Wednesday, February 13, 2013

Tumejifunza nini mdahalo Kenya?


WAGOMBE saba wa kiti cha urais nchini Kenya, juzi walichuana katika mdahalo mkali wa kwanza ambapo waliweza kujieleza kuhusu masuala mbalimbali ya sera za vyama vyao kuelekea uchaguzi mkuu ujao Machi 4.
Wagombea hao mbali ya mambo mengi waliyoyatolea ufafanuzi, wote walionyeshana ufundi katika suala la kuiepusha Kenya isirejee kwenye machafuko baada ya uchaguzi kama ilivyokuwa katika uchaguzi mkuu uliopita mwaka 2007.
Wagombea hao na vyama vyao kwenye mabano ni Raila Odinga (Cord), Uhuru Kenyetta (Jubilee), Prof. ole Kiyiapi (RRK), Peter Kenneth (KNC), Musalia Mudavadi (Amani), Martha Karua (NARC-Kenya), Paul Muite (Safina) na Mohammed Dida (ARC).
Tunawapongeza wagombea wote kwa umaridadi wa kujenga hoja na kutetea sera na ilani za vyama vyao, badala ya kujiegemeza katika kujadili masuala binafsi ya kushambuliana mtu na mtu.
Licha ya vijembe vidogovidogo vya hapa na pale lakini kimsingi mdahalo huo ulikuwa mzuri wenye kuwapa nafasi wananchi kuwapima wagombea wao kuona ni nani anastahili kuwaongoza.
Mdahalo wa juzi ni chachu na changamoto kwa wanasiasa wetu nchini ambao kila inapofika uchaguzi mkuu, wengi wanapiga porojo majukwaani badala ya kueleza sera na ilani zao. Swali ni je, tumejifunza nini katika mdahalo huo wa Kenya?
Bila shaka liko la kujifunza. Kwanza ni waandaaji na waendeshaji wa tukio hilo, waliwauliza wagombea maswahi makini ambayo yanamaliza kiu ya wananchi wa Kenya ambao wasingiweza kupata nafasi hiyo kuwauliza viongozi wao watarajiwa.
Pili, ni umakini na kujiamini kwa wagombea wenyewe. Hili ni jambo la pekee kwani tunaambiwa wako baadhi walilazimika kwenda mahakamani kuhoji kwa nini hawakuwa wameshirikishwa mwanzoni.
Tunasema hivyo kutokana na ukweli kwamba wanasiasa wengi wakati wa kuelekea uchaguzi hawapendi sana midahalo kutokana na kutojiamini nini waseme mbele ya wananchi.
Hii imetokea hata Tanzania wakati wa uchaguzi mkuu wa 2010 kwa mgombea wa CCM, Jakaya Kikwete, kukwepa siku za mwisho.
Kwa wanasiasa wakomavu na makini, midahalo ndiyo sehemu ya kujijenga na kujiongezea kura za wananchi, kwa hiyo wale wanoikimbia ni wazi wana kasoro, hawana hoja za kuwaeleza wapiga kura wao bali wanategemea majukwaa ili walopoke chochote bila mpangilio.
Kikwete alikwepa mdahalo uliokuwa umkutanishe na wagombea wenzake wawili, Dk. Willibrod Slaa (CHADEMA), na Prof. Ibrahim Lipumba (CUF) kati ya wagombea saba waliokuwa wakiomba nafasi hiyo.
Lakini huyo huyo alikuwa mwepesi wa kujitokeza katika mahojiano ya pekee aliyoandaliwa na chama chake na kurushwa katika vyombo vyote vya habari ambayo hayakuwa na maswali ya kidadisi zaidi kama tulivyoona katika mdahalo wa Kenya.
Yafaa kuutumia mdahalo wa Kenya kama changamoto kwetu kuwashinikiza wagombea wetu wa urais katika uchaguzi mkuu ujao wakubali kuandaliwa mdahalo wa kuwakutanisha pamoja na kunadi sera zao kwa hoja.

No comments:

Post a Comment