Thursday, February 14, 2013

Dk Slaa afunguka


KATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Dk. Wilbroad Slaa amesema siku za chama tawala kukaa madarakani zinahesabika, hatishwi na wanaomsema kuhusu imani yake na kwamba mchumba wake Josephine Mushumbuzi ni mwanamke imara.
Akizungumza katika mahojiano maalumu na Raia Mwema wiki hii, Makao Makuu ya CHADEMA, Dar es Salaam, Dk. Slaa alisema CHADEMA kimedhamiria kwa dhati kukiondoa madarakani Chama cha Mapinduzi (CCM) na kwa kuanzia ili kujisambaza hadi waliko wapiga kura, kimeamua kwamba katika kila kaya 30 za familia kutakuwa na balozi, wakati katika kila nyumba 10 kutakuwa na kiongozi wa shina, ambalo katika mfumo mpya wa uongozi, litaitwa ngazi ya msingi.
Aidha, Dk. Slaa katika mahojiano hayo yaliyochapishwa katika kurasa za 12 na 13, za toleo hili, na yatakayoendelea wiki ijayo, amesema katika kutekeleza mkakati wao wa kukipeleka CHADEMA chini kabisa kwa wananchi vijijini, sasa oparesheni za Vuguvugu la Mabadiliko (M4C) hazitakuwa za mkoa kwa mkoa tena, kama zilivyokuwa zikiratibiwa, bali zitakuwa zikifanyika kwa wakati mmoja na kwa mara kwa mara katika vijijini vyote vya Bara na Visiwani.
Anasema kuanzishwa kwa utaratibu huo mpya wa mfumo wa uongozi na oparesheni za M4C, kunalenga kuhakikisha kwamba hadi kufikia Septemba mwaka huu, CHADEMA inavifikia vijiji zaidi ya 18,000 nchini, kazi itakayokwenda sambamba na uzinduzi na ufunguzi wa matawi 18,000 ya CHADEMA na zaidi ya mashina ya msingi 50,000.
Kwa mujibu wa Dk. Slaa mikakati yote hiyo, inalenga pia kuhakikisha kwamba chama hicho kinachukua madaraka ya utawala wa Serikali za Mitaa katika uchaguzi wa 2014, kabla ya kukamata madaraka ya Serikali Kuu mwaka 2015.
Mfumo wa uongozi katika ngazi ya balozi wa nyumba kumi, ni mfumo ambao hadi sasa ulikuwa unatumiwa na CCM pekee kati ya vyama vyote vya siasa nchini, hali ambayo wachambuzi wa mambo wanasema mfumo huo ndio mara nyingi umekuwa ukikihakikishia ushindi chama hicho katika kila chaguzi za kisiasa zinazoshirikisha vyama vingi. Dk Slaa alisema viongozi wao nao katika ngazi hiyo, wataitwa jina hilo hilo la balozi kutokana na kile alichokiita ‘historia ya jina hilo.’
Akizungumzia mkakati huo wa kukizamisha chama chake hicho vijijini kuliko na watu wengi, uamuzi uliotokana na maazimio ya kikao cha Baraza Kuu kilichokutana hivi karibuni, na ambao unatakiwa kuanza rasmi Aprili mwaka huu, Dk Slaa alisema:
“M4C sasa inakwenda kuimarisha misingi ya chama vijijini. Katika kila kaya 30 za familia, CHADEMA tutakuwa na balozi wetu kama alivyo balozi wa nyumba kumi wa CCM. Na katika kila nyumba 10, tutakuwa na shina, ambalo tutaita ngazi ya msingi ya uongozi. Kwa nini na sisi tumeamua kiongozi wetu aitwe balozi, ni suala la historia tu. Baada ya hapo tunakuwa na waratibu wa M4C kwenye ngazi ya kijiji, ngazi ya kata, ngazi ya jimbo, ngazi ya wilaya, mkoa na ngazi ya kanda.
