Thursday, January 10, 2013

Wanaharakati wawasha moto


Mchakato wa kukusanya maoni ya Katiba Mpya kwa makundi maalum katika jamii, jana uliingia siku ya tatu, huku wanaharakati wa masuala ya jinsia na katiba wakipendekeza mambo mbalimbali, ikiwamo katiba kuwapa wananchi mamlaka ya kuwafukuza kazi viongozi wa kisiasa wanaochaguliwa, kama vile madiwani, wabunge na rais wanaposhindwa kuwajibika kikamilifu.

Pia wamependekeza Rais asiwe na mamlaka ya kuteua viongozi wa mihimili mingine ya dola peke yake na asiruhusiwe kusamehe wafungwa na watuhumiwa.

Vilevile, wamependekeza kwamba kupiga kura katika uchaguzi kufanywe kuwa haki na wajibu wa msingi wa kila raia wa Tanzania mwenye umri wa miaka 18, na kwamba, iwe ni kosa kwa raia yeyote kuamua kwa makusudi kutopiga kura.

Kadhalika, viongozi wa nchi katika nafasi mbalimbali wawe ni raia wa kuzaliwa na siyo wa kuandikishwa, na Katiba Mpya ipige marufuku wake wa marais kuanzisha Asasi zisizokuwa za kiserikali (NG’Os) kila mmoja.

Wanaharakati waliotoa mapendekezo hayo mbele ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba, kwa nyakati tofauti, katika ofisi za Tume hiyo na katika ukumbi wa Karimjee, jijini Dar es Salaam jana, ni pamoja na Mtandao wa Kijinsia (TNGP) na Jukwaa la Katiba Tanzania.

Walitoa mapendekezo hayo, ambayo ni sehemu ya maoni yao kwa Tume, wakitaka yaingizwe kwenye Katiba Mpya, ambayo iko katika mchakato wa kuundwa.


MAONI YA TGNP

Mwenyekiti wa TNGP, Profesa Mery Lusimbe, aliwaambia waandishi wa habari miongoni mwa mambo waliyopendekeza walipokutana na Tume hiyo jana ni pamoja na kutaka Katiba Mpya iwape wananchi mamlaka ya kuwafukuza kazi viongozi wa kisiasa wanaochaguliwa wanaposhindwa kuwajibika kikamilifu.

“Kama diwani, mbunge na rais watashindwa kufanya kazi zao vizuri wananchi wawe na mamlaka ya kuwaondoa madarakani badala ya kusubiri kipindi chote cha miaka mitano kimalizike.”

Alisema maoni mengine waliyowasilisha kwa Tume ni pamoja na kutaka Katiba Mpya itamke na kutambua haki za wanawake na kuzigawanya kwa usawa ili ziweze kuwanufaisha kiuchumi.
 Profesa Lusimbe alisema pia walipendekeza Katiba mpya isimamie usawa wa kijinsia, ikiwa ni pamoja na kuainisha mwanamke ni nani na haki zake ni zipi ili ziweze kuheshimiwa kikatiba.

Hata hivyo, katika hali isiyokuwa ya kawaida, Tume iliwataka TGNP kuandaa maelezo ya ziada ya hoja zao na kuyapeleka tena ili kujenga hoja zenye nguvu maelekezo, ambayo walikubali kuyatekeleza.

JUKWAA LA KATIBA

Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba Tanzania, Deus Kibamba, aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa miongoni mwa mambo waliyopendekeza ni pamoja na kutaka Rais asiwe na mamlaka ya kuteua viongozi wa mihimili mingine ya dola peke yake na pia asiruhusiwe kusamehe wafungwa na watuhumiwa.

Alisema pia walimependekeza kwamba, kupiga kura katika uchaguzi kufanywe kuwa haki na wajibu wa msingi wa kila raia wa Tanzania mwenye umri wa miaka 18, na kwamba, iwe ni kosa kwa raia yeyote kuamua kwa makusudi kutopiga kura.

Kibamba alisema pia wamependekeza viongozi wa nchi katika nafasi mbalimbali wawe ni raia wa kuzaliwa na siyo wa kuandikishwa, na Katiba Mpya ipige marufuku wake wa marais kuanzisha NG’O kila mmoja.

Alisema vilevile wamependekeza Katiba Mpya iweke mfumo wa uwiano wa kura na siyo mfumo wa viti maalum kama ilivyo sasa, pia irihusu matokeo ya urais yaweze kuhojiwa mahakamani kwa kipindi cha miezi sita na kusiwe na wabunge wala madiwani wa kuteuliwa na Rais tena.

Kwa mujibu wa Kibamba, mapendekezo mengine waliyoyatoa ni pamoja na kutaka uteuzi wa wakuu wa mihimili mingine ya dola kuthibitishwa na vyombo vya uwakilishi vya wananchi na wananchi wenyewe.

Alisema kwa mfano, nafasi kama za Jaji Mkuu, Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (Takukuru), Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), wenyeviti wa bodi za mashirika ya umma, walipendekeza zitangazwe kwa uwazi na wananchi waruhusiwe kutoa pingamizi/hoja juu ya wanaoomba nafasi hizo.

