Friday, January 18, 2013

Sumaye, Malecela wasigana maoni ya Katiba Mpya


MAWAZI wakuu wawili wastaafu, John Malecela na Fredrick Sumaye, jana walifika mbele ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba kutoa maoni yao huku wakisigana kimtazamo kuhusu madaraka ya Rais.
Wakati Malecela akipendekeza Katiba mpya isiruhusu madaraka ya Rais kupunguzwa, Sumaye alipendekeza utaratibu wa sasa ubadilike ili wakuu wa wilaya na mikoa watakaoteuliwa wasiwe wanasiasa.
Malecela ambaye alikuwa wa kwanza kutoa maoni yake, aliwaeza waandishi wa habari kuwa nchi zinazoendelea zina matatizo hivyo kupunguza madaraka ya Rais si sawa.
Alipendekeza uwakilishi wa wanawake katika Bunge uongezwe kwani Tanzania ilienda Beijing kudai haki na usawa kwa kina mama.
“Unajua wanaopinga viti maalum ni kutokana na watu wanavyochaguliwa na kuchaguana utaratibu ndio sio mzuri ndio maana watu wanapinga,” alisema.
Pia alitaka kuwepo na mabunge mawili ili mambo yachambuliwe kwa uhakika na ufasaha.
Sumaye naye katika maoni yake alisema kuwa kwa vile siasa inakua na huko mbeleni lazima mfumo utabadilika na kuongozwa na vyama vingine vinaweza kuwatoa wote madarakani kwa kuwa ni wanasiasa, hivyo ni vyema eneo hilo liwe la kiutumishi badala ya siasa.
Alisema kuwa kwa suala la Rais hakuna anayetaka madaraka yake yapunguzwe bali yaboreshwe ili kumfanya ang’aare na atakate.
“Sio kila watu ateue na ninachosema hapa si kumpunguzia nguvu ila nafasi za Gavana, Mwanasheria Mkuu, Katibu Mkuu Kiongozi na Jaji Mkuu zipite kwenye ngazi fulani kisha uteuzi wao uthibitishwe na Bunge,” alisema.
Sumaye aliongeza kuwa amependekeza wabunge wasiwe mawaziri japo watu wengine wanadhani litakuwa na gharama lakini itasaidia serikali na Bunge kufanya kazi na kuwaondoa wale wanaotegemea uwaziri kupitia ubunge.
Akizungumzia suala la Muungano, Sumaye alisema ni gumu na kama ingewezekana kungekuwa na sura ya serikali moja lakini kwa sasa ni gumu na kutaka kubaki kama ulivyo.
Alisema kuwa ni vyema ukaboreshwa hasa katika maeneo yenye manung’uniko.
Kwa upande wa serikali tatu, alisema kuwa muungano huo hautadumu kwa sababu uchumi wote utakuwa kwa serikali ya muungano na si Serikali ya Mapinduzi Zanzibar wala ya Tanganyika.
Naye Jaji Mkuu mstaafu, Barnabas Samatta, alitaka kuwepo na chombo kitakachoelimisha kuhusu Katiba.
Kuhusu suala la uteuzi wa viongozi, Samatta alitaka taratibu zibadilishwe ili kuwapata viongozi wazuri na wenye maadili, pia alisema kuwa utaratibu wa kuwapata majaji utazamwe upya ili kuondoa wasiwasi kwa wananchi kuhusu uhuru wa mahakama katika kutenda kazi zake.




Kutoka gazeti la nipashe :-
Mawaziri kutokana na wabunge limezidi kuwa la moto, baada ya Jaji Mkuu mstaafu, Barnabas Samatta, na Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, kuungana na Spika wa Bunge, Anne Makinda, kupendekeza Katiba Mpya ijayo izuie mfumo huo.

Jaji Samatta na Sumaye, walipendekeza hivyo kwa nyakati tofauti, ikiwa ni sehemu ya maoni yao waliyoyatoa kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, jijini Dar es Salaam, juu ya uundwaji wa Katiba Mpya.

Mbali na hayo, Jaji Samatta pia alipendekeza Katiba Mpya itamke namna ya kupata chombo kitakachofanya kazi ya kuwafundisha wananchi katiba ya nchi.

Pia alipendekeza utaratibu wa kupata viongozi mbalimbali wa serikali ubadilike ingawa hakusema namna utakavyokuwa ndani ya Katiba Mpya.

Vilevile, alipendekeza utaratibu wa kuwapata majaji ubadilike ili kutoa manung’uniko yanayotolewa na wananchi juu ya uteuzi wa watumishi hao wa umma.

Kuhusu Muungano, Jaji Samatta alikataa kueleza maoni yake, badala yake alisema suala hilo ni la kisiasa zaidi.

MAONI YA SUMAYE
Sumaye alisema japo watu wengine wanadhani mawaziri kutokuwa wabunge itakuwa na gharama, lakini akasema itasaidia serikali na Bunge kufanya kazi na kuwaondoa wale wanaotegemea uwaziri kupitia ubunge.

Pia alipendekeza Katiba Mpya itamke wakuu wa mikoa na wilaya wasiwe wanasiasa kama ilivyo sasa, badala yake wawe watumishi wa umma.

Alisema kwa kuwa siasa inakuwa na kwamba, katika siku za usoni lazima mfumo utabadilika na kuongozwa na vyama vingine vinavyoweza kuwatoa wote madarakani kwa kuwa ni wanasiasa, ni vyema eneo hilo liwe la kiutumishi badala ya siasa.

Vilevile, alisema hakuna anayetaka madaraka ya rais yapunguzwe, badala yake yaboreshwe ili kumfanya anga’are na atakate.

