1. KATIKA makala zilizotangulia tuliona namna ambavyo CHADEMA kupitia kwa viongozi wake na hasa wabunge ilivyosimamia msingi wa ‘kulinda rasilimali za nchi.’
Tuliona mfano wa ndugu Halima Mdee na suala la Ardhi alilofanikisha kulipitisha Bungeni na kuungwa mkono na wabunge wote licha ya itikadi za vyama.
Tumeona pia msingi wa vita dhidi ya ufisadi ambapo tuliona mfano wa Dk. Willibrod Slaa katika kupambana na wezi katika Benki Kuu ya Tanzania kupitia akaunti ya EPA.
Vile vile tumeona msingi wa ujenzi wa chama kama Taasisi kwa nguvu za mwenyekiti wa tatu wa chama, ndugu Freeman Mbowe, pamoja na timu ya uongozi wa chama.
Tuliona jinsi timu ya CHADEMA ilivyojigawa na kujipanga katika kampeni za uchaguzi wa Arumeru na chaguzi za udiwani kulionesha mbele ya macho ya Watanzania namna ya taasisi inayoitwa CHADEMA inavyoweza kushirikiana na kugawana majukumu.
Haya yote yaliwezekana kwa sababu ya ufuasi wa misingi ya chama badala ya ufuasi wa watu. Leo tunazumgumzia msingi wa umoja na msingi wa kuwatetea wanyonge kama silaha za ushindi katika chaguzi na tunatoa mifano wa ushindi wa chaguzi ndogo za mwaka jana.
2. Katika majira ya joto ya mwaka 64 Kabla ya kuzaliwa Kristo (BC), Marcus Tullius Cicero alikuwa anagombea nafasi ya juu kabisa ya uongozi (Consul) katika Jamhuri ya Roma.
Kaka yake Marcus aitwaye Quintus alimwandikia nduguye mkakati wa kushinda uchaguzi ule. Ingawa mapendekezo mengi sana ya Quintus kwa Marcus ilikuwa ni mikakati ya kushinda kwa gharama yeyote ile bila kujali maadili (kama ilivyo sasa kwenye chaguzi nyingi sana nchini), mkakati mmoja ni wa kuzingatia sana – Hakikisha wenzako wanakuunga mkono.
Ingawa wakati ule hapakuwa na vyama vya siasa tunaweza kutafsiri nino ‘wenzako’ leo kwamba ni pamoja na wanachama wenzako wa chama cha siasa ulichomo kwa wingi wao na uchache wao, ndugu zako, marafiki zako na makundi mbalimbali ya kijamii katika eneo unalogombea nafasi ya uongozi. Huu ni msingi wa umoja na mshikamano katika chama.
Kuanzia mwaka 2007 mpaka 2012 kumekuwa na chaguzi ndogo za ubunge katika majimbo ya Tunduru, Kiteto, Tarime, Mbeya Vijijini, Busanda, Biharamulo magharibi, Igunga na Arumeru Mashariki. Kulikuwa na makumi ya chaguzi za udiwani katika kipindi hicho.
Hata hivyo, chaguzi mbili za Ubunge zilikuwa zina msisimko wake – Tarime na Arumeru Mashariki. Wakati Tarime CHADEMA ilikuwa inatetea kiti, Arumeru ilikuwa ni kiti cha mpinzani wetu CCM.
3. Wakati CCM ilipata mgombea wake kwa namna ambayo iliwaacha wamepasuka makundi yanayohasimiana, CHADEMA ilipata mgombea wake kidemokrasia isiyokuwa na rushwa na wanachama wote kushikamana nyuma ya mgombea mmoja.
Msingi huu wa umoja na mshikamano ulikuwa ni silaha kubwa sana ya ushindi kwa chama kupitia mgombea wetu kijana wa miaka 26 tu, lakini mwenye uwezo mkubwa wa kujieleza na kujenga hoja, Ndugu Joshua Nassari.