Mambo mengine waliyopendekeza ni pamoja na kutaka Rais asiwe na madaraka ya kuteua wabunge na pia asiwe na mamlaka yote juu ya ardhi yote ya Tanzania na kwamba, mamlaka, ambayo yanatakiwa kubakia kwa Rais peke yake ni kuwa mkuu wa nchi na Amiri Jeshi Mkuu wa majeshi ya ulinzi na usalama.

“Ni ukweli usiopingika kuwa madaraka na mamlaka ya Rais hapa nchini ni makubwa mno na yaliingizwa kwenye katiba ya 1962, ambayo uyalimuweka Rais Mfalme kuhusiana na uteuzi wa watendaji na viongozi karibu wote nchini,” alisema Kibamba.

Alisema kwa kuwa kutafsiri sheria na kuhukumu ni jukumu la mahakama, ni kinyume kabisa cha utaratibu kumruhusu Rais anayeongoza mhimili wa dola au serikali kugeuka kuwa jaji wa kutoa msamaha kwa waliopatikana na hatia au walio mahabusu nchini.

Kibamba alisema jambo hilo linafifisha misingi mikuu miwili ya utoaji haki; ukiwamo msingi wa usawa mbele ya sheria, msingi wa kutokuwapo mwingiliano kati ya mahakama na serikali, na kwamba, linahitaji kura ya maoni.

“Inapendekezwa kuwa hata Rais kuwasamehe watuhumiwa wa wizi na ubadhirifu wa mali za umma kwa kuwa wamerejesha fedha walizoiba, nalo likatazwe katika katiba mpya. Uhalifu ni uhalifu na mwenye mamlaka ya kusikiliza mashauri yao na kuamua hatima yao ni mahakama pekee,” alisema Kibamba.

Alisema pia walipendekeza katiba ieleze wazi wabunge kutokuwa mawaziri ili kuondoa muingiliano wa mihimili na kuleta ufanisi katika utendaji wa mihimili ya dola (Serikali, Mahakama na Bunge).

Pia wabunge wasiteuliwe kuwa wakuu wa mikoa wala mhimili mwingine wowote wa serikali, ikiwimo bodi za mashirika ya umma.

Vilevile, katiba izuie ufisadi/uhujumu uchumi na kwamba, mtu akipatikana na hatia ya makosa ya uhujumu uchumi afungwe na afidie uharibifu uliofanyika kwa kufilisiwa mali zake kwa kiwango alichohujumu.

Kadhalika, wanataka katiba iseme rejista ya mali za watumishi wa umma ziwe wazi ili wananchi wote waweze kuzifahamu.

Pia walipendekeza mwenyekiti, makamu mwenyekiti, wajumbe na mkurugenzi wa uchaguzi wapendekezwe na vyama vya siasa, wathibitishwe na kuteuliwa na Bunge na watangazwe na Rais.

Walipendekeza pia kuwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) iwe na ofisi na watumishi katika kila jimbo la uchaguzi nchini na matokeo yote ya uchaguzi, kuanzia wa rais, wabunge, madiwani na viongozi wa serikali za mitaa, yahojiwe mahakamani.

Vilevile, walipendekeza chaguzi zote; yaani Uchaguzi Mkuu na uchaguzi wa serikali za mitaa, zisimamiwe na tume huru ya uchaguzi na kwamba, kuwe na sheria inayoweka mpito wa Rais anayemaliza kuelekea Rais mpya.

Kibamba alisema mpito huo utawezesha mahakama kuamua kama kuna jambo limehojiwa mahakamani na wagombea wengine na kwamba, sheria hiyo inatakiwa itabiri yanayoweza kutokea na suluhu zake na itamke wazi kamati itakayohusika na maandalizi ya uapishaji wa Rais mpya.


MAONI YA JUKWAA LA JINSIA

Mwenyekiti wa Jukwaa la Jinsia lililo chini ya Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania (Tawla), Magdalena Rwebangira, alisema walitoa maoni yao kwa Tume hiyo jana na kwamba, miongoni mwa mambo waliyopendekeza ni pamoja na kuangaliwa kwa maadili katika uteuzi wa majaji, uwezo wa jaji wa kuandika na pia waombe kazi.

Alisema pia walipendekeza mihimili mitatu ya dola kila mmoja ujitegemee.

MAONI YA TPSF 

Nayo Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) imependekeza Katiba Mpya iweke misingi imara itakayosaidia kuleta maendeleo katika uchumi nchini.

Mmoja wa wajumbe wa TPSF, ambaye ni Mwenyekiti wa Shirikisho la Wenye Viwanda Tanzania (TCI), Felix Mosha, alisema miongoni mwa misingi hiyo ni pamoja na utawala bora na kodi zinazozingatia ushiriki wa kila mtu.

Mosha alisema pia wamependekeza rasilimali za nchi lazima ziwe za Watanzania na ziwanufaishe na kwamba, mwekezaji wa nje lazima ashirikiane na Watanzania, uwapo mkakati wa wa kuwaendeleza kiuchumi, badala ya kubaki kuwa watazamaji.

Alisema pia walipendekeza uwekezaji katika ardhi uwashirikishe Watanzania na pia serikali iwe mwangalizi na kusiwapo na sheria itakayoleta ubaguzi wowote wa kijinsia katika umiliki wa ardhi.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment