CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimesema kuwa kimepokea kwa masikitiko na majonzi taarifa ya kifo cha mmoja wa viongozi na makamanda wa chama hicho mkoani Kagera, Geofrey Nguma, kilichotokea usiku wa kuamkia juzi.
Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa jana jijini Dar es Salaam na Kurugenzi ya Habari na Uenezi ilieleza Nguma ambaye hadi mauti yanamkuta alikuwa Katibu wa CHADEMA, Jimbo la Karagwe, ameacha pengo katika mapambano ya uhuru na mabadiliko ya kweli.
Taaarifa hiyo ilieleza kuwa, Nguma akiwa mwanachama na kiongozi, alijitolea kwa dhati kuunga mkono moto wa mabadiliko na kuwaongoza wanachama wenzake katika kuwatumikia wananchi wa Karagwe na Tanzania kwa ujumla kupitia CHADEMA.
“CHADEMA itamkumbuka Kamanda Nguma kwa moyo wake thabiti, akijituma muda wote na kujitolea kwa uwezo wake, kukilinda na kukitumikia chama kwa nguvu zake, kwa moyo wake na akili zake, ili kukidhi kiu ya Watanzania kupata utumishi bora kutoka CHADEMA,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.
Taarifa hiyo ilieleza kuwa, CHADEMA kitamkumbuka Nguma kwa namna alivyoshiriki na kusaidia kufanyika kwa mafanikio, mafunzo ya nadharia na vitendo ya wenyeviti na makatibu wa mikoa ya kichama nchi nzima, yaliyofanyika mwishoni mwa mwaka jana wilayani Karagwe, ikiwa ni sehemu ya ratiba ya Vuguvugu la Mabadiliko (M4C).
“Kwa niaba ya CHADEMA, Ofisi ya Katibu Mkuu inatoa pole za dhati kwa familia, Mwenyekiti wa CHADEMA mkoani Kagera, ndugu, jamaa wa marehemu na tunawaombea kwa Mwenyezi Mungu, awapatie moyo wa subira katika wakati huu mgumu wa majonzi ya kuondokewa na mpendwa wao,” ilieleza taarifa hiyo.
No comments:
Post a Comment