Friday, February 15, 2013

Zitto aionya Serikali fao la kujitoa

MBUNGE wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (CHADEMA), amesema vijana nchini hawapo tayari kurithishwa nchi ambayo haitakuwa na uwezo wa kulipa mafao ya wastaafu.

Zitto aliyasema hayo mjini hapa jana, alipokuwa akizungumza kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC) wakati wa mkutano wa tatu wa wadau wa NSSF.

Alisema kwamba, asilimia 22 ya uwekezaji wa mifuko ndiyo ipo kwenye majengo wakati asilimia 70 ya uwekezaji ipo kwenye mikopo ya Serikali.

“Tatizo linalokuja hapa ni kwamba Serikali hailipi madeni yake kwenye mifuko ya hifadhi na madhara yataendelea kuwa kwa wanachama na vijana hatupo tayari kurithishwa mafao ya wastaafu,” alisema Zitto.

Zitto, aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma kabla kamati hiyo haijafutwa na Spika hivi karibuni, alisema kuna haja ya kuangalia umri wa Watanzania kwa ujumla wao.

“Leo hii ukichukua mstari ukaukata katikati ya nchi ili kupata asilimia 50 ya Watanzania huku na kule ni wazi kwamba, asilimia 50 ya Watanzania ipo chini ya umri wa miaka 17, kwa hiyo, hii ni nchi ya watoto.

“Na asilimia 70 ya Watanzania wapo chini ya umri wa miaka 29, lakini hiyo ni hali ya sasa, miaka 50 ijayo sehemu kubwa ya wanaoonekana watoto leo, hao ndio watakuwa sehemu ya waliomo kwenye pensheni wakati huo.

“Tunavyozidi kwenda, idadi ya watu watatakiwa kuhudumiwa kama wazee waliostaafu na idadi hiyo itakuwa kubwa zaidi, lakini mfumo wa hifadhi unavyofanya kazi, unaonyesha wanaofanya kazi sasa ndiyo wanaowalipia pensheni wastaafu wa sasa,” alisema Zitto.

Zitto aliendelea kusema kwamba, kama kutakuwa na kundi dogo la wanaofanya kazi katika kipindi hiki, miaka inayokuja kutakuwa na mtikisiko wa pensheni kwa sababu kutakuwa na watu wengi wanaotakiwa kulipwa pensheni.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa NSSF, Dk. Ramadhani Dau, alijivunia mafanikio ya mfuko huo kwa kuwa umeendelea kupiga hatua katika uwekezaji.

Alisema kwa sasa michango ya wanachaa katika mfuko huo imeongeka na kufikia Sh bilioni 500 kwa mwaka jana, ambapo matarajio yao kwa mwaka 2013 ni Sh bilioni 594.

No comments:

Post a Comment