WABUNGE CCM NAO WAPANGA KUMNG’OA
MKAKATI wa Spika wa Bunge, Anna Makinda, kutaka kuitetea serikali hata pale inapofanya madudu ya wazi, umeelezwa kuwa chanzo cha kuvurunda kiutendaji kwa kiongozi huo wa muhimili wa dola.
Kutokana na udhaifu huo, Makinda amejikuta akibebeshwa lawama kutoka kwa wananchi, wafuasi wa vyama vya upinzani na kibaya zaidi hata baadhi ya viongozi wa juu na wabunge wa chama chake ambao baadhi wanadaiwa kusuka mkakati kutaka kumg’oa.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili mjini Dodoma hivi karibuni, mkakati huo unaongozwa na baadhi ya wabunge wa CCM wanawake ambao tangu awali hawakuunga mkono namna alivyoingia Bungeni kushika wadhifa huo.
Wapinzani hao wa Spika hasa wale wa kutoka ndani ya CCM, wameingiwa wasiwasi kwamba mwenendo wake wa kutaka kuibeba serikali, unawapa umaarufu wabunge wa upinzani na hivyo kuweka mazingira magumu ya CCM kushinda katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.
Katika mkutano wa kumi wa Bunge uliopita, Spika pamoja na Naibu wake, Job Ndugai, walionyesha udhaifu wa waziwazi wa kuibeba serikali pale walipoamua kupindisha kanuni kuibeba serikali.
Kiti cha Spika kilizima hoja mbili binafsi za Mbunge wa Ubungo, John Mnyika (CHADEMA), aliyekuwa na hoja ya kuboresha huduma ya maji katika jiji la Dar es Salaam na James Mbatia (NCCR-Mageuzi), aliyezimwa na hoja ya udhaifu wa mfumo wa elimu nchini.
Matumizi mabaya ya kanuni zilizotumika kuzima hoja hizo, uliibua vurugu na mzozo mkubwa na wa kwanza katika historia ya Bunge la Tanzania na kusababisha kuzima hoja nyingine binafsi mbili.
Spika Makinda amejikuta katika lawama kubwa zaidi pale kiti chake kiliporuhusu kupitisha mapendekezo ya serikali kufanya mabadiliko katika Sheria ya Ukaguzi wa Hesabu za Umma ya mwaka 2008 na kuvunja kamati za Bunge.
Katika mapendekezo hayo, serikali imeongeza vifungu vinavyopunguza nguvu ya Bunge katika kushughulikia taarifa ya Ofisi ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili katika ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, umebaini kuwa muswada huo wa sheria ambao ulipita kwa mbinde kutokana na upinzani wa wabunge wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), ulikuwa na nia ya kuwadhibiti wabunge wa kambi ya upinzani ili kuinusuru serikali.
Kwa mujibu wa ibara ya 143 (4) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano, (CAG) anawajibika kuwasilisha taarifa yake kwa Rais ambaye baada ya kuipitia, atawasilisha taarifa hiyo kwenye kikao cha Bunge kilicho karibu kabla ya kupita siku saba tangu kikao hicho cha Bunge kuanza.
Chini ya mabadiliko hayo sasa, ripoti za CAG baada ya kutoka kwa Rais, itawasilishwa na kujadiliwa katika kamati tatu zinazosimamia hesabu za serikali kwa ajili ya kufanya uchambuzi, kisha kuwasilisha Bungeni katika muda zitakaopangiwa.
Wachambuzi wa duru za siasa wanasema kuwa kwa mabadiliko hayo, Bunge halitakuwa tena na uwezo wa kuwawajibisha watendaji wa serikali ambao watabainika kuhusika na upotevu wa fedha au kufuja fedha za umma, hivyo kupunguza makali ya mijadala ya wabunge wa upinzani Bungeni.
“Hatua hiyo ni sawa na kulifunga mikono Bunge kutekeleza wajibu wake kuhusu ripoti ya CAG kwani halitaweza kujadli chochote kabla ya serikali kuipitia na kuipatia majibu yake,” alisema mtoa habari wetu.
Hata hivyo kamati za Bunge ambazo taarifa za CAG zinapaswa kuwasilishwa ni zile za hesabu za mashirika ya umma (POAC), iliyokuwa ikiongozwa na Zitto Kabwe ambayo kwa sasa imefutwa.
Kamati nyingine ni ile ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), inayoongozwa na Mbunge wa Augustine Mrema (TLP) na Kamati ya Hesabu za Serikali Kuu (PAC), iliyokuwa ikiongozwa na Mbunge wa Bariadi Mashariki, John Cheyo (UDP).
Hata hivyo wakati marekebisho hayo ya sheria yanafanyika na kupendekeza taarifa hizo ziwasilishwe kwenye kamati hizo, Spika Makinda kwa mamlaka aliyopewa amezifuta baadhi na kuziunganisha zingine kuwa moja.
Habari kutoka ndani ya ofisi ya Mwanasheria wa Serikali (AG), zilisema kuwa lengo la mabadiliko hayo ni kuikoa serikali na hoja za wabunge wa upinzani ambao mwaka jana nusura waiangushe serikali.
“Hatua hiyo itaiokoa serikali kwani utaratibu mzima wa kushughulikia taarifa hizo umebadilika na vimeongezwa vipengele vinavyoliwajibisha Bunge kwa serikali. Vipengele hivi vinazitaka kamati za Bunge zinapofanya uchambuzi wa ripoti ya CAG, kupeleka maazimio yake kwa serikali ili yatafutiwe majibu badala ya utaratibu wa sasa wa kupeleka hesabu zake moja kwa moja Bungeni,” alisema mtoa habari wetu kutoka ofisi ya CAG.
Kwa mujibu wa habari hizo, serikali imeleta mabadiliko hayo ambapo chini ya utaratibu huo, itakuwa na majibu ya hoja za wabunge tofauti na utaratibu wa zamani ambapo haikuwa rahisi kwa serikali kuwa na majibu sahihi.
Mwaka jana, Rais Kikwete alilazimika kufanya mabadiliko katika Baraza la Mawaziri na kuwaondoa mawaziri Sitta na Manaibu Waziri wawili, yakiwa ni matokeo ya mjadala wa ripoti ya CAG ambayo ilibainisha kuwapo kwa madudu mengi.
No comments:
Post a Comment