“Ofisi ya Katibu Mkuu Taifa ndiyo iliyokuwa inaratibu oparesheni zote za M4C. Sasa ofisi imekasimisha kazi hiyo ya kuratibu oparesheni za M4C kwa Waratibu wa Kanda. Hawa watachaguliwa na wanachama wetu huko huko kwenye ngazi ya kanda, kazi yetu sisi wa Makao Makuu, kupitia vikao vyetu vya chama itakuwa ni kuwathibitisha wale waliochaguliwa kuwa Waratibu.
“Tofauti na Oparesheni Sangara ambayo ilikuwa inakwenda mkoa kwa mkoa, oparesheni ya M4C itakuwa inafanyika kwa wakati mmoja katika vijiji vyote vya Tanzania, Bara na Visiwani. Kwa hiyo, unaweza ukapima mwenyewe aina ya kishindo kitakachotokana na oparesheni hiyo.
“Tunataka, kufikia Septemba mwaka huu tuwe tumevifikia vijiji vyote takriban 18,000 vya nchi hii. Tumewekeana malengo kitimu, ni vijiji vingapi vifikiwe na oparesheni ya M4C, na kwa maana hiyo hiyo, hadi kufikia Septemba CHADEMA tutakuwa tumefungua matawi ya ofisi za chama chetu vijijini zaidi ya 18,000 na mashina ya msingi (chini ya balozi) kiasi cha mara tatu ya idadi hiyo ya matawi.”
Katika mahojiano hayo, Dk Slaa alizungumzia pia wale wote wanaomshangaa Mchumba wake, Josephine Mshumbusi, kwa ushiriki wake wa moja kwa moja katika siasa za CHADEMA, pamoja na wote wanaohusisha upadiri na ukatoliki wake katika mbio zake za urais.
Akiwazungumzia wanaomshangaa Mchumba wake Josephine kushiriki moja kwa moja siasa za CHADEMA, Dk Slaa anasema: “ Kama kuna Watanzania wanashangaa kuniona nikiwa na Josephine kwenye siasa za CHADEMA, basi hao sijui bado wanaishi karne gani katika dunia hii. Ina maana watu hao hawajamwona Michelle akiwa na Obama?
“Ni lini walimuona Obama katika kipindi chake chote cha kampeni akiwa mpweke bila kuwa na Michelle? Kuna mazingira fulani, yalimlazimu Obama kuwa na familia yake nzima kwa maana ya mke wake na watoto wake wale wawili. Karne hii, mtu anamshangaa mgombea urais kuwa na mke wake. Anamshangaa katibu mkuu wa chama cha siasa kikubwa kama hiki kumtanguliza mbele mke wake katika shughuli za umma? Ni maajabu kweli kweli!
“Inawezekana wanaohoji hayo yote, hawamjui Josephine ni nani, ametokea wapi. Wanadhani ni kibaka tu niliyemuokota mitaani yupo kwa ajili ya kunichuna? Wamekosea. Kabla ya kuwa na mimi, huyu alikuwa ndiye mtaalam pekee wa IT (Teknolojia ya Mawasiliano), Mwakilishi wa UNHCR Kanda ya Afrika. Josephine ni international figure…mimi nimeishi na kufanya kazi Ulaya, najua aina ya mke wa hadhi yangu.
“Watu wanakimbilia majungu, hawataki hata kufikiri wafanye utafiti hata kidogo juu ya maisha ya mtu. Yeyote ambaye angefanya utafiti kidogo tu kuhusdu maisha ya Josephine; yeye ni nani na ametoka wapi, asingeweza kushangaa anapomuona akishiriki siasa za moja kwa moja na CHADEMA…huyu kwa asili yake ni ‘activist’ (mwanaharakati)…nambie ni kwa jinsi gani naweza kuzuia uana harakati wake eti kwa sababu tu ni first lady mtarajiwa?”
Kwa upande wa wale wanaosema kutokana na upadiri wake hafai kuwa Rais wa Tanzania kama ilivyotokea katika kampeni za Uchaguzi Mkuu wa 2010, Dk. Slaa anasema: “Upadiri na Ukatoliki wangu wanaujua zaidi wananchi wa Karatu. Hawa ndio walioandaa na kushuhudia sherehe zangu za kusimikwa upadiri mwaka 1977, na ndio ambao wamefurahia huduma yangu kama mbunge wao kwa miaka 15 hadi naondoka mwaka 2010. Jimbo la Karatu, kama yalivyo majimbo mengine yote, kuna wakristo na waislamu hivyo hao ndio wanaweza kuhoji kama katika utumishi wangu kwao, nilionyesha dalili yoyote ya kuwabagua kwa misingi ya dini.
“Wakati wa kampeni mwaka 2010, wapo waliosema nimetumwa na Kanisa Katoliki kugombea urais. Wengine wakasema nautaka urais ili nikatekeleze matakwa ya Kanisa. Lakini hao hao, ndio waliokuwa wakieneza taarifa kwamba mimi nilifukuzwa upadri. Yaani Kanisa linifukuze kazi ya upadri, halafu hilo hilo linitume kazi ya urais. Hao ni wale ambao mara nyingi nawaita watu wenye ufupi wa akili ya kufikiri!
“Wenye akili timamu walipaswa kujiuliza Dk. Slaa alitokaje kwenye upadri, kwa maana Kanisa Katoliki lina utaratibu wake wa kuwaondoa kazini mapadri. Kuna wanaoondoka kwa kufukuzwa, kuna wanaoondoka kwa kutoroka wenyewe, lakini kuna wanaoondoka kwa utaratibu kama wa kwangu wa kuandika barua kwa Papa ya kuomba, barua inapokewa na kujadili sababu zake, na wakishajiridhisha wanakupatia kile tunachokiita (kwa Kanisa Katoliki) Laicization, kwa maana ya kurudishwa kwenye kuwa muumini wa kawaida.
“Hata hivyo, tofauti ya muumini wa kawaida, na tofauti ya padri aliyefukuzwa au kuacha kazi kwa utoro, mimi nikiwa na wewe safarini tukapata ajali, ninayo ruhusa ya Papa na Kanisa ya kutoa sakramenti ya upako wa mwisho kwa mtu anayekata roho na sakramenti hiyo ikapokewa kwa Mungu mbinguni. Kama wakati inatokea ajali hiyo ninayo Komunyo, naruhusiwa pia kuitoa. Padiri aliyefukuzwa na au kotoroka hana ruhusa hii.
“Kwa hiyo, ni watu wale wavivu wa kufikiri, wavivu wa kufanya utafiti wanaoweza kuihusisha taasisi ya urais na upadiri wangu au ukatoliki wangu kwa sababu hawataki kujishughulisha kujua taasisi ya urais inafanyaje kazi, inaendeshaje nchi. Mimi niliondoka salama kwenye upadri. Sina ugomvi na mapadri wala maaskofu wangu. Labda kwa kuwakumbusha tu Watanzania, nilipokuwa Katibu Mkuu wa TEC, mimi Dk. Slaa ndiye niliyesimamia kupeleka mradi wa kwanza kabisa wa maji Kojani, Zanzibar, na hadi leo maji yale yapo yanatumiwa na jamii ya Kojani, ambao sidhani kama ndani yake kuna Mkristo hata mmoja.
“Watanzania turejee kwenye misingi yetu ya asili kama Taifa ambayo ilituwezesha kuishi kama ndugu moja na Taifa moja. Tuache kuingiza dini kwenye siasa. Dini ni ya watu na Mungu wao. Dini si suala la nchi. Ufisadi, rushwa na matumizi mabaya ya rasilimali za nchi yetu, mambo haya hayana dini!
Raia mwema

No comments:

Post a Comment