Tuesday, March 26, 2013

Chadema yampa mkuu wa mkoa siku tatu kuomba radhi


Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Kanda ya Kaskazini, kimempa siku tatu Mkuu wa Polisi Wilaya ya Arusha, Gilles Bilabaye, kuomba radhi wafuasi wa chama hicho na chama kwa kile wanachodai kutoa kauli za matusi.

Aidha, chama hicho kimetangaza mgogoro na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magessa Mulongo, kwa madai  ya kutumia madaraka yake vibaya na  nguvu kubwa ya Jeshi la Polisi kuzuia maandamano na kutoa lugha za matusi.

Akisoma tamko la chama hicho mbele ya waandishi wa habari jijini Arusha jana, Mjumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho, Godbless Lema, alisema viongozi hao waliwaita wafuasi wa Chadema kuwa ni wahuni, wavuta bangi na wanywa viroba, wasio na kazi ndio maana wanakubali kuandamana.

“Chadema tunatoa siku tatu kwa OCD kuomba radhi kwa kutumia njia ile ile ya radio za masafa mafupi na magari ya matangazo waliyotumia kutoa matusi hayo kuomba radhi vijana wa Arusha, kabla ya kuchukua hatua nyingine” alisema Lema kupitia taarifa fupi iliyosainiwa na Katibu wa Kanda hiyo, Amani Golugwa.

Lema alidai kuwa viongozi hao walitoa kauli hizo Jumamosi na Jumapili iliyopita, wakiwa katika harakati za kukabiliana na tishio la maandamano yaliyotangazwa na Chadema kabla ya kuahirishwa baada ya makubaliano kati ya Mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho Freeman Mbowe na Mkuu wa Jeshi la Polisi, Said Mwema.

Alisema iwapo Mulongo ataendelea na tabia ya kuwadharau wapiga kura wake, atamtangazia vita vya kuzuia wananchi kutii mikutano yake na kukataa kabisa kutoa ushirikiano naye.

“Huyu mtu anatumia vibaya madaraka yake na akiendelea hivi na kauli zake za matusi, nitazuia wapiga kura wangu kutomfuata kwenye mambo yake anayoitisha,”alisema. Akijibu tuhuma hizo kwa njia ya simu, Mulongo alisema kwa ufupi kuwa yeye ni mkuu wa mkoa anatimiza wajibu na majukumu yake ya kazi kuhakikisha maandamano hayafanyiki ili mkoa huo uendelee kuwa na amani.

Kwa upande wake,  Bilabaye  aligoma  kuzungumzia tuhuma dhidi yake, akisema mwenye mamlaka ya kuzungumzia suala lolote linalohusu jeshi hilo ni Kamanda wa Polisi Mkoa (RPC) hivyo  aulizwe yeye. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Lebaratus Sabas alipoulizwa kwa njia ya simu, alijibu kwa ufupi kuwa “No Coment”.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment