Monday, March 25, 2013

Mnyika: TISS isaidie serikali kutatua matatizo


MBUNGE wa Ubungo John Mnyika, ameitaka Idara ya Usalama wa Taifa (TISS) kuisaidia serikali kwa kuielekeza kutatua matatizo ya Watanzania badala ya kuhangaika na mikakati ya kuvidhoofisha vyama vya upinzani nchini.
Mnyika alitoa kauli hiyo juzi Kimara, Dar es Salaam, alipokuwa akitoa mada katika kongamano la siku moja lililoandaliwa Umoja wa Wanafunzi Wanachama wa CHADEMA Wanaosoma Vyuo Vikuu (Chaso).
Alisema sheria ya Usalama wa Taifa haijaruhusu idara hiyo kufanya ushushushu dhidi ya vyama vingine vya kisiasa ndani ya nchi kwa ajili ya kukisaidia chama kilicho madarakani.
“TISS inapaswa itambue kila inachokifanya kwa ajili ya kuisaidia CCM hakiivunji mioyo ya Watanzania katika kuipenda CHADEMA; kama inataka kukisaidia chama kilicho madarakani njia nzuri ni kukiambia kitatue matatizo yanayowakabili Watanzania,” alisema Mnyika.
Akizungumzia kushuka kwa ufaulu wa wanafunzi nchini, Mnyika alisema tatizo liko katika ofisi ya Waziri Mkuu kwa kushindwa kusimamia wajibu wake ipasavyo.
Alisema kwa sasa takwimu za kimataifa zinaonyesha katika shule zaidi ya 4,000 za Tanzania ni asilimia 4 tu ndizo zenye sifa ya kuitwa shule, hali aliyosema kama kungekuwa na nia ya dhati ya kuboresha kiwango cha elimu serikali ingeanzia hapo.
Naye Mwenyekiti wa Baraza la Vijana la CHADEMA (BAVICHA) Taifa, John Heche, aliyewataka wasomi nchini kutokuwa waoga kuhoji juu ya uendeshaji wa serikali kwa hofu ya kuitwa wapinzani.
Alisema viongozi wengi wa sasa serikalini hawajitambui na hawatambui umuhimu wa kuwa katika nafasi walizonazo zaidi ya kufikiria kujineemesha binafsi.
Aliongeza kuwa kama vijana waliobahatika kupata elimu ya vyuo vikuu watakuwa waoga wa kukemea maovu ya serikali kuna hatari ya siku moja taifa la Tanzania likapotea.

Tanzania Daima

No comments:

Post a Comment