Friday, February 15, 2013

Wananchi waja juu


WAHOJI JEURI YA KASHILILAH KUFICHA VIKAO VYA BUNGE GIZANI
SIKU moja baada ya Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashililah kudai kuwa wako katika mchakato wa kuandaa utaratibu kusitisha kurusha vikao vya Bunge moja kwa moja kwenye vyombo vya habari ili kuzuia purukushani za wabunge, wananchi wamechachamaa wakisema asithubutu.
Akizungumza na waandishi wa habari juzi jijini Dar es Salaam, Dk. Kashililah alisema kuwa wamefikia uamuzi huo kutokana na baadhi ya wabunge kukiuka kanuni kwa makusudi ili waonwe na wapiga kura wao.
Katibu huyo alikwenda mbali zaidi akiwadhalilisha wabunge wanawake kuwa, wale ambao wanajua siku hiyo watauliza maswali wanavalia kikweli kweli ili waonekane.
Kutokana na uamuzi huo wa Bunge, baadhi ya wananchi, viongozi wa kisiasa, dini, wanaharakati na wadau mbalimbali, walifika chumba chetu cha habari au kupiga simu wakipinga kauli hiyo ya Dk. Kashililah, huku wakihoji ni wapi amepata mamlaka ya kuwaamulia.
Pia wapo walioitafsiri kauli yake kwa wanawake wabunge kama matusi ya nguoni yaliyolenga kuwadhalilisha kuwa walikwenda bungeni kujipamba ili waonekane kwenye vyombo vya habari badala ya kujadili kero za wananchi.
Wengi walihoji sababu ya Spika Anne Makinda na wasaidizi wake kufikia hatua hiyo, kutaka kuzungumza na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ili kuzuia matangazo hayo, kwamba wanalenga kuficha kitu gani.
Nao wadau wa masuala ya habari walisema kuwa uamuzi huo unalenga kuiweka taaluma na vyombo vya habari mfukoni ili wananchi wasiiwajibishe serikali yao kwa uzembe, kwani habari zitakazokuwa zikitolewa ni zile zilizofanyiwa uhariri wa hali ya juu wa kusifia.
Msimamo wa CHADEMA
Akizungumza na Tanzania Daima kwa simu, Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), John Mnyika alisema kuwa wazo la kuacha kurusha matangazo ya Bunge moja kwa moja ni la kunyima haki ya wananchi kupewa taarifa kwa mujibu wa katiba ya nchi ibara ya 18.
Kwamba hali hiyo ni kuathiri uhuru wa wananchi kushiriki katika shughuli za utawala wa nchi moja kwa moja au kupitia wawakilishi wao, yaani wabunge kwa mujibu wa ibara ya 21.
“CHADEMA inauonya uongozi wa Bunge usithubutu kufanya maamuzi hayo, sisi tutawaongoza wananchi kuchukua hatua ambazo wataona zifaa dhidi ya uongozi wa Bunge, serikali na CCM ambayo imekuwa ikiingilia utendaji wa viongozi wa Bunge,” alisema.
Alisema kuwa CHADEMA inaona kwamba ni wazo binafsi la Katibu wa Bunge kwa kuwa kabla ya kuahirishwa kwa shughuli za Bunge katika mkutano uliopita, Spika Makinda alitoa wazo la kutaka chombo cha habari cha umma kiongezewe fedha zaidi kuweza kurusha moja kwa moja yote yanayotendeka bungeni.
Mnyika aliongeza kuwa, iwapo sio wazo binafsi la Kashililah, Spika wa Bunge ajitokeze na kueleza ni kikao kipi kingine kimejadili na kukubaliana kuuleza umma kuhusu wazo hilo lenye kushughulika na matokeo ya yanayojiri bungeni.
Alisema kuwa mfululizo wa matukio kuanzia kwenye kuondolewa kwa hoja za wabunge, kuvunjwa kwa baadhi ya kamati, kupitishwa kwa marekebisho ya sheria mbalimbali juu ya vifungu vinavyohusu ukaguzi wa fedha za umma na sasa kusudio la kuacha kurusha matangazo ya Bunge moja kwa moja; kunaonesha kwamba serikali inayoongozwa na CCM inawajibishwa bungeni na Kambi Rasmi ya Upinzani inayoongozwa na CHADEMA.
Mnyika aliongeza kuwa, badala ya katibu huyo kushughulikia matokeo na kuwakosesha haki wananchi, ajikite katika kushughulikia vyanzo vya hali inayoendelea bungeni kwa kuushauri uongozi wa Bunge kuzingatia kanuni na haki.
NCCR Mageuzi yanena
Chama cha NCCR-Mageuzi, kupitia kwa Kaimu Katibu Mkuu wake, Faustine Sungura, kimesema kuwa hatua hiyo ni kuwanyima haki wananchi juu ya kupata habari wakati Bunge likiendelea.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Sungura alisema kuwa hoja ya Katibu wa Bunge ni dhaifu na hasi, ambayo hailengi kujenga Bunge badala yake inabomoa.
Alisema kuwa wanapinga hatua hiyo kutokana na umuhimu wa wananchi kupata habari.
“Vurugu zinazodaiwa kutokea bungeni haziwezi kukomeshwa kwa kuzuia kurusha matangazo ya moja kwa moja. Vurugu hizo zinaweza kukomeshwa kwa kutumia utaratibu wa kawaida wa kutumia kanuni,” alisema.
Sungura alisema kuwa kuzuia matangazo ya moja kwa moja hakuwezi kumzuia mbunge anayejisikia kuongea kinachodhaniwa ni ‘pumba’ na kwamba hakuzuii wabunge wengine kutafakari kwa umakini.
CUF waonya
Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Prof. Ibrahim Lipumba alisema uamuzi huo ni kinyume na utawala bora, kidemokrasia na utawala wa sheria.
Alisema kuwa watawaagiza wabunge wao wapinge suala hilo kwa kufuata taratibu zilizopo, kwani wananchi wanadai haki yao ya kuona moja kwa moja kile wanachozungumza wawakilishi wao bungeni.
Asasi ya kiraia
Asasi ya Twaweza imesema kuwa imesikitishwa na msimamo huo kwa sababu nchi ilikuwa inasifika kwa uwazi.
Kwamba hata rais alishawahi kujivunia wazi na uwajibikaji, hivyo spika na naibu wake watafakari na watumie busara kwani wananchi wana haki ya kujua kuwa wanawakilishwa.
“Watafakari na kutumia busara, wanaposema Bunge limepoteza hadhi, hadhi hairudishwi kwa kuficha kutokuoneshwa bali kanuni na taratibu za Bunge ziboreshwe,” alisema.
Mkurugenzi wa Taasisi ya Raia ya kufuatilia mwenendo wa Bunge, Marcus Albanie alisema taarifa hizo zinabainisha kuwa matatizo makubwa yako katika uwezo wa viongozi wa Bunge.
“Sababu zilizobainishwa na Katibu wa Bunge hazina mashiko kwa kuwa kutafuta umaarufu ni moja ya mbinu za wananasiasa kukubalika na kuchaguliwa kushika dola.
Naye Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Bashir Ally alisema utaratibu huo wa Bunge yawezekana unawalenga watu waliowakusudia na si kwa Watanzania wengi.
Akifafanua kauli hiyo, Ally alisema Watanzania wengi ni maskini ambao hawana muda wa kuangalia vikao vya Bunge vya moja kwa moja, na badala yake wanautumia muda mrefu kuhangaikia kula yao.
“Nchi imepasuka vipande viwili sasa, lipo kundi la waliokuwa nacho wachache ambalo wanaishi mijini na wengi wasiokuwa nacho wanaoishi vijijini. Je, hao watapata hasara ipi katika hatua ambayo inachukuliwa na Bunge?” alihoji.
Hata hivyo, Ally alilitaka Shirika la Taifa la Utangazaji Tanzania (TBC) kama chombo cha umma na vingine vya binafsi kuandika habari za vijijini kama kuwapa changamoto wabunge, serikali na viongozi wa kisiasa ili waweze kuzitatua.

No comments:

Post a Comment