Wednesday, January 9, 2013
Vyama vyataka uundwaji wa wizara 15
VYAMA vya siasa vimeendelea kutoa maoni mbele ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba, huku baadhi ya vyama hivyo vikitaka kuwepo na wizara 15 badala ya 26 zilizopo sasa.
Vyama hivyo vilitoa maoni yao jana jijini Dar es Salaam, wakati tume inayosimamiwa na Jaji Joseph Warioba kama mwenyekiti ikiendelea kupokea maoni hayo.
Vyama hivyo pia vilieleza kuwa kama utawala wa mikoa utaimarishwa na madaraka kugawiwa hakutakuwa na umuhimu wa kuwa na wizara nyingi kama ilivyo sasa.
Aidha vyama hivyo pia vimetaka Rais aondolewe kinga ya kutokushtakiwa ikiwepo kupunguziwa madaraka ya kuteua wabunge, na mawaziri.
Pia walitaka Katiba hiyo itambue udini ikiwemo kuundwa Baraza la Dini ili kuokoa mivurugano inayotokea mara kwa mara.
Vyama hivyo pia vilitaka kuwepo kwa Tume Huru ya uchaguzi ili kuondokana na tume iliyopo sasa waliyodai kuwa na ukiritimba.
Pia vyama hivyo vilitaka ruzuku itolewe kwa vyama vyote bila kuangaliwa uwakilishi bungeni na uhuru wa vyombo vya habari katika kutekeleza majukumu ya kazi.
Chama cha Wakulima (AFP) kilipendekeza Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) ligawanywe sehemu mbili kuwepo na jeshi la vita na la maendeleo ambalo litaungana na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).
Pia walipendekeza umri wa mpigakura kuwa miaka 18 na mwisho wa kupiga kura miaka 80, kwa upande wa uchaguzi wa Rais na wabunge uwe unahitimishwa kila baada ya miaka kumi na serikali za mitaa miaka nane.
Kwa upande wa Chama cha National League for Democracy(NLD) kupitia mwenyekiti wake, Dk. Emanuel Makaidi, kilieleza kuwa uundwaji wa Katiba hii sio mpya bali wanarekebisha Katiba ya zamani.
“Kwanza huko ndani (akimaanisha alikotoa maoni) nimewaambia kuwa wasiseme tunatengeneza Katiba mpya siyo mpya bali inaboreshwa na nilichohoji walewale walioharibu Katiba ya awali ndio haohao wanaosimamia na kuongoza upatikanaji huu wakitaka mpya ipatikane basi kungekuwa na mkutano wa taifa; wanaongopea watu sio Katiba mpya hii,” alisema.
Pia walitaka elimu ya msingi, sekondari na chuo iwe ya lazima.
Maoni hayo yametolewa na vyama vitatu, NLD, CCK na AFP; Tume ya Mabadiliko ya Katiba inaendelea kupokea maoni ya makundi maalumu hadi Januari 25, mwaka huu.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment