Thursday, January 10, 2013

CHADEMA wajichimbia kunoa makali


SEKRETARIETI ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), imejichimbia mkoani Kilimanjaro kwa ajili ya kutengeneza mpango mkakati wa namna ya kuendesha shughuli zao kwa mwaka huu.
Itakumbuka kuwa moja ya maazimio ya kikao cha Kamati Kuu kilichofanyika jijini Dar es Salaam mwishoni mwa mwaka jana, iliazimiwa kuwa mwaka 2013 ni wa kutumia nguvu ya umma kuishinikiza serikali ya Rais Jakaya Kikwete, kuwajibika kwa wananachi.
Akizungumza na Tanzania Daima jana, Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa, alisema mpango huo ni sehemu ya mpango mkubwa wa miaka mitano wa chama hicho ulioanza mwaka 2011 na kuendelea hadi 2016.
Alifafanua kuwa kulikuwa na minon’gono kwenye baadhi ya mitandao ya kijamii kuwa baadhi ya wajumbe wakiwamo wabunge wa chama hicho, hawakualikwa kwenye kikao hicho, jambo alilodai kuwa ni uzushi.
Dk. Slaa alisema kuwa wajumbe wasiotokana na sekretarieti walioalikwa ni wale wenye majukumu maalumu ndani ya chama.
“Sisi tuna wabunge 49 na katika kikao hiki wabunge waliohudhuria ni sita, ukimuacha Mwenyekiti wetu, Freeman Mbowe na hawa wabunge wameingia kwa kofia za nafasi zao katika chama,” alifafanua.
Katibu Mkuu huyo aliongeza kuwa mkakati wanaoupanga utafika katika ngazi nyingine za chama hicho kwa uamuzi kabla ya kutekelezwa.
Kwa sasa CHADEMA imejizatiti kwa kile inachokieleza kuwa ni mikakati maalumu ya kuchukua dola kutoka kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mwaka 2015.
Katika kudhibiti hilo, chama kimewataka wanachama wake kuacha kupoteza muda kwa kulumbana juu ya nani awe mgombea urais na badala yake utatengenezwa utaratibu maalumu wa wanachama kutangaza nia.
Hivi karibuni Mwenyekiti wa chama hicho, Mbowe, aliweka bayana kuwa hana mpango wa kuwania wadhifa huo wa urais na badala yake atakuwa na jukumu la kuwafunda wagombea makini watakaopeperusha bendera ya chama hicho kwa nafasi zote za uongozi wa vijiji na mitaa, udiwani, ubunge na urais.

No comments:

Post a Comment