Wateta kwa saa moja
Waahirisha maandamano
Waahirisha maandamano
Maandamano hayo yalitangazwa na Chadema yakiwa na lengo la kutaka kushinikiza Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa na Naibu wake, Philipo Mulugo, wajiuzulu kutokana na matokeo mabaya ya mtihani wa kidato cha nne ya mwaka 2012 ambayo zaidi ya asilimia 60 ya watahiniwa wote walipata sifuri.
Makubaliano hayo yalifikiwa katika kikao kilichofanyika jana makao makuu ya jeshi hilo jijini Dar es Salaam kati ya Mkuu wa Jeshi la Polisi, Inspekta Jenerali (IGP), Said Mwema na Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe.
Viongozi wengine waliohudhuria kikao hicho ni Kamishina wa Operesheni, Paul Chagonja; Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova; Katibu wa Baraza la Vijana Chadema (Bavita), Deogratius Munishi, na Ofisa Habari wa Chadema, Tumaini Makene.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na kusainiwa na Msemaji wa Jeshi la Polisi, Advera Senso na Makene, baada ya mazungumzo, Chadema walikubali kusitisha maandamano hayo ili kutoa fursa ya wananchi kushiriki kwa amani mapokezi ya Rais wa Jamhuri ya Watu wa China, XI Jinping.
Katika kikao hicho, Mbowe na IGP Mwema walikubaliana kufanya kikao cha pamoja ndani ya siku 14 ili kuweka utaratibu mzuri utakaoweka namna nzuri ya kuwasiliana na kushirikiana pasipo migongano huku kila upande ukitimiza wajibu wake kwa maslahi ya taifa.
KABLA YA MAKUBALIANO
Kabla ya makubaliano hayo jana jioni, Kamanda Kova alikuwa ametangaza kupiga marufuku maandamano hayo.
Kamanda Kova akizungumza na waandishi wa habari, alisema amepiga marufuku maandamano hayo kwa kuwa tayari Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, amekwisha kuunda tume kuchunguza sababu za matokeo hayo kuwa mabaya.
Kutokana na sababu hiyo, alisema ni mapema mno kuchukua hatua nyingine na kwamba ni busara kusubiri matokeo ya tume hiyo.
Alitaja sababu nyingine za kupigwa marufuku hayo ni ziara ya kiserikali ya Rais wa Jamhuri ya Watu wa China, Xi Jinping, ambayo ilianza jana jioni.
Aliongeza kuwa ziara ya Rais wa China ina umuhimu mkubwa kwa nchi, hivyo siyo busara kufanya maandamano huku ikiendelea.
Kwa mujibu wa Kamanda Kova, Jeshi la Polisi lilipokea barua kutoka kwa Katibu wa Chadema Kanda ya Dar es Salaam, Henry Kilewo, yenye KUMB. Na: CDM/KN/MK/002/2013 ya Februari 22, mwaka huu ikiwa na kichwa cha habari kuhusu taarifa ya maandamano na mkusanyiko kwenda Ofisi ya Waziri Mkuu, Februari 25, mwaka huu.
Alisema maelezo ya katibu huyo yalidai kuwa wanataka kufanya mkusanyiko na maandamano leo na siyo Februari 22 kama barua hiyo ilivyoeleza hapo awali.
Kova aliongeza kuwa baada ya kupokea barua hiyo, jeshi hilo lilifanya mazungumzo na katibu huyo na kumpa barua yenye KUMB. Na. DSMZ/SO.7/2/A/VOL.II/16 Machi 23, mwaka huu kutoka kwake mwenyewe (Kova).
Barua hiyo ilieleza kutokukubaliana na maandamano hayo kwa kutoa sababu hizo na kuwapa ruhusa ya kukata rufaa kwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Imanuel Nchimbi, kwa mujibu wa sheria kwani wao siyo watu wa mashindano bali watekelzaji wa sheria.
Kwa mujibu wa Kova, chama hicho hakikuridhishwa na sababu hizo na hivyo kupanga kuendelea na msimamo wa kufanya maandamano hayo leo kuanzia Ofisi ya Waziri Mkuu kuelekea maeneo mabalimbali ya Jiji la Dar es Salaam.
Kutokana na hilo, Kamanda Kova alitoa amri kwamba mtu yeyote atakaye husika katika maandamano hayo atachukuliwa hatua.
Alisema wasingewashughulikia wanyonge wanaoonekana kushiriki katika maandamano bali na wale watakaohusika kuwezesha kufanyika kwa matukio hayo bila kujali cheo cha mtu.
Aliwaagiza wakazi wa Jiji la Dar es Salaam kwenda maeneo yao ya kazi bila hofu yoyote kwani jeshi hilo lilikuwa limejipanga vya kutosha kudhibiti tukio hilo.
HALI ILIVYOKUWA ARUSHA
Kabla ya makubaliano ya kusitishwa kwa maandamano hayo kufikiwa, Katibu wa Chadema Mkoa wa Arusha, Amani Golugwa, alisema maandamano yangefabyika leo.
Alisema sababu zilizotolewa na Jeshi la Polisi ni za kufedhehesha.
“Kitendo walichofanya kwa barua hii, polisi sasa wameanza kuzidisha (ma)shaka tuliyokuwa nayo kwao, ingawa katika siku za hivi karibuni hali ilianza kuwa nzuri kidogo,” alisema.
Alisema polisi wametafuta uhalali wa kuzuia maandamano hata katika suala muhimu kama elimu.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment