Friday, February 15, 2013

Taarifa ya CHADEMA: Utaratibu wa kuwapata wajumbe wa mamlaka za Serikali za Mitaa

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimewasilisha kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba tarehe 14 Februari 2013 maoni na mapendekezo ya CHADEMA juu ya muongozo uliotolewa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba kuhusu muundo, utaratibu wa kuwapata wajumbe wa mabaraza ya katiba ya wilaya (Mamlaka za Serikali za Mitaa) na uendeshaji wake.

Maoni na mapendekezo yaliyowasilishwa katika nyaraka ya kurasa tisa yamehusu vipengele vyote kumi vya muongozo huo, katika hatua ya sasa tunatoa taarifa kwa umma kuhusu kipengele kimoja cha muundo wa mabaraza ya katiba katika ngazi ya wilaya uliopendekezwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba.

CHADEMA hakikubaliani na muundo wa kuwa mabaraza hayo ya wilaya yatakuwa na wawakilishi walioteuliwa na ngazi ya kata; badala yake CHADEMA kinapendekeza kuwa wajumbe wote waliochaguliwa kuwakilisha vijiji au mitaa au shehia waingie moja kwa moja kwenye mabaraza ya wilaya.

Hivyo, kwa upande wa Tanzania bara, katika mikoa yote ngazi ya kuwapata wajumbe wa mabaraza ya katiba ya wilaya (Mamlaka za Serikali za Mitaa) isiwe ngazi ya kata; bali wajumbe wapigiwe kura ya kuchaguliwa kwenye ngazi ya kijiji/mitaa.

Kwa upande wa Zanzibar, katika Mikoa yote ngazi ya kupata wajumbe wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya (Mamlaka za Serikali za Mitaa) itakuwa ni Shehia kwa wajumbe kupigiwa kura kwenye ngazi za Sheria.

Hii itafanya kuwa na utaratibu unafanana kwa kuzingatia kifungu cha 17 (8) cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba kwa kila upande wa Muungano tofauti na mapendekezo ya Tume ambapo wakati kwa upande wa Tanzania bara kuna mfumo wa mapendekezo ya uteuzi kwenye ngazi moja (kijiji/mtaa) na uchaguzi katika ngazi nyingine (kata), kwa upande wa Zanzibar uchaguzi ungefanyika moja kwa moja katika ngazi moja (Shehia); pamoja na tofauti za mifumo ya Serikali za Mitaa.

Aidha, muundo na utaratibu huu ni muhimu katika kurekebisha upungufu katika mchakato uliotangazwa kukamiilika wa ukusanyaji wa maoni ya wananchi binafsi uliofanyika kwa awamu nne mwaka 2012 ambapo tume ilifanya mikutano 1776 tu na wananchi wachache kutoa maoni kutokana na sababu mbalimbali.

Izingatiwe kuwa upungufu katika mchakato wa ukusanyaji wa maoni ya wananchi binafsi ilisababisha idadi ndogo ya watu waliotoa maoni ambapo mpaka awamu nne zinakamilika jumla ya watu 318,223 tu ndio waliotoa maoni sawa na asilimia 0.7 ya wananchi wote zaidi ya milioni 44.9.

Hivyo, muundo wa mabaraza ya katiba ya wilaya wenye uwakilishi kutoka kwenye kila kijiji/mtaa/shehia utaongeza idadi na wigo wa ushiriki wa wananchi kwa kuhakikisha kila kata na kila kijiji/mtaa au sheria zimeshiriki katika kupitia rasimu ikiwemo kutoka katika maeneo ambayo hayakufikiwa na tume katika awamu zote nne za mikutano ya kukusanya maoni kwa wananchi binafsi.

Ikiwa Tume itaona ugumu wa ufanisi wa uendeshaji wa mabaraza kutokana na idadi ya wajumbe, basi tume ikubali pendekezo la awali la kuwa mabaraza hayo yaanzie kwenye ngazi ya kata ili wawakilishi hao kutoka kwenye vijiji/mitaa wakutane katika kata zao na ngazi ya wilaya ihusishe wawakilishi wa makundi mbalimbali ya wananchi katika jamii ya ngazi ya wilaya.

Utaratibu huu utawiana na muundo wenyewe wa Tume ambao kitaifa umehusisha makundi mbalimbali, Vyama vya siasa na Taasisi, lakini kwenye mabaraza wananchi wanatakiwa tu kuchagua wawakilishi kwa msingi wa umri. Ikumbukwe kuwa kwenye ngazi ya kijiji hakuna mikutano inayowakutanisha wananchi kwa umri au jinsia.
Pia, muundo na utaratibu huu utaondoa migogoro itakayojitokeza kwa ngazi ya kamati ya maendeleo ya kata (ambayo mwenyekiti wake ni diwani na wajumbe wake ni wenyeviti wa mitaa; ambao wote ni viongozi wa kisiasa wanaotokana na vyama vya siasa); kufanya uchaguzi baada ya wananchi wote kuwa tayari wametoa mapendekezo yao katika mikutano ya vijiji/mitaa.

Inafahamika kwa mujibu wa matokeo ya uchaguzi na vitongoji, vijiji na mitaa wa mwaka 2009 na Uchaguzi wa Udiwani wa mwaka 2010 zilivyo na hodhi ya chama kimoja katika maeneo mbalimbali nchini hali ambayo inaondoa uhalali wa kamati hizo kufanya kazi ya uteuzi wa wajumbe iwe ni kwa  niaba ya tume au kwa niaba ya wananchi.

Aidha, pamoja na kifungu cha 18 (6) kueleza aina nyingine ya Mabaraza ya Katiba kuwa Tume inaweza kuruhusu Asasi, Taasisi au Makundi ya Watu kuwasilisha maoni yao kuhusu Rasimu ya Katiba; ruhusa na utaratibu huo hauondoi haja ya asasi, taasisi  na makundi hayo kuwa na uwakilishi katika mabaraza ya katiba yanayosimamiwa na tume kwenye ngazi ya wilaya.

CHADEMA kinatahadharisha kwamba muundo na utaratibu huu uliopendekezwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba utarudisha nyuma jitihada za kujenga muafaka wa kitaifa kuhusu mchakato na maudhui ya katiba mpya.
Imetolewa tarehe 15 Februari 2013 na:

John Mnyika (Mb)
Mkurugenzi wa Habari na Uenezi


No comments:

Post a Comment