“Siyo kila watu ateue. Na ninachosema hapa si kumpunguzia nguvu. Ila nafasi za gavana, mwanasheria mkuu, katibu mkuu kiongozi na jaji mkuu nafasi zao zipite kwenye ngazi fulani kisha uteuzi wao uthibitishwe na Bunge,” alisema Sumaye.

Kuhusu Muungano, Sumaye alisema ni suala gumu na kama ingewezekana kungekuwa na sura ya serikali moja, lakini kwa sasa ni gumu, hivyo akataka ubaki kama ulivyo.

Hata hivyo, alipendekeza uboreshwe, hasa katika maeneo yenye manung’uniko.

Kwa upande wa serikali tatu, alisema Muungano huo hautadumu kwa sababu uchumi wote utakuwa kwa Serikali ya Muungano na si serikali ya mapinduzi Zanzibar na ya Tanganyika.

“Ikiwa serikali tatu hali itakuwa tete sana maana Muungano atamiliki rasilimali watu na uchumi na hawa wengine kubaki wakiwa hawana vyote na matatizo yakianza muungano utavunjika, Serikali moja ni nzuri sana lakini hatuwezi kurudi nyuma”alisema.
 
MAONI YA MALECELA


Waziri Mkuu mstaafu, John Malecela, alipendekeza Katiba Mpya itambue mabunge mawili, badala ya moja na kuacha kugusa madaraka aliyonayo rais.

Alitoa kauli hiyo jana alipofika katika ofisi za Tume ya Mabadiliko ya Katiba, jijini Dar es Salaam, kwa ajili ya kutoa maoni yake.

Alisema kuwapo mabunge mawili ni muhimu, hususani kwa nchi zinazoendelea na kwamba, yanasaidia kuchambua baadhi ya mambo kwa undani.

Malecela alisema ametoa maoni kwamba, madaraka ya rais yaachwe kama yalivyo kwa kuwa ni muhimili unaojitegemea. Alihoji kwamba, ikiwa madaraka hayo yatapunguzwa yatapelekwa katika muhimili upi?

“Hapa tunapunguza madaraka ya rais halafu tunayapeleka wapi kwa kuwa mihimili mingine ya Mahakama na Bunge inajitegemea na haiwezi kupelekewa madaraka hayo?” alihoji Malecela.

Alisema kwa nchi changa kama Tanzania, bado kuna haja ya rais kuwa na madaraka makubwa ili kumuwezesha kuisimamia nchi anayoiongoza.

Alipendekeza Katiba Mpya itambue nafasi za viti maalum za ubunge kwa wanawake ili kufikia idadi ya asilimia 50 kwa 50.

Alisema kinacholalamikiwa katika nafasi hizo, ni namna zinavyopatikana, lakini siyo umuhimu wake kwa maendeleo ya taifa.

Wakati Malecela na Sumaye wakitaka madaraka ya rais yasipunguzwe, mapema wiki hii Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, naye alitoa mapendekezo kama hayo na kusema kwamba, unahitajika umakini katika kutekeleza suala hilo.

Balozi Sefue alisema iwapo maamuzi yoyote juu ya suala hilo yatachukuliwa kiholela, kuna hatari rais akashindwa kuwashika Watanzania pamoja kama taifa.

Alisema hayo alipozungumza na waandishi wa habari, jijini Dar es Salaam wiki hii, muda mfupi baada ya kuongoza makatibu wakuu wa wizara, katika mkutano na Tume ya Mabadiliko ya Katiba, kwa ajili ya kutoa maoni juu ya uundwaji wa Katiba Mpya.

Balozi Sefue alisema madaraka ya rais wa nchi kama Tanzania yenye mifumo changa, hayapaswi kudhoofika kwa namna yoyote, badala yake yanatakiwa kuwa imara kwa kuwa ndiye anayehodhi mamlaka ya nchi.

“Hivyo, tusije kumpunguzia madaraka rais kiasi, ambacho akashindwa kutushika pamoja kama taifa. Tusiwe wepesi kusema punguza, punguza madaraka ya rais,” alisema Balozi.
Kabla ya Balozi Sefue na Malecela kusema hayo, tayari baadhi ya makundi katika jamii, wakiwamo wanasiasa, wanaharakati, wafugaji nakadhalika, wamekuwa wakipendekeza kuwapo na udhibiti mkubwa wa mamlaka ya rais.

Katika mapendekezo yao, makundi hayo yanataka pamoja na mambo mengine, rais asiwe na mamlaka ya kuteua viongozi wa mihimili mingine ya dola peke yake na asiruhusiwe kusamehe wafungwa na watuhumiwa.

Pia kila atakayeteuliwa na rais lazima aombe kazi husika kwenye tume huru za kitaalamu na athibitishwe na Bunge, pia rais asiteue Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na asiwe na mamlaka ya ardhi.

JAJI WARIOBA: MAKUNDI 80 YAMESHATOA MAONI
Akizungumzia mchakato wa utoaji wa maoni, Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, alisema hadi sasa makundi maalum 80 yameshatoa maoni.

Alisema kwa siku wastani wa makundi tisa yalikuwa yanatoa maoni yao na kwamba, ifikapo mwisho wa mwezi huu makundi yote yatakuwa yamemaliza kutoa maoni.

Jaji Warioba alisema mwezi ujao Tume itaanza kuchambua maoni yote yaliyotolewa na wananchi na kwamba, baada ya hapo wataandika rasimu ya Katiba Mpya.

Alisema rasimu inatarajiwa kukamilika Juni, mwaka huu, ambayo itapelekwa kwenye mabaraza ya katiba kwa ajili ya kupitiwa. Aliwahakikishia Watanzania kwamba, malengo ya kupatikana Katiba Mpya kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, yatafikiwa kwa kuwa wako ndani ya muda waliopangiwa.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment