Friday, February 15, 2013

CHADEMA kanda ya mshariki kufunika jiji tarehe 02/03/2013 taarifa ya tolewa kwa umma


TAARIFA KWA UMMA
Kanda ya Mashariki ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) imefanya kikao cha kwanza cha timu ya uratibu ya kanda na kufanya maamuzi mbalimbali ya maandalizi ya Operesheni ya vuguvugu la mabadiliko (M4C) katika mkoa wa Pwani na mikoa ya kichama ya Kinondoni, Ilala na Temeke. 
Kikao hicho cha kazi kimefanyika wilayani Kibaha tarehe 12 Februari 2013 na kuhudhuriwa wajumbe wa Mabaraza ya Uongozi ya Mikoa tajwa ya Kanda, wabunge wa ndani ya kanda na wajumbe wa kamati kuu wanaishi katika kanda ya Mashariki.
Wajumbe wa mabaraza ya uongozi walioshiriki katika kikao husika ni pamoja na wenyeviti wa mikoa, makatibu wa mikoa, waratibu wa shughuli za mabaraza ya vijana (BAVICHA), wazee na wanawake (BAWACHA) na wajumbe wa baraza kuu kutoka katika mikoa husika. 
Wabunge walio katika Kanda ya Mashariki ni John Mnyika (Ubungo), Halima Mdee (Kawe) na Suzan Lyimo, Maulidah Komu na Phillipa Mturano; wote wa viti maalum.
Mosi; kikao kimeamua kwamba makao makuu ya Kanda ya Mashariki yawe Mkoa wa Pwani katika wilaya ya Kibaha.
Pili; Kikao kimeunda kamati ya maandalizi ya Mpango Kazi na Bajeti ya M4C pamoja na Mkakati wa kutafuta rasilimali kwa ajili ya kuendesha Operesheni ya M4C katika Kanda ya Mashariki. 
Kanda ya Mashariki ya CHADEMA inatoa mwito kwa wanachama na wapenda mabadiliko wote kuwasilisha maoni na mapendekezo yao kupitia ofisi za chama za mikoa ya kanda husika kabla ya tarehe 22 Februari 2013 ili kuzingatiwa wakati wa maandalizi ya mkakati husika.
Tatu; Kikao kimeunda kamati ya kuandaa mapendekezo ya muundo wa ofisi ya kanda ikiwemo kuhusu majukumu na mfumo wa utendaji wa mratibu wa kanda na afisa wa kanda. Kanda ya Mashariki ya CHADEMA inakaribisha maombi kutoka kwa wanachama wenye sifa na vigezo vya kuwa mratibu wa kanda na afisa wa kanda. 
Mwanachama yeyote mwenye uwezo na uadilifu wa kukitumikia chama katika mojawapo ya nafasi hizo awasiliane na ofisi yoyote ya mkoa wowote wa kanda ya mashariki kwa ajili ya kupewa orodha ya majukumu na vigezo. 
Baada ya kupokea maelezo na maelekezo waombaji wanapaswa kuwasilisha maombi yao kabla ya tarehe 22 Februari 2013 kwa njia ya nakala tete (Soft Copy) kupitia barua pepe masharikichadema@yahoo.com ya CHADEMA Kanda ya Mashariki na nakala mango (hard copy) kupitia ofisi yoyote ya Mkoa wa Kanda ya Mashariki.
Nne; kikao kimepokea na kuridhia uamuzi wa uongozi ya Mkoa wa Tanga wa mkoa huo kuwa sehemu ya Kanda ya Kaskazini ya CHADEMA. Kikao hicho kilishirikisha pia kamati ya uongozi ya mkoa wa Tanga kama waalikwa.
Tano; kikao kimepanga tarehe 2 Machi 2013 kufanya mkutano maalum wa kanda ya Mashariki kwa ajili ya kufanya uteuzi wa awali wa mratibu na afisa wa kanda, kupitisha mpango kazi na bajeti ya kanda pamoja, kupanga mkakati wa kutafuta rasilimali za kuendesha operesheni katika kanda, kuunda timu ya operesheni ya kanda na kuanza maandalizi ya mafunzo kwa timu husika.
Imetolewa tarehe 15 Februari 2013

Henry Kilewo
Mratibu wa Muda
Kanda ya Mashariki (CHADEMA)

No comments:

Post a Comment