchangia kuanzia sh 5,000
No comments:
Post a Comment