Friday, January 11, 2013

John Mnyika: Sera ya Majimbo ya CHADEMA siri ya Maendeleo

John Mnyika
Kila jimbo litataka kujifananisha na mafanikio fulani fulani.
Dhana ya ushindani na upekee imeshindikana katika mazingira ya sasa ambapo kila halmashauri inaongozwa na maelekezo ya Dar es Salaam na inajivunia mafanikio ya nchi kwa ujumla wake.

Katika kuendeleza dhana hii potofu Profesa Muhongo amejibu tangu wakati wa ukoloni tulikuwa tukiendesha nchi kwa katani na akawataka wananchi wa Mtwara warudishe mapato ya katani.

Profesa Muhongo anapaswa kuisoma historia ya Mtwara toka wakati wa ukoloni atagundua kwamba mikoa ya kusini nayo ilikuwa na nafasi yake katika uchumi na biashara. Huu ni mjadala mwingine, hata hivyo suala la msingi hapa ni umuhimu wa ushindani.

Hata binadamu, ukipewa uhuru wa kujiamulia una uwezo wa kufanya vitu vya pekee zaidi kuliko ukiwa sehemu ya mfumo mpana. Hii ni saikolojia ya maendeleo. Hii ndio falsafa ya nguvu ya umma!

Kupanua vyanzo vya mapato
Majimbo yanapopaswa kujitegemea kwa aina fulani moja kwa moja yanapaswa kuanza kutafuta njia za kujitegemea.

Hii itasaidia vyanzo vya mapato kupatikana. Hii ni kutokana na kanuni ya mwitu (the law of the jungle).

Sasa hivi kila mahali wanaitazama Dar es Salaam ikusanye pesa nchi nzima na kutoka kwa wahisani na kila eneo linaachama mdomo kwa ajili ya kupokea!

Mwaka 2005 wapinzani wa hoja hii walitoa hoja kwamba lipo jimbo ambalo halina rasilimali na walitolea mfano wa jimbo la kusini. Hawa ni watu ambao pengine walikuwa hawafahamu kwamba Tanzania ina rasilimali kila mahali.
Wananchi wengi wamekuwa wakilalamika kuwa mikoa ya kusini haina maendeleo.

Wakati huo tuliwaeleza ukweli ni kwamba tafiti zinaonyesha mikoa ya kusini ina rasilimali na mali asili nyingi sana tatizo kubwa ni miundo mbinu. Tuliwapa mfano kuwa Jimbo la Pwani ya Kusini kwa mfano lina mikoa ya Lindi, Mtwara na maeneo mengine yana rasilimali kama madini, bandari, uvuvi, nishati ya gesi, kilimo cha korosho, mikoko pamoja na utalii.

CHADEMA imeendelea kuwaeleza wananchi umuhimu wa mfumo mpya wa utawala kwani kila jimbo lina rasilimali za kutosha ila kwa kuwa serikali ya CCM imekuwa ikiwahadaa wananchi na kuwafanya wabweteke kisaikolojia ili wasijiletee maendeleo, imekuwa ikipinga vikali serikali ya majimbo.

Baada ya ugunduzi wa ziada wa gesi, sasa hoja imebadilika kutoka kusini haina rasilimali; sasa lugha ni kuwa kusini haipaswi kudai manufaa ya rasilimali hizo kwa kuwa ni za nchi nzima.

Hata kama kungekuwa hakuna maliasili: ukweli unabaki kwamba duniani kote, ziko nchi ambazo hazina maliasili lakini zimeneemeka kutokana na kutoa huduma tu!

Lakini kwa upande mwingine kama sehemu ya sera ya majimbo lipo pato ambalo litakusanywa serikali kuu na kusaidia katika maeneo ambayo yana mapungufu. Hivyo, Prof. Muhongo atambue kwamba hata katika sera ya majimbo, upo mfumo mpya wa utawala ambao unawezesha rasilimali za nchi kutumika kwa manufaa ya Watanzania wote na si Watanzania wa eneo fulani pekee ila mfumo huo unahakikisha hata Watanzania wa maeneo yenye rasilimali wananufaika na rasilimali ambazo Mungu amewajalia katika maeneo yao.

Muundo mpya unaosaidia utekelezaji majukumu
Hapa ni mjadala wa kipi kinaanza muundo ama majukumu (Stucture or function). Sera ya majimbo inachukua mtazamo wa kwamba yote yanakwenda pamoja.

Wachambuzi wengi wamekuwa wakitoa hoja kwamba matatizo ya msingi ya mwananchi ni hali mbaya ya maisha, kipato duni, uchumi mbovu, elimu duni nk.

Na wanachotaka wananchi ni suluhisho la haya matatizo ya msingi sio ‘porojo’ za sera.

Lakini ukweli ni kuwa kuna uhusiano wa moja kwa moja na kimatokeo baina ya masuala haya (Direct and causality relationship). Kwa mfano, asili ya wananchi wa Geita au Kilwa kuwa na uchumi mbovu ni sera mbovu ya madini au sera ya nishati iliyopitishwa na Dar es Salaam lakini pia mfumo mbovu wa mgawanyo wa mapato unaosimamiwa toka Dar es Salaam na kwa hulalishwa na sheria na mikataba mibovu.

Pengine wananchi wa Geita au Kilwa na jimbo lao au kanda yao wanajua zaidi nni ambacho wanataka; sehemu ya tiba ni kuwapa sehemu ya mamlaka ya kujiamulia mambo yao.

Tatizo la elimu pengine ni maagizo ya waziri toka Dar es Salaam ambaye hajui kabisa hali ya Mwanza ni tofauti na Mtwara. Sasa hata elimu aamue waziri Dar es Salaam? Changamoto ya nchi yetu ni wananchi kukosa motisha na hisia za umiliki (Sense of Ownership).

Ujinga, umaskini, maradhi ni matokeo tu, chanzo ni uongozi. Kuweka uongozi bora ni suala moja. Kushughulikia mfumo na muundo wa uongozi/utawala ni sehemu ya suluhisho.

Upo wasiwasi wa kufanya hivi kwamba kuna kutengeneza matabaka. Hata sasa matabaka katika nchi yetu yapo, tena mabaya zaidi.
Maana haya ni ya mtu na mtu. Afadhali utofauti wa kisera kati ya jimbo na jimbo kuliko mtu na jirani yako!

Kuna hofu kwamba yapo majimbo yatakayojitenga. Katika muundo wa Tanzania ya jimbo lenye makabila mbalimbali haliwezi kujitenga ilhali jeshi, mambo ya nje na masuala kadhaa nyeti yako kwenye kapu moja. Huku ni kuhofia kivuli! Huku ni kuyaficha majimbo ambayo ni siri ya maendeleo ya nchi na wananchi.

Kupunguza gharama za uendeshaji wa serikali
Serikali ya majimbo haiongezi ngazi yoyote ya utendaji kwa kuwa inavunja ngazi ya mkoa (ambayo inazidi kuongezwa kila wakati) na kutengeneza ngazi ya jimbo (majimbo ni machache kutegemea na makubaliano ya Kikatiba). 

Wakati huo huo ukubwa wa serikali kuu utapunguzwa kwa kuwa wizara zitabaki chache za mambo ya kitaifa (federesheni) mathalani ulinzi, mambo ya nje, fedha.

Wizara nyingine zote zinakuwa katika ngazi ya majimbo husika kwa mujibu wa utaratibu wa majimbo husika. Kutokana na ukaribu wa utoaji huduma na utendaji mwishowe gharama za utendaji zitakuwa ndogo kuliko Dar es Salaam inavyoendesha nchi mzima katika kila jambo.

Mathalan utoaji wa pasi za kusafiria (paspoti), vibali vya elimu na mambo mengine mengi; serikali ya majimbo itahakikisha mfumo wa utendaji unatukuwa mdogo kwa kujenga mifumo iliyokaribu zaidi. Hii ndio nguvu ya umma!

Msingi wa tisa ni wananchi kunufaika kutokana na matunda ya raslimali za eneo lao.

Mfumo wa sasa ambapo rasilimali zote zinamilikiwa na “Dar es Salaam” kwa maana ya serikali kuu, unafanya wananchi wasinufaike na raslimali za maeneo yao kikamilifu.

Mathalan kodi za madini, mbuga za wanyama n.k. sehemu kubwa inakuja serikali kuu na ama kugawanywa katika mfumo ambao haunufaishi maeneo husika au kutumika katika matumizi ya anasa ya serikali kuu.

Mathalan pamoja na kuchimba madini yenye thamani Geita ni moja ya wilaya maskini kabisa. Wanaofaidi madini ya Geita wako Dar es salaam.

Serikali ya majimbo itakuwa na sehemu ya mamlaka ya ugawanyaji wa mapato yanayotoka katika eneo husika. Pamoja na kukusanya mapato ya pamoja ya serikali kuu. Hii ndio nguvu ya umma!

Na hapa hoja ya ukabila isiingizwe kwa kuwa Watanzania wa maeneo hayo ni watu wa makabila mbalimbali ambao ni wakazi wa maeneo husika. Hali iko hivyo vile vile kwa upande wa gesi asili, ndio maana kabla ya kufafanua kuhusu miradi iliyoanza hivi sasa, Rais na Waziri Muhongo waeleze mapato na manufaa ambayo wananchi wa maeneo husika na nchi kwa ujumla imepata kutoka gesi ilipoanza kuvunwa katika mikoa ya kusini mwaka 2004 na hatua ambazo serikali imechukua mpaka sasa dhidi ya madai ya ufisadi wa baadhi ya viongozi katika mapato ya rasilimali hizo muhimu za taifa.

Serikali ieleze imefikia wapi katika kurejesha kiasi cha dola milioni 20.1 (zaidi ya bilioni 30) zilizopunjwa kifisadi katika mauzo ya gesi asili huku miradi ya maendeleo katika maeneo ambayo gesi hiyo imetoka kama Songosongo na maeneo mengine nchini ikiwa na upungufu wa fedha.

Hatua za kibunge kwa wananchi wa kusini
Kwa upande wangu hata baada ya maandamano na mkutano wa wananchi wa Mtwara walioufanya Desemba 27, 2012 na madai potofu ya Profesa Muhongo ya Desemba 29 2012, nitaendelea kutekeleza kusudio langu nililolieleza Desemba 26 2012 la kutumia kifungu cha 10 cha Sheria ya ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge kutaka nakala ya mkataba wa mkopo wa masharti kiasi cha dola za Marekani bilioni 1.225 (shilingi trilioni 1.86) kutoka China.

Nitataka pia nakala za mikataba ya mradi wa miundombinu ya gesi asilia ambayo itahusisha ujenzi wa mitambo ya kusafishia gesi asilia katika mikoa ya Lindi na Mtwara na ujenzi wa bomba kuu la kusafirishia gesi asilia la inchi 36 kutoka Mtwara kupitia Lindi, Pwani hadi Dar es Salaam lenye umbali wa kilometa 532.

Hii ni kwa sababu mpaka sasa Wizara ya Nishati na Madini haijatekeleza pendekezo nililowasilisha bungeni tarehe Julai 27, 2012 kwamba kutokana na unyeti wa mradi huo. kwa mustakabali wa nchi na maisha ya wananchi wa sasa na baadaye serikali ilipaswa kuwasilisha bungeni na kuweka wazi kwa umma mkataba wa mradi husika kwa manufaa ya wananchi wote.

2 comments: