MWANASHERIA Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Fredrick Werema amewasilisha sababu 10 katika Mahakama ya Rufani nchini, akiomba itengue hukumu ya Mahakama Kuu Kanda ya Sumbawanga ambayo Aprili mwaka jana ilimvua ubunge, aliyekuwa Mbunge wa Sumbawanga Mjini, Aeshi Hillary (CCM).
Jaji Werema amedai kuwa hukumu hiyo iliyomvua ubunge Aeshi ilikuwa na dosari za kisheria, na hivyo kuiomba Mahakama ya Rufani itoe amri ya kusitisha utekelezwaji wake.
Rufaa hiyo iliwasilishwa chini ya hati ya dharura ambayo bado haijapangiwa jopo la majaji wa kuanza kuisikiliza.
Mwanasheria Mkuu anaiomba Mahakama ya Rufani itangaze kwamba uchaguzi wa jimbo hilo uliofanyika Oktoba 31 mwaka 2010, ulikuwa ni wa huru na haki.
Kwamba matokeo yaliyomtangaza Aeshi kuwa mshindi yalikuwa ni halali na yalikidhi matakwa ya sheria ya uchaguzi na kanuni zake.
Mbali na mwanasheria mkuu, warufani wengine ni Justus Kasirama (msimamizi msaidizi wa uchaguzi Kata ya Katandala) na Vistus Kapufi (msimamizi msaidizi wa uchaguzi Kata ya Matanga).
Warufani hao waliwasilisha rufaa hiyo Januari 10 mwaka huu, dhidi ya aliyekuwa mgombea wa ubunge wa jimbo hilo kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Nobert Yamsebo.
Kwa mujibu wa hati hiyo ya rufaa, warufani hao wanadai kuwa, wamefikia uamuzi huo chini ya hati ya dharura kwa sababu jimbo hilo halina mwakilishi tangu matokeo ya uchaguzi yalipofutwa Aprili 30 mwaka jana.
Hukumu ya kutengua ubunge wa Aeshi ilitolewa na Jaji Bethuel Mmila ambapo mwanasheria mkuu anadai kuwa ikiwa rufaa hiyo haitaamriwa, wakazi wa jimbo hilo wataendelea kubaki bila mwakilishi bungeni.
“Tunaiomba Mahakama ya Rufaa itoe amri ya kuifuta hukumu iliyotolewa na Mahakama Kuu ambayo ilimvua ubunge Aeshi, na pia itoe amri ya kuiweka kando amri ya kutekelezwa kwa hukumu ile,” ilieleza hati hiyo.
Miongoni mwa sababu zilizoainishwa na wakata rufani ni kwamba Mahakama Kuu ya Sumbawanga, ilijielekeza vibaya kisheria kupanga tarehe ya kusikiliza na hatimaye kutoa uamuzi katika kesi ya uchaguzi kabla ya mdaiwa wa kwanza (Yamsebo) kuweka dhamana ya gharama (security of Cost).
Aidha, waomba rufaa hao wanadai Jaji Milla alikosea kisheria kuamuru kwamba kutofautiana kwa ushahidi wa mashahidi wanne wa upande wa mlalamikaji, hakukuwa na uzito ambao ungesababisha kuvuruga msingi wa haki.
Aidha, wanadai kuwa jaji alikosea kisheria kusema kwamba kulikuwepo na vurugu katika mikutano ya kampeni ya Yamsebo katika vijiji vya Kisumba na Namtimbwa Septemba 5 na Oktoba 22, mwaka 2010.
Warufani hao wanadai kuwa kutokana na kupingana kwa ushahidi wa mashahidi wanne, jaji huyo alikosea kusema kwamba usumbufu uliotokea katika vijiji hivyo uliathiri mikutano ya kampeni za ubunge wa jimbo hilo.
Pia, wanadai kuwa jaji alijielekeza vibaya kwa kushindwa kuchambua ushahidi uliotolewa kwa kiwango kinachotakiwa cha kuthibitisha pasipokuacha shaka yoyote na matokeo yake alifikia uamuzi ule wa kumvua ubunge Aeshi, ambao wanadai siyo sahihi kisheria.
Mbali na hayo, wanadai kuwa jaji alikosea kisheria kwa kuhamisha jukumu la kuthibitisha kesi kutoka kwa mlalamikaji wa kwanza (Yamsebo) kwenda kwa (Aeshi), kwa madai ya kuwepo kwa rushwa ambayo inadaiwa kutolewa Oktoba 29, mwaka 2010, katika Shule ya Msingi Kantalamba na kuamua madai hayo yalithibitishwa bila kuacha shaka yoyote.
Warufani hao vile vile wanadai kuwa jaji alikosea kuamua kwamba mashahidi wawili wa utetezi walikuwa mawakala wa mlalamikiwa wa pili (Aeshi) na ndio waliotoa hiyo rushwa inayodaiwa huku akijua na kwa idhini yake.
No comments:
Post a Comment