KATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa, amesema ni wazi kuwa Jeshi la Polisi limeamua kumlinda Ramadhan Ighondu na wenzake wa Idara ya Usalama wa Taifa (TISS).
Kauli ya Dk. Slaa inakuja siku chache baada ya Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Saidi Mwema, kudai kuwa wameshindwa kutoa taarifa za suala la mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari Nchini, Dk. Steven Ulimboka, kwa kuwa ni siri ya taifa.
Wakati IGP Mwema akidai hivyo, jeshi hilo pia lilitangaza kuwa linamsaka Dk. Ulimboka na hivyo kumtaka wakili wake, Nyaronyo Kicheere, awasaidie kumpata.
Akizungumza na gazeti hili jana, Dk. Slaa alisema kuwa kama ni kweli kauli ya IGP ni kwamba sakata hilo ni siri ya taifa, polisi watakuwa wanawalinda watumishi wa TISS na Rais Jakaya Kikwete.
Alihoji kuwa kama uhai wa Mtanzania ni siri ya taifa, sasa taifa ni nini? Alidhani taifa ni Watanzania mmoja mmoja kwa umoja wao kumbe taifa ni Rais Jakaya Kikwete.
“Kumbe Taifa ni Kikwete ambaye kimsingi nilidhani ni mtumishi wa Watanzania aliyepewa dhamana ya kuwalinda na mali zao. Maajabu!” alisema Dk. Slaa.
Oktoba 17 mwaka jana, Kicheere alisoma tamko la Dk. Ulimboka kwa niaba yake, likieleza jinsi alivyotekwa, kuteswa na kutupwa kwenye msitu wa Mabwepande usiku wa June 26 mwaka jana pamoja na watuhumiwa aliyodai walihusika.
Katika tamko hilo, Dk. Ulimboka alisema kuwa tukio la kutekwa kwake, kusukumizwa kwenye gari, kupigwa, kufungwa mikono na miguu, kunyofolewa kucha na kutolewa meno, lilitokea wakati akiwa na kikao na ofisa aliyetambulishwa kwao kuwa ni ofisa wa Ikulu, Ramadhan Abeid Ighondu.
“Nathibitisha kwamba Ramadhan Ighondu alitambulishwa kwetu kwa jina la Abeid. Binafsi ninamfahamu sana bwana huyu kwa sababu alikuwa akitumwa mara kwa mara kuja kukutana na mimi na tumekutana mara kadhaa kabla ya tukio lile,” lilisomeka tamko hilo na kuongeza: “Nakumbuka kuwa Abeid alitambulishwa kwetu na kigogo mmoja, nikiwa pamoja na wawakilishi wengine wa madaktari kuwa yeye (Ramadhan Ighondu) ndiye atayehusika katika kuchukua madai na hoja za madaktari katika mgogoro kati ya madaktari na serikali.
“Nathibitisha kwamba mfanyakazi huyu wa Ikulu, ndiye aliyenipigia simu na kuniita kwenye kikao ambako muda mfupi baadaye nilitekwa. Katika mawasiliano hayo, Abeid alikuwa anatumia simu Na. 0713 760473,” alisongeza Dk. Ulimboka kupitia tamko hilo.
Hakuna mashaka kuwa anamtambua Abeid kwa sura na namba aliyokuwa anatumia kuwasiliana naye mpaka siku ya kutekwa kwake. Ni namba hiyo hiyo iliyoandikwa na gazeti la MwanaHalisi.
“Katika mawasiliano hayo, mimi nilikuwa natumia simu 0713 731610 na kwamba mimi naamini kwa dhati kuwa ofisa huyo wa Ikulu bado yuko hai na mimi na wenzangu tuko tayari kutoa ushirikiano kwa chombo huru kuhakikisha haki inatendeka,” alisema.
Aliongeza kuwa kwa nyakati tofauti Abeid alitumwa kwake kukagua/ kuchukua nyaraka zake mbalimbali ikiwa ni pamoja na vyeti kwa ajili ya uthibitisho wa taaluma na masomo yake.
Hadi sasa mtuhumiwa pekee anayedaiwa kuhusika katika tukio hilo raia wa Kenya, Joshua Mulundi, ndiye aliyefikishwa mahakamani kujibu mashtaka ya kutaka kumuua Dk. Ulimboka.
Katika siku za hivi karibuni, mtuhumiwa huyo amekuwa akitoa malalamiko ya kutaka upelelezi wa kesi yake uharakishwe ili atendewe haki na kutaka adhaminiwe.
Licha ya Dk. Ulimboka kumtaja mtuhumiwa huyo aliyedai ni wa Ikulu, jeshi la polisi halijawahi kumhoji mtu huyo kubaini ukweli, badala yake sakala hilo limekuwa mithili ya mchezo wa kuigiza kutokana na kauli tata zinazotolewa na viongozi wa jeshi hilo.
Dk. Ulimboka juzi alizungumza na gazeti hili na kusema kuwa ameshangazwa na kauli ya polisi kuwa wanamtafuta, akidai haishi mafichoni, simu yake inajulikana na anapatikana wakati wote.
No comments:
Post a Comment