Mara baada ya mgombea kupatikana CHADEMA kwa njia ya kidemokrasia, haikuwa na kazi ya kuanza kuponya majeraha ya makundi, bali moja kwa moja ilianza kuweka mikakati ya kufanya kazi kwa pamoja na kwa ushirikiano kuleta ushindi.
Wabunge, madiwani,viongozi wa chama wa ngazi mbalimbali na wanachama wa kawaida kutoka pande mbalimbali za nchi walijigawa katika vijiji na kata zote za jimbo la Arumeru Mashariki kwa kazi moja tu -Ushindi.
Hali ilikuwa hiyo hiyo kwa viongozi waliokwenda kushiriki kuleta ushindi kwenye kata mbali mbali zilizokuwa zinagombewa nafasi ya udiwani.
4. Katika uchaguzi mdogo wa Arumeru CHADEMA ilifanya uamuzi mkubwa na wa kimkakati kutoa tafsiri yake ya uchaguzi ulena.
Uamuzi wa CHADEMA kuwa na tafsiri yake mahususi ya uchaguzi na kuileza kwa umma kuliitofautisha na CCM.
Wapinzani hawa walijikuta hawana wanachopigania zaidi ya kuonesha ufuasi mkubwa wa watu na kupiganiakutunza heshima ya chama na familia ya mgombea wao.
Kwa kukosa tafsiri ya uchaguzi ule CCM ilijikuta ikitoa matusi tena matusi ya nguoni dhidi ya viongozi wa CHADEMA ambao wala hawakuwa wagombea katika uchaguzi ule.
Viongozi wakubwa kabisa walioshika dhamana ya nchi walijiingiza katika mjadala wa kujadili vitu kama nani ni mtoto wa Nyerere nani sio.
Zilifanyika siasa za masuala la majawabu ya masuala dhidi ya siasa za matusi, kebehi na vitisho. Masuala haya hayakuwa kwenye ajenda ya wananchi wa Arumeru.
Washindani wetu wa CCM walichelewa kuona hatari ya hoja ya Ardhi na walipoanza kutoa ahadi mbalimbali za kumaliza kero ya Ardhi kwa wananchi hawakuichagua na badala yake wakamchagua kwa kura nyingi sana ndugu Joshua Nassari kuwa Mbunge wa Jimbo Lao.
CHADEMA ilicheza vizuri karata zake kwa kujiegemeza kwa masuala ya wananchi na namna ya kutatua kero zao. Sasa Nassari lazima aibebe ajenda Ardhi.
Hana namna ni lazima awe sauti ya wananchi masikini waliofukarishwa na mfumo mbovu wa kugawa Ardhi ulioanzishwa wakati wa ukoloni na kuendelezwa chini ya Uongozi wa CCM.
Tangu mwanzo kabisa, CHADEMA ilisema katika uzinduzi wa kampeni za uchaguzi mdogo wa Arumeru Mashariki “Uchaguzi wa Ubunge Arumeru Mashariki ni kipimo cha namna wananchi mnavyoridhika na watawala, namna mnavyoridhika na mgawo wa Ardhi na namna mnavyoridhika na mgawanyo wa Maji katika Wilaya yenu.”
Muda wote wa kampeni ujumbe kwa wananchi ulikuwa mmoja na wenye kukonga nyoyo zao. Pamoja na kwamba wapiga kampeni waliweka maneno mengine ya kukoleza kampeni, lakini mgombea alielezea kwa ufasaha namna anavyoyajua matatizo ya Arumeru, alivyoyaishi na atakavyo yashughulikia pindi akipewa ridhaa ya kuwawakilisha.
5. Chaguzi zote mbili ziliweka rekodi yake. Arumeru Mashariki ilikuwa ni jimbo la kwanza kuchukuliwa na chama cha upinzani katika uchaguzi mdogo katika kipindi cha miaka 15 na kwa mara ya pili tu tangu mfumo wa vyama vingi uanze (rejea ushindi wa chama cha UDP jimbo la Busega mwaka 1997), Tarime CHADEMA ilivunja nuksi ya chama cha upinzani kupoteza chaguzi ndogo kwa muongo mzima mfululizo.
Kwa upande wa chaguzi za madiwani, chama cha CCM kilikuwa kikizoa viti vya udiwani kwa zaidi ya theluthi mbili ya viti vinavyogombewa, lakini katika uchaguzi wa mwezi Machi mwaka 2012 kwa mara ya kwanza CCM ilipoteza zaidi ya nusu ya viti vilivyokuwa vinagombewa.
CHADEMA ilinyakua viti vya udiwani katika Mikoa ya Ruvuma, Mbeya na Mwanza na kuonesha kuongezeka kwa kukubalika kwa chama nchi nzima.
Kama chaguzi ndogo za Machi mwaka 2012 ilikuwa ni ‘kura ya maoni’ dhidi ya chama tawala, ni dhahiri chama hicho kilikataliwa na wananchi kila kona ya nchi.
Kama tulivyosema katika makala ya kwanza kabisa ya “fuata misingi,” kulinda rasilimali za nchi ni moja katika misingi ya Chama na kilizingatia hilo katika kuunda ajenda yake.
Kilizingatia pia msingi wa umoja wa wanachama katika muda wote wa kampeni, na hatimmae kufanikiwa.
Siri ya mafanikio haya ya CHADEMA kiuchaguzi na kimpangilio ni misingi ya chama, misingi inayoisimamia na kuijenga.
Chama kinapoweka pembeni tofauti za kimtazamo au za kibinafsi na kujikita katika msingi wa chama kinapata urahisi sana kushinda.
Chama ambacho kinaendekeza tofauti binafsi miongoni mwa wanachama au viongozi au kutokana na ugomvi wa madaraka au woga na chuki au maslahi binafsi kinapoteza mshikamano wa kusuka watu pamoja na kupigania ushindi. Tuone mfano wa kilicho endeleaa jijini Mwanza.
6. CHADEMA ilitumia msingi wa kumtetea mnyonge kushinda uchaguzi wa kata ya Kirumba, Mwanza. Iwapo CCM ingeshinda kata ile wangeweza kuchukua Umeya wa Jiji la Mwanza. CHADEMA ikaeleza wananchi madhara ya kurejesha Jiji kwenye mikono ya CCM wananchi wakaelewa.
Wananchi wakatupa ushindi mkubwa. Ushindi ule ulikuwa na damu maana Mbunge wetu wa Jimbo la Ilemela Highness Kiwia alipigwa mapanga na kuumizwa vibaya sana alipokuwa kwenye juhudi za kulinda ushindi wa chama.
Bahati mbaya, nyufa za ufuasi wa watu na maslahi binafsi zilianzakujionyesha katika chama na hata kupoteza mafanikio ya ushindi wa Machi mwaka 2012.
Baada ya ushindi na baada ya CCM kugawa Halmashauri zile, takribani kila diwani akataka kuwa Meya, wakisahau misingi ya ushikamano uliotufanikisha katika chaguzi ndogo.
Ufuasi wa watu na maslahi binafsi ukawa na nguvu zaidi ya ufuasi wa misingi ya chama ambayo ni kutumikia wananchi.
Leo CHADEMA imekosa vyote, haina Umeya wa Jiji la Mwanza wala Manispaa ya Ilemela.Ufuasi wa watu umesaliti hata damu yetu sisi wenyewe, umedharau mamlaka ya watu na heshima waliyotupa.
Mfano huu wa pili unaonesha jinsi ambavyo ufuasi wa watu hutokana na faida za kimaslahi binafsi badala ya ukombozi wa wananchi wanyonge. Watu wanayumba, misingi hubakia.
7. Ufuasi wa watu unaua mshikamano ndani ya chama, kuzalisha makundi/kutengeneza makundi bandia na kupoteza malengo kutoka kupambana na adui kwenda kupambana wenyewe.
Ufuasi wa misingi (values) hubakiza chama salama na kukipeleka mbele kwani kila mnapopotoka misingi itawarudisha kwenye malengo.
No comments:
Post a Comment