Maandamano na mihadhara ya kutoa matamko kuhusu suala la gesi asilia ambayo Serikali ya Tanzania imenuia kuisafirisha kutoka mikoa yenye (au inayopakana) na maeneo yanye rasilimali hizo ni ishara tosha kuwa wananchi wanapaza sauti ili mawazo yao yasikilizwe na viongozi.
Wananchi hawa wanapokosa fursa rasmi na sahihi ya kuwasilisha makusudio yao, si jambo geni kuona kuwa watatumia njia yoyote iliyobaki ili wasikike.
Yumkini, Serikali yetu inatokana na watu katika jamii ambao waliona wana uwezo wa kuchagiza maendeleo, hivyo wakajitokeza kuomba ridhaa ya kuwasilisha mawazo ya watu na/au kuwawakilisha watu kutoka katika makundi na maeneo mbalimbali.
Ni dhahiri kuwa, ili watu waendelee kuamini kuwa uwakilishi wao unafanyika sawia, basi mawazo yao na maoni yao hayana budi kupewa kipaumbele kwa kusikilizwa na kutolewa maafikiano ya ni ipi njia bora ya kuchagiza maendeleo hayo hasa pale suala la rasilimali linapohusika.
Mikoa ya Lindi na Mtwara wamepaza sauti zao kuonesha kuwa ama hawajaridhika na uwiano wa kimaendeleo unaoonekana nchini Tanzania, iwe ni kwa sababu zilizo dhahiri ama za kufikirika, lakini kwa ujumla wanapingana na mpango wa Serikali wa kusafirisha rasilimali yao kwenda kwingineko.
Ikiwa ni Serikali imezembea kutoa elimu sahihi kuhusu mpango wake, ama ikiwa ni baadhi ya watu wameweza kutoa elimu potofu kwa wananchi wa Mtwara, bado kunahitajika vikao baina ya Wananchi na Viongozi wa Kiserikali ili kujadili tofauti zinasosababisha mvutano ili kuweza kufikia muafaka wa faida na hasara zinazogombewa na kila upande.
Huenda nia ya Wananchi wa ukanda wa Kusini wanaona yale yale yaliyotokea katika mikoa ambayo ina rasilimali za kutosha, maendeleo yao hayaendani na thamani ya rasilimali zilizopo katika maeneo hayo na hivyo wanahofia yayo hayo ndiyo yatakayowapata.
Huenda Wananchi hawa wanaona rasilimali chache zinazopatikana kwenye maeneo yao hadi sasa hazijaweza kuwaletea maendeleo yaliyokusudiwa, kwa hivyo wanaingiwa na hofu kuwa rasilimali hii ikiwaponyoka, wataendelea kupoteza zaidi. Ikiwa wananchi wa mikoa inayodhaniwa kuwa imeendelea kiuchumi hawakuhoji na/au kutoa maoni ya jinsi amavyo wanadhani matumizi ya rasilimali zinazotoka kwenye maeneo yao zigawanywe, hilo haliwaondolei haki wananchi wa mikoa inayohoji wakati huu kuhusu matumizi, mgawanyo na faida ya rasilimali zinazowazunguka.
Huenda Wananchi wa maeneo haya wana taarifa potofu kuhusu maendeleo ya baadhi ya mikoa kwa nadharia ya upendeleo, pasina kujifunza na kujua watu wa maeneo yanayosadikiwa kuwa yameinuka kiuchumi, ni jitihada gani za kusukumana binafsi walijiwekea hadi kufikia walipofika.
Lakini la zaidi sana, ni kuwa nyakati na majira hubadilika. Huenda wananchi wa Kusini wanazo mbinu na maarifa zaidi za jinsi ya kuitumia rasilimali hii kwa faida ya wote.
Hivyo basi, ni vyema na sahihi kabisa kwa Serikali sikivu, kufanya jambo la mbolea kwa kuwasikiliza Wananchi wake, kujadiliana, kukubaliana na kuwekana sawa katika tofauti zilizopo, hata ikiwa wana itikadi zinazotokana na vyanzo mbalimbali iwe kidini au kisiasa, mwanadamu yeyote aliyekuzwa katika mazingira hayo lazima atakuwa na itikadi, hoja siyo kujadili itikadi, bali yatokanayo na itikadi hizo na kama yana msingi wowote wa kimaendeleo kwa jamii nzima.
Ni hatari kwa ulimwengu wa sasa kuamini kuwa inawezekana kuwalazimisha watu wakubali jambo, bila ya wao kuhoji, “kwa nini?”. Wananchi wanayo haki ya kuhoji, kusikilizwa, kupewa ufafanuzi na majibu kwa hojaji zao. Kinyume na hapo ni kukaribisha hujuma kwa miradi ya Serikali na tafaruki isiyo na sababu za msingi.
---
Subi
AMBAYE AMEFUATILIA HISTORIA YA SOMALIA ESPECIALLY MZEE EDWIN MTEI AMBAYE PIA ANAMFAHAMU MIKHAIL GORBACHOR ALIIFANYA NINI USSR NA BAADA YA DHAMBI HIYO DUNIA IMEINGIA KWENYE ANGAMIZI LA UTANDAWAZI ULIOJENGA MATABAKA MAWILI DUNIANI MATRIONELLER WACHACHE SANA WAKIISHI PEPONI DUNIANI NA MABILIONI YA MASIKINI WA DUNIA WAKIISHI JEHANAMU DUNIANI WANACHOSHABIKIA CHADEMA NI KUIVUNJA TANZANIA VIPANDE VIPANDE KWAO DUNIA NI UWANJA WA FUJO WANATAKA WAKIRUDI KUZIMU WASIFIWE KWA KUFANYA FUJO NA KUONDOKA WAKAACHA DUNIA IKIWAKA MOTO
ReplyDelete