Juzi Tume ya Mabadiliko ya Katiba ilianza rasmi kupokea maoni ya makundi maalum kwa ajili ya mchakato wa kuandikwa kwa katiba mpya ya Tanzania.
Tume hiyo inayoongozwa na Waziri Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba, ilianza kukusanya maoni ya vyama vya siasa vya Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi na jana ilikuwa inakutana na, UMD, NLD, AFP na CCK katika ofisi zake jijini Dar es Salaam na katika ukumbi wa Karimjee.
Kasoro kubwa ambayo ilijitokeza tangu juzi na jana, ni Tume hiyo kuvizuia vyombo vya habari kuingia na kusikiliza maoni yaliyokuwa yanatolewa na vyama vya siasa bila kuelezwa sababu za msingi za kufanya hivyo.
Kwa maneno mengine, Tume ilikutana na kupokea maoni ya vyama vya siasa katika mkutano wa siri ili umma usijue mambo yaliyowasilishwa kwa ajili ya kuingizwa katika Katiba mpya ambayo inatarajiwa kupatikana mwaka 2014.
Tunashindwa kuelewa ni sababu zipi hasa zimeifanya Tume kutumia njia ya siri katika kukusanya maoni ya makundi maalum ambayo yanawakilisha maslahi ya jamii.
Inashangaza kuona Tume inavizuia vyombo vya habari kusikiliza maoni ya makundi maalum wakati katika mikutano ya hadhara ya kukusanya maoni ya mtu mmoja mmoja katika mikoa yote, vyombo vya habari viliruhusiwa na kuripoti mambo yaliyozungumzwa na umma
ukaelewa yaliyozungumzwa!
Tume hiyo tangu ilipoanza kutekeleza majukumu yake baada ya wajumbe wake kuteuliwa na kuapishwa na Rais Jakaya Kikwete, ilikuwa ikivishirikisha vyombo vya habari kwa kueleza kila hatua iliyokuwa inatekelezwa ikiwamo changamoto na mafanikio katika mchakato wa kukusanya maoni ya wananchi.
Itakumbukwa kuwa Jaji Warioba, amekuwa akisisitiza kuwa Tume yake itatekeleza majukumu yake kwa uhuru kwa maana ya kutoingiliwa na mtu au kikundi chochote pamoja na uwazi. Uwazi huo uko wapi?
Kitendo cha Tume kuwazuia waandishi wa habari kuingia katika kumbi za mikutano wakati vyama vya siasa vilipokuwa vinatoa maoni bila kueleza sababu za maamuzi hayo, kinaacha maswali mengi kuliko majibu. Kitendo hicho kinaweza kutafsiriwa vibaya; kwamba Tume hiyo siyo huru na inatekeleza majukumu yake kwa kupewa maelekezo.
Maofisa hao waliwazuia waandishi wa habari kuingia ndani ya kumbi ambazo mikutano hiyo ilikofanyikia kwa maelezo kwamba wamepewa maelekezo hayo na viongozi wao.
Kitendo hicho kiliwafanya waandishi wa habari kulazimika kusubiri nje ya kumbi hizo kupata kutoka kwa viongozi wa vyama vya siasa kilichojiri kwenye mikutano yao na Tume.
Maelezo yaliyotolewa na viongozi wa Tume hayana hoja za msingi za kushawishi kuhusu sababu za kuwazuia wanahabari.
Jaji Warioba alisema walishindwa kuwaruhusu waandishi kuhudhuria mikutano hiyo kutokana na kumbi za mikutano kuwa finyu wakati Naibu Katibu wa Tume hiyo, Casmir Kyuka, alisema kuwa ni utaratibu wa Tume kwamba wanapokutana na makundi, yakiwamo yanayohusisha vyama vya siasa, hawafanyi mikutano ya wazi.
Hata hivyo, hatua ya jana ya Jaji Warioba kutangaza rasmi kuwa vyombo vya habari havitaruhusiwa kuhudhuria vikao vya Tume na makundi maalum bila kueleza sababu, inatushawishi kuelewa kwamba kuna kitu.
Kimsingi, maamuzi ya Tume kuvizuia vyombo vya habari kusikiliza maoni ya vyama vya siasa, ni kuwanyima wananchi haki ya kupata habari kuhusu mchakato wa Katiba.
Matokeo yake ni kuwa kuna uwezekano wa maoni yaliyotolewa na vyama kupotoshwa ikiwa waandishi watasubiri kupewa taarifa za upande mmoja wa vyama vilivyotoa maoni bila umma kujua Tume ilivyoyapokea maoni hayo.
Ushauri kwa Tume ni kuwa ijitathmini upya kuhusiana na utaratibu wa kupokea maoni ya makundi maalum ili kujenga mazingira ya uwazi baadaye kuondoa uwezekano wa kuzuka kwa malalamiko yasiyo ya lazima dhidi ya Tume.
Mwanafalsafa mmoja wa kale aliwahi kusema kuwa mawasiliano katika taasisi ni muhimu sana kama damu katika mwili wa binadamu na taasisi isiyo na mfumo mzuri wa mawasiliano haiwezi kudumu.
Tume haina budi kujisahihisha kwa kuvitumia vyombo vya habari kwa uwazi katika mchakato mzima, vinginevyo jamii itashindwa kuielewa na kuiamini.
Moja ya vyama vikuu vya siasa nchini hivi karibuni kilidai kuwa kina wasiwasi na mchakato wa Katiba mpya na kudai kuwa Katiba imeshaandikwa na kundi fulani isipokuwa mchakato unaoendelea sasa ni wa kuthibitisha kuwa Watanzania wote walihusishwa.
Tume isikubali usiri utawale mchakato huo kwa kuwa hali hiyo baadaye inaweza kuthibitisha madai kuwa Watanzania hawakushirikishwa.
CHANZO: NIPASHE

No comments:
Post a Comment